1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umri wa kustaafu ni mdogo!Israel acheni ujenzi

22 Julai 2009

Wahariri wa Magazeti ya hapa Ujerumani hii leo wamejikita zaidi katika mada ya umri mwafaka wa kustaafu na changamoto zake, ziara ya Joe Biden makamu wa rais wa Marekani huko Ulaya ya Mashariki pamoja na suala la Israel

https://p.dw.com/p/Iv8K
Makazi ya Har Homur -Jerusalem MasharikiPicha: picture-alliance/ dpa


Tuanze basi na mada zinazohusiana na hapa Ujerumani. Gazeti la Schwäbische linaanza kwa kuelezea suala la malipo ya uzeeni na kustaafu na linasema kampeni za uchaguzi zimeweka bayana ukweli uliopo na hali halisi ya suala hilo ambayo haivutii. Mijadala inayoendelea kuhusu wakati na umri mwafaka wa kustaafu imebadili mtazamo wake katika miaka ya sasa. Hata hivyo ipo siku ambayo wanasiasa watalazimika kukabiliana na hali halisi. Kwa sasa umri wa kustaafu ni miaka 67. Hilo linadhaniwa kuwa ni mapema sana. Tatizo lililopo ni kwamba mabadiliko ya kima cha uzazi yamesababisha changamoto nyingi katika suala hilo. Kwa kifupi idadi ya watoto wanaozaliwa ni ndogo sana ikilinganishwa na ile ya wazee waliopo. Tatizo hilo sharti lijadiliwe, linamaliza gazeti la Schwäbische.


Gazeti la Der Neue Tag linawatolea wito wanasiasa kulijadili suala hilo kwa kina.Gazeti hilo linasisitiza kuwa tofauti ya umri iliyopo kati ya vijana na wazee ni tatizo na hali ambayo imekuwako kwa muda mrefu. Jamii sharti iwe jasiri ndipo iweze kukabiliana na tatizo hili. Wanasiasa tayari wameshauriwa kukubaliana na hali halisi badala ya kulitweza linamaliza.


Gazeti la Nürnberger Zeitung kwa upande wake linawakosoa wanasiasa kwa kutolipa uzito suala hili. Badala yake wanalikwepa.Likitolea mfano gazeti hilo linaeleza kuwa hakuna mtu yoyote aliye na umri wa miaka 69 anayeweza kujibandika mfuko wa simiti kama anavyosisitiza mkurugenzi wa kampuni ya IG-BAU Klaus Wiesehügel. Yeye ana mtazamo tofauti kuhusiana na suala hilo.Klaus Wiesehügel anapendekeza kuwa na mfumo unaozingatia aina ya kazi afanyayo mtu badala ya kuwa na umri maalum wa kustaafu bila kujali hilo.Gazeti hilo linafafanua kuwa idadi ya watu wanaofanya kazi ngumu za mikono imepungua kwa kiasi kikubwa na wengi wanapendelea zaidi kupata ajira katika sekta za huduma na mawasiliano. Kulingana na Gazeti la Nürnberger kuna haja ya kuwa na mfumo unaoweza kunyumbuka kulingana na mahitaji ya jamii. Linamalizia kwa suali: Jee kuna umuhimu wa kuubadili mfumo huo kwa kuzingatia umri na sekta ya ajira?


Tukibadili mada gazeti la Volkstimme la Magdeburg linaangazia ziara ya makamu wa rais wa Marekani Joe Biden katika eneo la Ulaya Mashariki.Picha maridhawa za Joe Biden zimetanda kote nchini Ukraine pindi alipowasili na kuendelea na ziara yake.Kiongozi huyo anakabiliwa na kibarua kigumu zaidi ya kile cha Rais Obama ambacho ni kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya mashariki.Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden analazimika kusawazisha mambo katika nyanja za kidiplomasia katika mataifa ya Georgia na Ukraine na wakati huohuo Marekani ikiwa muangalifu kwasababu ya mchango wa Urusi kwasababu ya suala la NATO. Georgia na Ukraine zimepania kujiunga na jumuiya hiyo ya kujihami ila Urusi kwa upande wake inapinga vikali hatua hiyo ambayo tayari imeighadhabisha. Hatua ya kuipanua jumuiya ya kujihami ya NATO imezua mitazamo tofauti kati ya wanachama na hata kama Joe Biden anaunga mkono hatua hiyo hilo huenda lisitimie linamaliza gazeti la Volkstimme.


Tukiingia kwenye eneo la Mashariki ya Kati Gazeti la Dresdner Neueste Nachrichten linasema ni nadra sana kwa Marekani kuishinikiza Israel pamoja na wandani wake. Hata Ujerumani iliyo na nafasi muhimu maalum kihistoria imejisogeza mbali na Israel katika suala zima la kujenga makazi kwenye eneo la Jerusalem Mashariki.Mataifa hayo mawili yanafahamu bila wasiwasi wowote kuwa kamwe hayatovumilia mvutano wowote kati yao na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Kiongozi huyo alipuuzilia mbali juhudi za kusaka amani ya eneo la mashariki ya kati baada ya kuidhinisha ujenzi wa makazi ya kifahari katika eneo la Jerusalem mashariki. Gazeti hilo linamaliza kwa kusema kuwa kwa sababu ya hilo Rais Obama hana budi kuthibitisha kuwa ni mpatanishi anayezingatia ukweli na haki katika mchakato mzima wa kutafuta amani kati ya Israel na Palestina ambao uko hatarini.


Mwandishi: Thelma Mwadzaya /DPA

Mhariri: Josephat Charo