1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kufunga vituo Kaskazini-Mashariki DRC

Iddi Ssessanga
21 Desemba 2017

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC - MONUSCO umentagaza azma ya kufunga kambi zake za kijeshi kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, huku DRC na Uganda zikikubaliana kulikabili kundi la ADF kwa pamoja.

https://p.dw.com/p/2pl9B
DR Kongo Blauhelm-Soldaten
Picha: DW/F. Quenum

Eneo la Bogoro ndiko yalikofanyika mauaji makubwa mwaka 2003, na kusababisha vifo vya wanakijiji karibu 200 na kusababisha kufunguliwa mashitaka ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu yaliopelekea kiongozi wa wanamgambo Germain Katanga kuhukumiwa kifungo cha miaka 12 gerezani.

"Tumelaazimika kupunguza pakubwa bajeti yetu wakati kazi tunayotarajiwa kufanya ni kubwa. Ndiyo sababu tumeona bora tupunguze idadi ya kambi bila kupunguza uwezo wa operesheni," alisema Julius Fondong, msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, maarufu MONUSCO.

Wengi wa wakaazi wa Bogoro wamepinga waziwazi hatua ya kufunga kambi hiyo kutokana na kuendelea kwa wasiwasi kuhusu usalama. Baadhi wamefikiria hata kuondoka kijijini hapo na kuwafuata walinda amani. "Wanajeshi wetu watawekwa kwenye kambi tatu za operesheni: Komanda, Aveba na Bunia," alisema Fondong.

Semuliki, Nord-Kivu, DR Kongo: Der Untergeneralsekretär der Vereinten Nationen für Friedenssicherungseinsätze, Jean-Pierre Lacroix, besuchte heute den Stützpunkt Semuliki
Naibu Katibu Mkuu wa UN anaehusika na ulinzi wa amani Jean-Pierre Lacroix alipotembea kambi ya UN ilioshambuliwa Desemba 7, ambapo wanajeshi 14 waliuawa.Picha: Monusco/A.Khan

Uamuzi huo unafuatia kufungwa kwa vituo kadhaa vingine vya Umoja wa Mataifa nchini DRC. Mwezi Julai, Umoja wa Mataifa ulitangaza kufungwa kwa vituo vitano katika mkoa jirani wa Kivu Kaskazini licha ya kuwepo kwa makundi kadhaa ya wanamgambo.

Tangazo hilo limekuja mnamo wakati Umoja wa Mataifa umekumbwa na shambulio baya zaidi katika kipindi cha karibu robo karne. Desemba 7, wanajeshi 14 wa kulinda amani walikuwa na wengine 53 walijeruhiwa katika shambulio la kuvizia lililofanywa na wapiganaji, ambao zana zao zilihusisha magruneti yanayorushwa kwa roketi.

Umoja wa Mataifa unao wanajeshi karibu 19,000 pamoja na polisi na waangalizi nchini DRC, huu ukiwa ndiyo ujumbe wake mkubwa na ghali zaidi ukiwa na bajeti ya zaidi ya dola bilioni moja.

Operesheni ya pamoja dhidi ya waasi wa ADF

DRC na Uganda zinapanga operesheni ya pamoja dhidi ya kundi la waasi wa Uganda wa Allied Democratic Forces - ADF, ambao wamelaumiwa kwa shambulio la Desemba 7, ambamo pia wanajeshi watano wa DRC waliuawa.

"Makamanda wa ADF ni raia wa Uganda. Kutakuwepo na mfumo ili kuwezesha majeshi ya nchi mbili kushirikishana katika taarifa za kijasusi na kuendesha operesheni za pamoja," alisema Jenerali Marcel Mbangu Mashita, Kamanda wa ngazi ya juu wa DRC katika eneo la Mashariki.

Kongo - Operation gegen die ugandischen Rebellen der ADF-Nalu
Waajeshi wa DRC wanaoshiriki operesheni za kupambana na waasi wa kundi la ADF-NALUPicha: Reuters/Kenny Katombe

Wawakilishi wa majashi ya mataifa hayo walikutana katika mji wa mpakani wa Kasindi wiki iliopita. Chini ya mpango huo, wanajeshi wa Uganda hawatavuka kuingia DRC lakini watajikita kwenye eneo la mpakani.

"(Jeshi la Uganda) linaimarisha usalama kwenye mpaka wa pamoja na Congo ili kuzuwia jaribio lolote la ADF kuvuka na kufanya mashambulizi dhidi ya shabaha za masalahi kwao nchini Uganda," alisema msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Richard Karemire.

MONUSCO imeahidi kuwasaka waliohusika na shambulio la Desemba 7. Lakini haikushiriki katika mazungumzo ya mataifa mawili kati y amaafisa wa Uganda na DRC.

Makundi hasimu wa wanamgambo yanadhibiti sehemu za mashariki mwa DRC, muda mrefu tangu kumalizika kwa vita vya mwaka 1998-2003, ambamo mamilioni ya watu walifariki, hususani kutokana na njaa na magonjwa.

DRC na Uganda zilikuwa mahasimu katika mgogoro huo, na katika miaka iliyofutia, uhusiano kati ya mataifa hayo umekuwa mgumu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.

Mhariri: Saumu Yusuf