1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuizingatia ripoti ya jopo la Umoja wa Mataifa

Josephat Charo2 Februari 2007

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na maswala ya mabadiliko ya hali ya hewa, Stavros Dimas, amesema umoja huo unatakiwa kuzingatia ripoti kuhusu ongezeko la joto duniani iliyotolewa leo mjini Paris, Ufaransa na kuunda sera za kukabiliana na tatizo hilo. Wakati huo huo, wanaharakati wa mazingira wamezihimiza nchi zilizoendelea kiviwanda, hususan Marekani, zipunguze viwango vya gesi inayotoka viwandani.

https://p.dw.com/p/CHKo
Kiongozi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhifadhi mazingira, UNEP, Achim Sreiner
Kiongozi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhifadhi mazingira, UNEP, Achim SreinerPicha: AP

Onyo kali lililotolewa na wanasayansi wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa linatakiwa kuzingatiwa kwa makini kama mwito wa kutafuta njia za kukabiliana na tatizo hilo. Kiongozi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhifadhi mazingira, Achim Steiner, ameyasema hayo kufuatia ripoti ya kurasa 21 iliyotolewa leo mjini Paris Ufaransa na jopo la Umoja wa Mataifa la kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

´Ni kauli ya ushahidi mbalimbali uliowasilishwa kwa ulimwengu kuhusu vipi mabadiliko ya matumizi ya nishati inayotokana na takataka na ardhi, yanavyoiathiri mifumo katika sayari yetu.´

Achim Steiner amesema ni muhimu kuitathmini ripoti hiyo kama itazingatiwa zaidi kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yamesababishwa na binadamu, ikiwa sayansi inatosha na ulimwengu utafanya nini kukabiliana na tatizo hilo. Aidha Steiner amesema huu si wakati watu kukaa na kusema hatuwezi kufanya lolote. Yeyote atakayekataa kuchukua hatua wakati huu kufuatia ripoti iliyotolea leo siku za usoni ataingia katika vitabu vya historia kama mtu asiyejali, ameongeza kusema Achim Steiner.

´Kama wewe ni mtoto wa kiafrika uliyezaliwa mwaka huu wa 2007, hakuna tu uwezekano unapofikia umri wa miaka 50 ukakabiliwa na magonjwa mapya, bali unaweza kulazimika kuyahama makazi unayoishi kwa sababu tathmini inaonyesha Afrika huenda ina asilimia 30 ya miundombinu yake katika mwambao wa pwani itakayoathiriwa kufikia mwisho wa karne hii na ongezeko la kiwango cha maji baharini.´

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na maswala ya mazingira, Stavros Dimas, akijibu matamshi ya Steiner amesema Umoja wa Ulaya unajitahidi kufikia lengo la kiwango cha nyuzi mbili za joto, lakini hata hivyo utazingatia ripoti ya jopo la IPCC. Aidha Dimas amesema Umoja wa Ulaya utazingatia matokeo ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa na kuunda sera zake kama itakavyostahili. Amesema ipo haja ya kuyachunguza mapendekezo ya wanasayansi.

Umoja wa Ulaya unatizamwa kama kiongozi katika vita dhidi ya ongezeko la joto la dunaini. Umeanzisha mfumo wa biashara ya gesi ambapo kampuni hununua na kuuza haki ya kutoa gesi ya carbon dioxide kulingana na viwango vilivyowekwa na serikali za mataifa wanachama. Dimas amesisitiza lengo la kufikia nyuzi mbili linaungwa mkono na mataifa yote ya Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, amesema Ujerumani itayahimiza mataifa wanawachama wa Umoja wa Ulaya yakubali kupunguza gesi ya carbaon dioxide kwa kiwango kikubwa katika mkutano wa kilele wa umoja huo utakaofanyika mapema mwezi ujao. Wakati haya yakiarifiwa, waziri wa mazingira wa Italia, Alfonso Pecoraro Scanio, ametaka kufanyike kikao cha dharura cha bunge kuzipiga jeki sera za mazingira. Wanaharakati wa mazingira wameonya kwamba Italia inavuta mkia katika kuyalinda mazingira.

Ripoti nyengine itakayotolewa na jopo la Umoja wa Mataifa la kupambana na ongezeko la joto duniani, IPCC baadaye mwaka huu, itahusu njia muafaka za kupunguza ongezeko la joto duniani.