1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Ukraine, watoa onyo kwa serikali

23 Januari 2014

Upinzani nchini Ukraine umetishia kufanya mashambulizi leo, hadi hapo serikali itakapofikia makubaliano ya kusitisha mapambano ambayo yamesababisha vifo vya wanaharakati watano.

https://p.dw.com/p/1Avw4
Waandamanaji wakipambana na polisi mjini Kiev
Waandamanaji wakipambana na polisi mjini KievPicha: Reuters

Vifo hivyo ni vya kwanza tangu kuzuka kwa maandamano ya kuipinga serikali miezi miwili iliyopita. Waandamanaji na polisi nchini Ukraine wamepambana tena mapema leo (23.01.2014), baada ya ghasia kuzuka hapo jana Jumatano na kuigeuza sehemu ya katikati ya mji mkuu, Kiev kuwa uwanja wa vita, huku polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe.

Vifo hivyo vimezusha hofu mpya baada ya miezi miwili ya maandamano ya kuipinga serikali yaliyochochewa na hatua ya serikali kutosaini makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara na Umoja wa Ulaya, kutokana na shinikizo la Urusi.

Upinzani watoa onyo

Viongozi wa upinzani, akiwemo bingwa wa zamani wa ndodi, Vitali Klitschko, wameanzisha mazungumzo na Rais Viktor Yanukovych na wanatarajia kukutana leo, huku madai makubwa yakiwa kuitishwa kwa uchaguzi wa mapema.

Kiongozi wa upinzani, Vitali Klitschko
Kiongozi wa upinzani, Vitali KlitschkoPicha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Fatherland, Arseniy Yatsenyuk, aliwaonya waandamanaji katika Uwanja wa Uhuru kwamba Rais Yanukovych ana hadi saa 24 za kukubaliana na upinzani kuhusu suluhisho la kupatikana amani, akisema yuko tayari kufa kwa sababu hiyo.

Klitschko aliuambia umati uliofurika katika uwanja huo, kwamba waandamanaji watafanya mashambulizi kama Rais Yanukovych hatotoa nafasi ya kufikiwa makubaliano. Picha za televisheni zimeonyesha polisi wa kikosi maalum kinachojulikana kama Berkut, wakiwa katika mtaa wa Grushevsky katikati mwa mji mkuu Kiev, huku mamia ya waandamanaji wakikabiliana nao.

Mratibu wa huduma za matibabu, Oleg Musiy, amekiambia kituo cha redio cha upinzani kuwa watu watano waliuawa katika ghasia za jana Jumatano na wengine kiasi 300 walijeruhiwa. Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Ukrainska Pravda, watu wanne kati ya watano waliouawa, walikutwa na majeraha ya risasi.

Urusi kutoingilia kati ghasia za Ukraine

Wakati huo huo, Urusi imesema haitaingilia kati ghasia zinazoshika kasi nchini Ukraine na kwamba inaamini uongozi wa nchi hiyo utatafuta suluhisho la mzozo huo.

Rais Viktor Yanukovych akiwa na Rais Vladmir Putin
Rais Viktor Yanukovych akiwa na Rais Vladmir PutinPicha: Reuters

Msemaji wa Rais Vladmir Putin, Dmitry Peskov, amesema hawana haki kwa namna yoyote ile kuingilia kati masuala ya ndani ya Ukraine na kwamba Urusi haijawahi kufanya hivyo na haitafanya hivyo.

Jana Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, alitoa wito wa kusitishwa kwa ghasia nchini Ukraine na kuonya kuwa Kamati Kuu ya Umoja wa Ulaya itatathmini uwezekano wa kuichukulia hatua.

Barroso alisema wameshtushwa na taarifa za kuuawa kwa wanaharakati waliouawa wakati polisi walipoivamia kambi moja ya maandamano na kuanza kupambana na waandamanaji wanaoipinga serikali.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Josephat Charo