1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

U.N yakosoa makapuni ya ulinzi ya sekta binafsi

Tuma Provian Dandi29 Novemba 2007

Raia wengi katika nchi zinazokabiriwa na mizozo ya kisiasa na vita wamekuwa wakipoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa, yote hayo yakisababishwa na askari kutoka sekta binafsi za ulinzi.

https://p.dw.com/p/CUia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: AP

Umoja wa Mataifa umesema haufurahishwi na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari hasa wale wa mashirika ya kibinafsi, wanaolinda usalama katika nchi zenye mizozo ya kivita kutokana na kutumia nguvu kubwa kuliko kawaida dhidi ya raia.

Vitendo vinavyopingwa na Umoja wa Mataifa ni mauaji ya raia, ubakaji, ujambazi, ubaguzi pamoja na kutotenda haki miongoni mwa wananchi wanaokuwa katika mazingira ya vita.

Kwa Mujibu wa Umoja wa Mataifa, vitendo vichafu vinavyofanywa na askari kutoka sekta binafsi vimetanda katika nchi za Iraq na Afghanistan, ambako vita imekuwa ikitatiza haki za binadamu kwa kipindi kirefu.

Ripoti mpya iliyotolewa na Umoja huo imeeleza kwamba katika kipindi cha miaka kumi iliyopita mashirika mengi ya ulinzi yameibuka katika nchi mbalimbali, lakini askari wake hawafanyi kile wanachopaswa kufanya kwa maslahi ya raia walio katika matatizo ya mapigano na mashambulizi.

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni umebaini kwamba mashirika mengi ya ulinzi katika nchi za Afghanistan na Iraq, yanafanya kazi zake baada ya kukodiwa na serikali ya Marekani kupitia Wizara ya Ulinzi. Si Iraq na Afghanistan pekee ambako majeshi ya kibinafsi yanatikana, bali pia katika nchi zinazoendelea kumekuwa na utitiri wa makampuni ya ulinzi, ambayo licha ya kupata pesa nyingi, lakini msaada wake umekuwa mdogo kwa maslahi ya wananchi.

Nchini Iraq askari wa mashirika binafsi wanawajibika zaidi kwa wakuu wao wanaowapatia maelekezo, ambako takwimu zinaonesha kwamba wanausalama elfu 25 kutoka makampuni binafsi wameajiriwa kwa shughuli za kusimamia usalama wa raia.

Kwa mujibu wa mtaalamu mmoja wa uchumi nchi Uingereza, masharika ya ulinzi ya kibinafsi yanaingiza hadi dola bilioni 100 kila mwaka kutokana na shughuli zake.

Katika ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa hivi karibuni, maofisa waliiomba Marekani kuliangilia tatizo hili kwa undani kwa vile wakati mwingine askari wa sekta isiyo rasmi hawana mafunzo ya kutosha kulinda raia hasa nchini Iraq.

Ripoti hiyo inazidi kufafanua kwamba Marekani inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba mateso na uonevu mwingine unaofanywa na askari wa kukodi vinakomeshwa kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni Shirika la upelelezi la Marekani FBI lilitoa ripoti nyingine inayoonesha kwamba watu 14 kati ya 17 waliouawa mwezi wa septemba mwaka huu nchini Iraq, vifo vyao vilitokana na askari wa kukodi kutoka makampuni ya binafsi.

Na hivi sasa uchunguzi mwingine unafanyika juu ya kampuni ya ya ulinzi ya Marekani inayoitwa Blackwater, iliyopewa zabuni ya kulinda maafisa wa Kimarekani wanaofanya kazi nchini Iraq.

Umoja wa mataifa unasisitiza makampuni yote yanayoanzisha vikosi vya ulinzi visivyo vya kiserikali, yanapaswa kutoa elimu ya Haki za Binadamu na kuwajibika ikiwa lolote baya litatokea kwa raia watakaokuwa chini ya ulinzi wa askari binafsi.

Uamzi huo utasaidia kulinda maisha ya raia katika maeneo yenye vurugu za kivita na mapigano.