1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watu 400,000 wanakabiliwa na njaa Tigray

3 Julai 2021

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 400,000 katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula.

https://p.dw.com/p/3vymX
Äthiopien Tigray-Krise | Soldaten TPLF
Mitaa ya jimbo la Tigray, EthiopiaPicha: Ben Curtis/AP/picture alliance

 Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa huo amearifu hayo na kutoa mwito wa msaada wa dharura kuwasaidia mamilioni ya watu wa jimbo hilo linaloandamwa na mzozo kwa zaidi ya miezi nane.

Mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na wapiganaji tiifu kwa chama kinachotawala jimbo la Tigray cha TPLF yalizuka tena mwezi uliopita pale waasi waliapoanzisha mashambulizi makali yaliyoshuhudia wakiukamata mji mkuu, Mekele.

Mapema wiki hii vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia viliharibu madaraja mawili yaliyokuwa njia kuu ya kupeleka msaada wa kiutu unaohitajika kwenye jimbo la Tigray.

Hatua hiyo ilizusha lawama kwamba serikali mjini Addis Abbaba inalenga kutatiza kabisa shughuli za kupeleka msaada wa kiutu kwenye jimbo hilo.

Baraza la Usalama laarifiwa hali mbaya ya Tigray

Siku ya Ijumaa ilishuhudia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likifanya kikao cha kwanza cha wazi kuhusu mzozo wa Tigraya ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwatumbukiza mamia kwa maelfu wengine kwenye baa la njaa.

Äthiopien | Zerstörte Brücke am Tekeze Fluss in Tigray Region
Kuharibiwa kwa daraja la mto Tekeze kumetatiza usambazaji wa msaada wa kiutu TigrayPicha: Roger Sandberg/AP/picture alliance

Ramesh Rajasingham kaimu mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa alikiambia kikao hicho kwamba hali "imezidi kuwa mbaya” tangu kurejea tena kwa makabiliano baina ya pande hasimu wiki za karibuni.

"Zaidi ya watu 400,000 wanakadiriwa kuwa wamo kwenye kundi la wanaoukumbwa na baa la njaa na wengine milioni 1.8 wanakaribia kukubwa na ukosefu wa chakula” amesema afisa huyo.

Rajasingham ameongeza kuwa mashirika mengine yanakadiria kuwa idadi ni kubwa kuliko inayotajwa na kwamba zaidi ya watoto 33,000 wana utapiamlo mkali.

Mwanadiplomasia huyo alitoa mwito akisema „Maisha ya wengi ya watu hawa (wa Tigray) wanategemea uwezo wetu wa kuwafikia na chakula, dawa, virutubisho na msaada mwingine wa kiutu” akisisitiza kwamba msaada huo unahitajika sasa na siyo wiki inayokuja.

Serikali yakanusha kutumia njaa kama silaha

Äthiopien | Jubel beim Einmarsch der TDF in Mekelle
Wapiganaji wa kundi la TPLFPicha: DW

Serikali ya Ethiopia imekanusha madai kwamba inahujumu msaada wa kiutu kwenye jimbo la Tigray.

"Madai kwamba tunapanga kuwabana pumzi watu wa Tigray kwa kuwanyima kupata msaada wa kiutu na kutumia njaa kama silaha ya vita ni uzushi usio na kifani” amesema naibu waziri mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen alipozungumza na wanadiplomasia mjini Addis Ababa.

Kiongozi huyo amesema maafisa wa serikali wanatumia kila njia iliyopo kuwaepusha rais wa Tigray na madhila yanayowakumba.

Chanzo: AFPE