1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Syria na masharti ya kushiriki mazungumzo ya amani

27 Januari 2016

Mjumbe wa upinzani nchini Syria amemtaka mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wa Syria, Staffan de Mistura afafanue kama mazungumzo ya amani ya Syria yaliyopangwa kufanyika siku ya Ijumaa yatafanikiwa.

https://p.dw.com/p/1Hkmu
Picha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Riad Naasan Agha amesema kuna tatizo ambalo wangependa lipatiwe ufumbuzi na kwamba De Mistura aelezee hasa malengo muhimu ya mazungumzo ya amani ya Syria na kueleza kama mazungumzo hayo yatakuwa na lengo la kuuondoa utawala uliopo au ni kwa lengo tu la kufanyika mazungumzo.

Akizungumza katika mahojiano aliyofanyiwa kwenye kituo cha televisheni cha Al Jazeera, Agha ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya mazungumzo inayoyawakilisha makundi kadhaa yenye silaha iliyoundwa mjini Riyadh, Saudi Arabia, amesema wana nia na amani na wanaamini katika kupatikana suluhisho la kisiasa na wanataka majibu kuhusu suala hilo.

Hayo yanajiri wakati ambapo kundi kubwa la upinzani katika vita vya Syria likisema litahudhuria tu mazungumzo ya amani ya Geneva iwapo vizingiti vitaondolewa kwenye miji iliyozingirwa, hali inayozusha wasiwasi wa uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo hayo.

Katika barua yake iliyomuandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, kundi hilo linaloungwa mkono na Saudi Arabia limerejea wito wake wa kutaka kusitishwa kwa mashambulizi kwenye maeneo ya raia. Barua hiyo ilitumwa jana baada ya mkutano wa kamati kuu ya mazungumzo, ambapo ulijadili kuhusu mwaliko wa kushiriki katika mazungumzo hayo ya Geneva, uliotolewa na De Mistura.

Upinzani waweka masharti zaidi

Barua hiyo pia inataka kuachiwa huru kwa wafungwa, hasa wanawake na watoto. Hatua hizo zimetajwa kwenye azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi uliopita hivyo kuidhinisha mchakato wa amani ya Syria.

Kundi hilo limesema ili mazungumzo hayo yaweze kufanikiwa, baraza hilo linapaswa kufanya kila liwezekanalo kuondoa vizingiti vilivyowekwa vinavyopingana na utekelezaji wa azimio la 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ban Ki-moon
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema ni Wasyria pekee ndio wamealikwa katika mazungumzo ya amani mjini Geneva, taarifa inayokinzana na kuleta utata kuhusu hatua ya Uturuki kusema kwamba itajumuishwa katika mazungumzo hayo.

Hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, alisema kuwa nchi yake itasusia mazungumzo hayo kama kundi la Wakurdi wa Syria, ambalo Uturuki inaamini lina maungamano na wanamgambo wanaopigana ndani ya Uturuki, watakuwa miongoni mwa wajumbe katika meza ya mazungumzo.

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov na mwenzake wa Ufaransa, Laurent Fabius leo wanajadiliana kuhusu maandalizi ya mkutano wa amani ya Syria uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa, huku baadhi ya wajumbe wakiwa wameshawasili mjini Geneva tayari kwa mazungumzo hayo.

Mazungumzo hayo yana lengo la kuanzisha mchakato wa amani kwa ajili ya kumaliza mzozo ulioanza mwaka 2011, wakati wa mapigano ya kumpinga Rais Bashar al-Assad, lakini yakageuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RETRE,APE,AFPE
Mhariri:Josephat Charo