1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za watoto ziingizwe kwenye sheria Ujerumani

Lilian Mtono
20 Septemba 2017

Makundi ya utetezi nchini Ujerumani yanaitaka serikali ijayo kuhakikisha inaingiza haki za watoto na vijana katika katiba. Yanasema kushindwa kuwalinda kizazi kichanga kunaweza kusababisha matatizo makubwa huko mbeleni.

https://p.dw.com/p/2kOb4
Berlin - junge Paare - Eltern - Kinder
Picha: Getty Images/S. Gallup

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Watoto (UNICEF) lilitumia siku ya watoto Jumatano hii (20.09.2017) kuushinikiza muungano wa serikali ijayo kuhakikisha inaingiza haki za watoto katika sheria za msingi za nchi ama "Grundgesetz." 

"Mabunge, utawala ama mahakama zinatakiwa kutambua maamuzi yao yanaweza kumaanisha nini kwa raia wadogo", amesema mwenyekiti wa UNICEF nchini Ujerumani, Jürgen Heraeus, alipozungumza na gazeti la Passauer Neun

Ujerumani inapiga kura ya wabunge Septemba 24, huku chama kinachoongozwa na Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union (CDU) kikitarajiwa kupata ushindi mkubwa dhidi ya chama pinzani cha Social Democrats (SPD).

Heraeus ameonya kwamba pamoja na vyama vingi kuelezea nia ya kuwalinda watoto wakati wa kampeni, lakini bado havipo wazi kama watayatekeleza hayo. "Baada ya uchaguzi, maslahi ya watoto hayapewi tena kipaumbele, na huwekwa nafasi za chini" alisema.

Waziri anayeshughulikia masuala ya familia wa Ujerumani Katarina Barley kutoka chama cha SPD pia ametoa mwito wa kuingizwa kwa haki za watoto katika sheria ya msingi, akisema kwamba "maslahi na haki za watoto bado havijapewa nafasi ya kutosha kila sehemu nchini Ujerumani."

Wapinzani kuhusu mabadiliko hayo wanadai kwamba watu wote, ikiwa ni pamoja na watoto wanaguswa na sheria hiyo ya msingi na haihitaji kutaja mtu mmoja mmoja.

Griechenland Europa Migration
UNICEF imesema kiwango cha umasikini kwa watoto kimeongezeka kutokana na watoto wengi wa wakimbizi kuingia UjerumaniPicha: Getty Images/AFP/A. Messinis

Kiwango cha umaskini wa watoto chaongezeka

Kulingana na mwenyekiti huyo wa UNICEF nchini Ujerumani, umasikini wa watoto nchini humo unaongezeka, hasa baada ya kuwasili kwa takriban watoto 300,000 wa wakimbizi, ambao familia zao zimefanikiwa kuanza kujitegemea tena baada ya kipindi kirefu. Ni wazi kwamba wazazi wengi wanaolea watoto peke yao hutegemea msaada mdogo wanaoupata katika kipindi kirefu.

Aliliangazia hilo katika baadhi ya miji, ambayo ni pamoja na Berlin, ama eneo la viwanda lililopo Magharibi mwa Ujerumani na Ruhr ambako hadi asilimia 35 ya watoto wanaishi kwenye nyumba zinazotegemea kipato kitokanacho na mafao ya kutokuwa na ajira.

"Watoto hawa wanahitaji kupewa nafasi sawa na kusaidiwa wajisikie kwamba wanahitajika." alisema.

Alisisitiza kwamba ilikuwa ni muhimu kwa wenyeji na serikali ya shirikisho kufanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha kwamba kunakuwepo na elimu bora kuanzia shule ya chekechea hadi sekondari nchini kote.

Mwito wa UNICEF wa kutambuliwa kwa haki za watoto uliongezewa kasi na makundi ya misaada ya German Child Protection na wakfu wa watoto, German Children's Fund, ambayo wiki hii yaliwasilisha mpango wenye mambo matano katika kukabiliana na umasikini wa watoto. 

CDU Parteitag in Essen
Kumeibuka hoja ya umri wa kupiga kura kushuka kutoka 18 hadi 16Picha: Getty Images/S. Gallup

Kupanua wigo wa haki ya kupiga kura?

Kuelekea kwenye uchaguzi unaofanyika jumapili hii (24.09.2017), kumekuwepo pia na miito kutoka kwa kundi la vijana nchini Ujerumani kupewa nafasi zaidi ya kuzungumza kwenye siasa.

Mgombea wa Ukansela kupitia SPD, Martin Schulz yeye pia ameshauri kupunguzwa kwa umri wa kuruhusiwa kupiga kura kutoka miaka 18 ya sasa hadi 16 kwenye chaguzi za shirikisho.

Wakati mpango huo ambao unaungwa mkono na chama cha Kijani na Chama cha mrengo wa kushoto, haujapata uungwaji mkono mkubwa katika CDU. Peter Altmaier, mkuu wa utumishi katika makazi ya kansela, mnamo siku ya jumatatu aliliambia gazeti la Spiegel kwamba anaiona hoja hiyo ya kupiga kura kuanzia miaka 16 kuwa ni nzuri.

Wajerumani wengi wanasherehekea siku ya watoto duniani ama Weltkindertag Septemba 20, ingawa siku ya kimataifa ya watoto inayotambulika na Umoja wa Mataifa ni Novemba 20. Baadhi ya maeneo nchini Ujerumani ya Mashariki yaliyokuwa yakimiliwa na wajamaa, bado yanaadhimisha siku ya nyakati za Soviet iliyotengwa kwa ajili ya vijana, Juni 1.

Mwandishi: Lilian Mtono/DW English Page

Mhariri: Mohammed Khelef