1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNITED NATIONS:Myanmar yashtumiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

12 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7GY

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa kauli inayoshtumu hatua ya serikali ya Myanmar ya kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wakidai demokrasia vilevile kutoa wito wa kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa.Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Ghana katika Umoja wa Mataifa Leslie Christian anayeongoza wa baraza hilo.Baraza hilo lililo na nchi 15 wanachama linatoa taarifa yake ya kwanza tangu maandamano hayo kuanza mwezi jana.Sir JOHN SAWERS ni Balozi wa Uingereza katika Umoja wa mataifa

''Ni ujumbe wa nguvu na ulio wazi kabisa kwa serikali ya Myanmar….kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Matifa lina mtizamo wa pamoja na linapinga namna serikali ya Myanmar inaendesha sera zake.Ni dhahiri kabisa kuwa serikali ya Myanmar sharti ichukue hatua mwafaka ili kuanzisha maridhiano ya kitaifa.''

Shirika la Kutetea haki za binadamu Amnesty International linapokea vizuri kauli hiyo ila kuongeza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lingechukua msimamo mkali zaidi dhidi ya serikali ya Myanmar.Shirika hilo aidha linasisitizia Baraza hilo wito wake wa kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya silaha.Marekani kwa upande wake inatoa wito kwa uongozi wa kijeshi wa Myanmar kuwaachia wafungwa wa kisiasa aidha kushiriki katika majadiliano na vyama vya upinzani kama linavyodai Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa.

Takriban watu 13 waliuawa na wengine 2100 kukamatwa na kuzuiliwa wakati uongozi wa kijeshi wa Myanmar ulipovamia maelfu ya waandamanaji wanaodai demokrasia.Maandamano hayo yaliongozwa na watawa wa Kibudha tangu mwezi jana na mwanzoni mwa mwezi huu.