1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upigaji kura wafanyika Baraza Kuu la UN

28 Juni 2016

Nchi tatu kutoka barani ulaya na mbili kutoka katika mataifa ya bara la Asia zinapambana kuwania viti ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika uchaguzi unaofanyika mjini New York nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/1JEoV
Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika moja ya vikao.
Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika moja ya vikao.Picha: Getty Images/AFP/K. Betancur

Wanachama wa Baraza Kuuu la Umoja wa Mataifa watapiga kura kuchagua nchi zitakazojaza nafasi tano zisizo za kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ingawa nafasi mbili miongoni mwa nafasi hizo tayari zimekwishafanyiwa uamuzi. Ethiopia na Bolivia zinashiriki uchaguzi huo bila kupingwa baada ya kuteuliwa na kanda zao kuwania nafasi hiyo lakini bado ziatapaswa kupata theluthi mbili ya kura ndani ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linaloundwa na nchi wanachama 193.

Human Rights Watch yataka rekodi ya haki za binadamu izingatiwe

Mataifa ya Italia , Uholanzi na Swideni yote kwa pamoja yanawania nafasi mbili wakati ambapo nchi za Kazakhstan na Thailand zinawania kiti ambacho kimetengwa kwa ajili ya bara la Asia.

Mtendaji Mkuu wa Human Rights Watch nchini Marekani, Keneth Roth.
Mtendaji Mkuu wa Human Rights Watch nchini Marekani, Keneth Roth.Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Katika kuelekea upigaji kura huo , Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa mwito kwa mataifa wananchama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuzingatia rekodi ya haki za binadamu kwa mataifa ya Kazakhstan na Thailand.

Utawala wa kijeshi wa Thailand ambao uliingia madarakani mnamo mwaka 2014, umepiga marufuku shughuli za kisiasa pamoja na kuweka sheria kali zinazokandamiza uhuru wa kutoa maoni.

"Thailand inaahidi kuongoza harakati za kulinda haki za binadamu kimataifa kama mwanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakati ikishiriki kuvunja haki hizo ndani ya taifa lake " amesema Philippe Bolopion ambaye ni naibu mkurugenzi wa idara ya ushauri ya shirika la Human Rights Watch.

Wakati Kazakhstan ikiwania kupata kiti katika Baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa uliokuwa muungano wa kisovieti mnamo mwaka 1991 imekuwa ikikosolewa kwa kuwabana waandishi wa habari pamoja na kudhibiti shughuli za kisiasa.

"Majadiliano yamekuwa yakiendelea katika Umoja wa Mataifa mjini New York katika mazingira ambayo yasingeweza kukubaliwa nchini Kazakhstan kwenyewe " anasema Bolopion.

Kwa upande wake Italia inawania kupata nafasi katika baraza hilo ikijinasibu kuwa iko katika njia panda ya nchi zinazozungukwa na bahari ya Mediteranea na pia ikijivunia uzoefu wake katika kushughulikia mgogoro wa wakimbizi.

"Nadhani tuko katika nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yanayohusiana na amani na usalama " alisikika balozi wa Italia kwenye Umoja wa Mataifa Sebastiano Cardi.

Italia yajivunia rekodi yake ya kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi

Italia pia inaonekana kupewa nafasi katika juhudi za kuiondoa Libya kutoka katika machafuko yanayoikabili.

Baadhi ya wakimbizi wakiwasili kuingia nchini Italia.
Baadhi ya wakimbizi wakiwasili kuingia nchini Italia.Picha: Reuters/Marina Militare

Uholanzi ambayo ni makao makuu ya mahakama ya uhalifu ya Umoja wa Mataifa na mahakama nyingine za kidunia imekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha kuwa haki inapatikana kimataifa mnamo wakati Swiden ikijivunia rekodi yake ya utoaji misaada duniani.

"Italia na Uholanzi ziko katika nafasi nzuri ya kupata viti katika baraza hilo usalama" anasema David Malone ambaye ni mwakilishi wa wanafunzi .

Nchi tano zitakazochaguliwa kuingia katika Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa zitaanza rasimi majukumu yake ndani ya umoja huo January 1, mwakani zikiungana na nchi nyingine tano wananchama wa kudumu wa Umoja huo ambazo ni Uingereza , Ufaransa, China , Urusi na Marekani.

Kama chombo kikuu chenye nguvu katika Umoja wa Mataifa , Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina mamlaka ya kuweka vikwazo, kuidhinisha mikataba ya amani pamoja na kuruhusu matumizi ya nguvu kijeshi.

Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga