1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la wakimbizi kuzuiwa

16 Oktoba 2015

Umoja wa Ulaya na Uturuki zimekubaliana kushirikiana katika kuushughulikia mgogoro wa wakimbizi. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya alifahamaisha hayo baada ya mkutano uliofanyika mjini Brussels

https://p.dw.com/p/1GpBc
Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Ulaya na Uturuki zimekubaliana juu hatua ya kuwazuia wakimbizi kuingia katika nchi za Umoja huo.

Kulingana na mapatano yaliyofikiwa, Uturuki imekubali kuwakabili watu wanaowasafirisha wakimbizi kwa njia za kihalifu na pia imekubali kuwaweka nchini mwake wakimbizi zaidi, kati ya mamilioni wanaowasili nchini humo kutoka Syria.

Makubaliano hayo yalifikiwa kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Brussels hadi leo alfajiri .

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker ameeleza kwamba
taarifa ilipatikana mapema leo juu ya kufikiwa makubaliano baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki. Ameeleza kwamba mpango wa pamoja uliokubaliwa unalenga shabaha mbili.Kwanza kuhakikisha kwamba wakimbizi walioko nchini Uturuki wanabakia katika nchi hiyo "

Bwana Juncker amesema lengo la pili la mpango wa pamoja baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ni kuwazuia wakimbizi na wahamiaji kuingia Ulaya kwa kupitia Uturuki.

Uturuki kupewa fedha zaidi

Kulingana na mpango huo wa pamoja viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubali kuipa Uturuki fedha , kiasi cha Euro Bilioni 3 ili iweze kuwahudumia wakimbizi walioko katika nchi hiyo kutoka Syria na pia wamekubali kuuharakisha mchakato wa kulegeza masharti ya kupata vibali kwa wananchi wa Uturuki wanaotaka kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema makubaliano yaliyofikiwa na Uturuki ni hatua muhimu lakini amesema makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk akisalimiana na Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk akisalimiana na Rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: Reuters/F. Lenoir

Amesema maamuzi muhimu yaliyopitishwa yatasaidia katika juhudi za kuidhibiti mipaka ya Umoja wa Ulaya. Bwana Tusk ameunga mkono makubaliano juu ya mpango wa pamoja baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki wenye lengo la kuishughulikia mizizi ya tatizo la ukimbizi.

Uturuki ndicho kituo muhimu cha kwanza kilichotumiwa na wakimbizi 600,000 walioingia barani Ulaya mnamo mwaka huu.Wengi wao wametumia njia za mkato ambazo ni za hatari.

Mkimbizi apigwa risasi na kufa

Hata hivyo mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ulifanyika katika mukhtadha wa kifo cha mkimbizi mmoja kutoka Afghanistan aliepigwa risasi na walinzi wa mpakani wa Bulgaria, wakati akijaribu kuingia Ulaya kutokea Uturuki.Bulgaria imeweka polisi na wanajeshi 2000 kwenye mpaka wake na Uturuki.

Kwa mujibu wa taarifa mtu huyo alipigwa risasi wakati kundi kubwa la wakimbizi lilipokuwa linajaribu kuvuka mpaka. Mtu mwengine pia alijeruhiwa kwa kupigwa risasi. Waziri wa mambo ndani wa Bulgaria amesema wakimbizi 50 kutoka Afghanistan walisimamishwa na walinzi wa mpakani walipokuwa wanajaribu kuvuka mpaka.

Watu 3000 wameshakufa mnamo mwaka huu tangu mgogoro wa wakimbizi uanze.Wengi wamekufa maji wakati wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania ili kuingia Ulaya.

Mkataba baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ulifikiwa baada ya wajumbe wa Halmashauri ya Umoja huo kufanya ziara nchini Uturuki katika jitihada za mwisho za kuishawishi serikali ya nchi hiyo kutia saini makubaliano.

Mwandishi:Mtulla Abdu/afp, dpa

Mhariri: Gakuba Daniel