1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mzingiro unaoendelea Syria ni uhalifu wa kivita

Caro Robi
20 Machi 2018

Mkuu wa tume ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al Hussein amesema operesheni ya kijeshi inayoendelea Syria ya kuuzingira mji wa Ghouta Mashariki kwa miaka mitano ni uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/2uc3Y
Syrien Ost-Ghouta
Picha: Reuters/B. Khabieh

Al Hussein ambaye alizuiwa na Urusi kuhutubia kikao rasmi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, aliwasilisha hotuba nzito kuishutumu Syria na washirika wake kwa uhalifu wa kivita na mbinu nyingine zinazokiuka sheria kuhusu vita kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Zeid Ra'ad al Hussein hususan amemshutumu Rais Bashar al Assad wa Syria kwa kuwashambulia watu wake akisema kwa kuwatesa na kuwaua kiholela raia wake, Assad amepoteza mamlaka yake kama kiongozi. Mzozo huo wa Syria mwezi huu umeingia mwaka wake wa nane.

Zeid amkosoa vikali Assad

Nchi nane wanachama wa Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema ni muhimu Umoja huo ufuatilie mara moja hatua madhubuti kuhakikisha azimio la kusitisha mapigano Syria linatekelezwa iwapo nchi kama Urusi na mshirika wake Syria hayatekelezi makubaliano hayo.

Schweiz UN-Menschenrechtsrat in Genf - UN-Hochkommissar Said Raad al-Hussein
Mkuu wa Tume ya kutetea haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al HusseinPicha: Getty Images/AFP/J.-G. Python

Barua iliyotumwa kwa wanachama wote 15 hapo jana imeelezea kutiwa wasiwasi kwa nchi hiyo kutokana na kushindwa kutekelezwa kwa azimio lililopitishwa na Baraza hilo la Usalama mnamo tarehe 24 Februari, la kutaka kusitishwa mapigano katika eneo la Ghouta Mashariki na kote nchini Syria ili misaada ya kiutu iweze kufikishwa na wagonjwa walio katika hali mahututi waweze kuondolewa katika maeneo ya mapambano.

Barua hiyo ilitiwa saini na Ufaransa, Kuwait, Poland, Sweden, Uingereza, Marekani na Uholanzi. Hata hivyo wizara ya ulinzi ya ulinzi ya Urusi leo imetoa taarifa kuwa idadi jumla ya raia walioondolewa Ghouta Mashariki na kupelekwa maeneo salama tangu kuanza operesheni ya kiutu imeongezeka hadi watu 79,702 wengi wao wakiwa watoto.

Zeid amesisitiza kuwa wale wanaoendeleza maovu Syria sharti wachukuliwe hatua za kisheria na hili ni jambo Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama halipaswi kulipigia karata kama linatarajia kuonekana kuwa asasi zilizo halali na zenye mamlaka. Amelihimiza Baraza la Usalama kuiwasilisha Syria katika Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC.

AfD yadai Syria ni salama

Hayo yanakuja huku wanasiasa wa chama chenye siasa kali za mrengo wa kulia cha Ujerumani Alternative für Deutschland AFD walioizuru Syria mapema mwezi huu wakidai Syria inaweza kuorodheshwa nchi salama ambapo Wasyria wanaoomba hifadhi Ujerumani, wanaweza kurejeshwa nchini mwao.

Deutschland Pressekonferenz der Syrien-Reisegruppe der AfD in Berlin
Wabunge wa Chama cha Ujerumani cha AfdPicha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Kundi la wanasiasa saba wa AfD walifanya ziara isiyo rasmi Syria kutathmini hali halisi ya kiusalama kwa matumaini kuwa wataimarisha juhudi za chama chao za kuwarejesha nusu milioni ya wakimbizi wa Syria wanaoishi Ujerumani. Ziara hiyo ililaaniwa vikali na serikali ya Ujerumani na vyama vingine vya kisiasa.

Wakiongozwa na mbunge Christian Blex, wanasiasa hao wa AfD hapo jana katika mkutano na wanahabari wamesisitiza kuwa licha ya kuwa kuna maeneo ambayo bado yanakumbwa na vita, lakini kuna mengine ambayo ni salama kabisa Syria na kutaka wakimbizi wa Syria wanaoishi Ujerumani kurejeshwa kwao.

 

Mwandishi: Caro Robi/ap/dpa/Dw English

Mhariri:Josephat Charo