1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamewasili Dhaka, Bangladesh

30 Aprili 2018

Kikundi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kinachochunguza janga la Myanmar kuhusu Warohingya kimewasili katika mji mkuu wa Bangladesh.

https://p.dw.com/p/2ww2n
Myanmar Mitglieder UN-Sicherheitsrat zu Besuch
Picha: Reuters/M. Nichols

Dhaka ni mji mkuu wa Bangladesh, ambako walikimbilia kiasi ya Warohingya 700,000 kujinusuru na ukandamizaji na mauaji ya  wanajeshi wa Myanmar.

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa utakutana na kiongozi mkuu wa Myanmar, Kansela Aung San Suu Kyi, (AUNG SAN SU CHII) na kamanda Mkuu wa jeshi Jenerali Aung Hlaing wakati wa ziara ya siku mbili kabla ya kuzuru jimbo la kaskazini la Rakhine, eneo ambalo Warohingya walitoroka.

Wanatarajiwa kutathmini athari za uvamizi wa jeshi pamoja na maandalizi ya serikali ya kuwarejesha wakimbizi kutoka Bangladesh.

Katibu mkuu wa masuala ya mambo ya nje wa Mynamar, Myint Thu ameliambia shirika la habari la Associated Press, "Mawaziri watajadili kwa kina mpango wa kuwarejesha wakimbizi kama ilivyokubaliwa na mataifa husika na baadaye kuwapa makazi."

Mipango ya kuwarejesha Warohingya nyumbani

Ameongeza kusema, "ujumbe wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne utapelekwa kwenye vituo vya wakimbizi na pia katika vijiji vilivyoko kaskazini mwaka Rakhine."

Wakimbizi Warohingya wanangángánia chakula wakitoroka vita Myanmar
Wakimbizi Warohingya wanangángánia chakula wakitoroka vita MyanmarPicha: Getty Images/AFP/M. Uz Zaman

Jeshi lilifanya mashambulio katika  jimbo la Rakhine baada ya maafisa wa ulinzi kushambuliwa mwezi Agosti mwaka uliopita. Jeshi limelaumiwa kwa kukiuka haki za binadamu, ikiwemo kunajisi, mauaji, kutesa na hata kuteketeza nyumba za Warohingya, hali ambayo Marekani na Umoja wa Mataifa zimeitaja kuwa safisha safisha ya kikabila.

Serikali ya Myanmar iliruhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuzuru jimbo hilo, ombi ambalo awali lilikataliwa kwa kamati huru ya kufanya uchunguzi. Mwezi Machi mwaka uliopita, kamati hiyo ilisema kuwa ilipata ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya makabila madogo ya Kachin,Shan na Warohingya "katika kile ambacho huenda kikazingatiwa kama ni uhalifu, katika sheria za kimataifa."

Warohingya wataka mazingira salama

Wakachin na Washan ni makabila mengine madogo ambayo yanataka uhuru na yanajihusisha na  vita vya ukombozi dhidi ya serikali.

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Karen Pierce -mmoja wa wajumbe wanaozuru Mynamar, baada ya mkutano alisema, "Baraza la Usalama litaendelea kufanikisha mpango wa kuwarejesha wakimbizi, lakini Warohingya wanastahili kurejea kwenye mazingira salama."

Maelfu ya wakimbizi walikusanyika kwenye makambi yao huku kukiwa na joto kuukaribisha ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa, waliyabeba mabango, mengine yaliyokuwa yameandika "Tunataka haki."

Mnamo mwezi Desemba Bangladesh na Myanmar zilikubaliana kuanza mpango wa kuwarejesha wakimbizi mwezi Januari, lakini kulikuwa na wasiwasi miongoni mwa wafanyikazi wa kutoa misaada na Warohingya wenyewe  kuwa wangelezamishwa kurejea Mynmar katika mazingira yasiyo salama.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman