1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upepo wa mabadiliko wavuma Arabuni

4 Februari 2011

Huku maandamano ya kuupinga utawala wa Misri yakiendelea, kile kinachoonekana kama upepo wa maguezi uliloanzia na mapinduzi yaliyomng'oa Zein El-Abidine Ben Ali wa Tunisia, kimeanza kusambaa nchi nyengine za Kiarabu.

https://p.dw.com/p/10AtP
Maandamano nchini Tunisia
Maandamano nchini TunisiaPicha: picture alliance/dpa

Maandamano Jordan

Hivi leo kundi la waandamanaji 1,000 lilikusanyika nje ya ofisi za Waziri Mkuu mpya wa Jordan, Maaruf Bakhit, wakiitikia wito wa tawi la kijeshi la Chama cha Ikhwanul Muslimin, Udugu wa Kiislamu, liitwalo IAF.

Waandamanaji walipiga kelele ya kudaia uhuru na mageuzi zaidi na kupinga sheria za kikandamizaji.

"Tunataka serikali kwa ajili ya masikini. Tunataka sheria za uchaguzi zinazowaridhisha wazee na vijana." Walisema.

Baadaye walielekea kwenye ubalozi wa Misri uliopo karibu na eneo hilo, wakiwa na mabango yanayosomeka: "Tunawapa heshima kubwa na kuwaunga mkono ndugu zetu wa Misri."

Maandamano Misri
Maandamano MisriPicha: AP

Kiongozi wa Ikhwanul-Muslimin, Hammam Said, ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa, wanaandamana kwa ajili ya kuunga mkono ushujaa wa Wamisri katika mapambano yao ya kumuondosha dikteta, akikusudia Rais Hosni Mubarak.

Bakhit aliteuliwa Jumanne iliyopita na Mfalme Abdullah wa Pili, ambaye alimtaka mara moja kushughulikia madai yote ya waandamanaji, ambao walishakuwa mitaani kwa karibuni wiki nzima, kabla haya ya Wamisri.

Hata hivyo, IAF hawakukubaliana na uteuzi wa Bakhit, wakimuona si mwanamageuzi halisi.

Maandamano Syria

Maandamano Misri
Maandamano MisriPicha: AP

Nako mjini Damascus nchini Syria, maandamano yalitarajiwa baada ya sala ya Ijumaa, leo hii, ingawa hadi sasa hakujakuwa na taarifa za kufanikiwa au kutofanikiwa kwake.

Mashahidi waliokuwapo nje ya jengo la Bunge, ambapo maandamano hayo yalikuwa yafanyike, wanasema kwamba mpaka mchana, watu pekee walionekana hapo ni askari kanzu, wakiwa katika makundi madogo madogo.

Maandamano Algeria

Kwengineko, nchini Algeria, wapinzani wamesema wataendelea na maandamano yao ya wiki ijayo, kama yalivyopangwa, licha ya Rais Abdelaziz Bouteflika, kuwawahi kwa kutangaza mabadiliko makubwa ya kisera katika utawala wake.

Kiongozi wa Muungano wa Wafanyakazi wa Sekta ya Umma, Rashid Malawi, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba, licha ya Bouteflika kuondoa sheria ya hali ya hatari iliyowekwa kwa miaka 19 sasa, bado wataendelea na maandamano yao kama kawaida.

Msimamo huu umethibitishwa pia na kiongozi wa chama cha upinzani cha kiliberali, RCD, Mouhsine Belabas.

"Tutaandamana kwa sababu Bouteflika hajakubaliana na madai yetu ya kuondoa hali ya hatari bila ya masharti." Amesema Belabas.

Utawala wa Rais Bouteflika umeweka sharti la maandamano yote kufanyika nje ya mji mkuu wa Algeria, Algiers.

Algeria, kama zilivyo Tunisia na Misri, ina idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na ajira, huku kiwango cha umasikini kikipanda, na serikali ikiendelea kutawala kwa mkono wa chuma.

Vuguvugu la vijana wa Kitunisia lililoanza mwezi Disemba mwaka jana, lilifanikiwa kumng'oa Rais Zein El-Abidine Ben Ali katikati ya mwezi uliopita, huku Rais Hosni Mubarak wa Misri akijikuta kwenye seng'enge ya waandamanaji kwa karibuni wiki mbili sasa.

Hata hivyo, maandamano ya Waalgeria ya tarehe 22 mwezi uliopita, yalishindwa kukusanya watu wengi, na matokeo yake ikawa ni rahisi kwa polisi kuyakandamiza, huku yakiwaacha watu kadhaa wamejeruhiwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters/DPA
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi