1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waishinikiza Israel,kuondoa vikwazo Gaza

19 Julai 2010

Wataka ukanda huo utumike kuinua wakaazi wa Gaza kiuchumi

https://p.dw.com/p/OOni
Mkuu wa masuala ya nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton(Katikati), akitembelea kiwanda cha kutengeneza saruji cha mashariki ya Jabaliya,katika ukanda wa Gaza,jana Jumapili. Umoja huo umeitaka Israel kuondoa vizuizi ili kuwanufaisha kiuchumi wakaazi wa Gaza.Picha: AP

Umoja wa Ulaya umezidi kuendeleza shinikizo zaidi kwa Israel,kwa kuitaka kuondoa vizuizi vyake katika ukanda wa Gaza,na kuruhusu usafirishwaji wa bidhaa katika eneo hilo,ili kuinua uchumi wa wakaazi wa ukanda huo.

Mkuu wa masuala ya nchi za nje wa umoja wa ulaya,Catherine Ashton ametoa kauli hiyo,ikiwa ni mara ya pili kwa umoja huo,kuendelea kuibana Israel,na kutaka eneo hilo,kuendelea kuwa njia muhimu ya kuinua mapato kwa wakaazi wa eneo hilo.

Ashton ametoa kauli hiyo mara baada ya kukutana na Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel,Avigdor Lieberman na kueleza kuwa sera mpya za Israel katika ukanda huo ni hatua nzuri,lakini amesisitiza kuwepo kwa umuhimu mkubwa wa kuondolewa vikwazo zaidi, ili kuruhusu shughuli mbalimbali za kiuchumi,ambazo zitawanufaisha zaidi wakaazi wa eneo hilo.

Ashton amesisitiza kwamba atarejea tena katika ukanda huo katika kipindi cha miezi michache ijayo,kwa nia ya kuzidisha kasi ya kuondolewa vizuizi zaidi katika ukanda huo.

Israel mwezi uliopita,iliregeza masharti ya vizuizi ilivyoweka miaka minne iliyopita,kwa kuruhusu bidhaa za matumizi ya nyumbani kuvuka mpaka huo,lakini imeshikilia msimamo wake wa kukataa bidhaa zinazohusiana na ujenzi,kwa kueleza kuwa zinaweza kutumiwa katika kutengenezea silaha na wapalestina,huku ulinzi na ukaguzi katika mpaka huo ukiwa ni wa hali ya juu.

Ashton,anakuwa afisa wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka Umoja wa ulaya,kuzuru Gaza,tangu kuanza kuondolewa vizuizi katika ukanda huo,ambapo anatarajiwa kukamilisha ziara yake ya siku tatu leo,baada ya kukutana na Rais Mahmoud Abbas wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina.

Ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya,unaunga mkono mtazamo wa Marekani wa kuwa na nchi mbili huru,Israel na Palestina ambapo ameeleza kuwa umoja huo unaangalia njia zitakazowezesha kufikiwa hilo,ili kuwasaidia wapalestina kudhibiti mipaka yao na Israel,na kuwepo kwa hali ya usalama zaidi katika eneo hilo.

Katika ziara yake,Ashton leo ametembelea mahema ya familia za wanajeshi wanaoshikiliwa huko Gaza,na kutoa mwito kwa Chama cha Hamas,kumuachia huru mwanajeshi wa kiisraeli Gilad Shalit , ambaye amekuwa akishikiliwa kwa zaidi ya miaka minne.

Katika kuutanzua mgogoro wa kihistoria baina ya Israel na Palestina,Bibi Ashton ameutaka uongozi wa Palestina,kuingia katika mazungumzo ya ana kwa ana na Israel,huku akionyesha kutofurahishwa kwake na mkakati wa Israel wa kuendeleza makaazi katika eneo la Jerusalem ya mashariki.

Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas kwa upande wake,akizungumza katika mahojiano na gazeti la Jordan mwishoni mwa wiki,ameeleza kuwa yupo tayari kwa majadiliano mapya na Israel,lakini akiweka sharti la kuwepo kwa majeshi ya kimataifa,katika kulinda amani mipakani,katika eneo la wapalestina.

Kutokana na kauli hiyo, Bibi Ashton ameeleza wazi kuwa huu ni wakati muafaka wa kuanza upya kwa mazungumzo zaidi ya upatanishi mwezi Agosti mwaka huu,kabla ya kukutana na Waziri mkuu wa Israel,Benjamin Netanyahu.

Israel mwezi uliopita,iliregeza masharti ya vizuizi katika ukanda huo,unaodhibitiwa na chama cha Hamas,kufuatia mbinyo mkali kutoka jumuiya ya kimataifa kufuatia wanajeshi wa Israel kuuvamia msafara wa wanaharakati waliokuwa katika meli ya misaada kwa ajili ya wakaazi wa Gaza,mwezi Mei,na kusababisha vifo vya raia 9 wa kituruki kuuawa, mmoja akiwa pia raia wa Marekani.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ DPA

Mhariri; Josephat Charo