1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 30,000 wameathirika na mzozo wa Ukraine

29 Aprili 2016

Zaidi ya watu 10,000 wameuawa na wengine 20,000 wamejeruhiwa, tangu kuanza mgogoro wa Ukraine Aprili mwaka 2014. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti, iliyowasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/1If6D
New York UN Sicherheitsrat Sitzung MH17
Picha: picture-alliance/dpa/J. Szenes

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa Taye-Brook Zerihoun, ameliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa kwamba idadi sahihi ya walioathirika nchini Ukraine ni watu 30,729 ikiwamo 9,333 waliouawa na 21,396 waliojeruhiwa.

Ameongeza kwamba tukio la juzi Aprili 27, la mashambulizi ya mabomu limepelekea raia wanne kuuawa pamoja na wengine wanane kujeruhiwa katika enel la Olenivka karibu na mji wa Donetsk.

"Mapigano yamezuka tena katika wiki za hivi karibuni katika kiwango kilichoonekana mara ya mwisho Agosti mwaka 2014. Wakati mapigano yalipokuwa yamepamba moto zaidi," amesema Zerihoun katika mkutano huwo.

Halikadhalika amezilaumu pande zote mbili kwa kuzuwia ujumbe wa usimamizi wa kimataifa kufanya kazi yake, uliotumwa baada ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya mjini Minsk Febuari 2015 kati ya Ukraine, Urusi, Ufaransa, na Ujerumani.

Zerihoun aliongeza, kwa mujibu wa takwimu za kundi hilo la usimamizi, maeneo yanayodhibitiwa na uasi ndio yenye vizuwizi zaidi. Aidha Zerihoun amezitolea wito pande zinazozozana kusitisha mapigano hayo.

Mazungumzo ya mwanzo tokea Disemba

Ukraine Donezk ukrainische Soldaten
Picha: picture-alliance/dpa/S. Vaganov

Kikao hicho cha jana cha Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa kilikuwa cha kwanza kuzungumzia mgogoro wa Ukraine tangu Disemba mwaka jana. Katika kikao hicho Zerihoun amesema mzozo huo haujasahaulika.

"Wakati vita vya Mashariki ya Ukraine vikiwa vinatimiza mwaka wake wa tatu, Baraza la Usalama linakutana leo likifahamu umuhimu wa mgogoro huu na pia likiwa na matumaini. Kushindwa kutekelezwa kikamilifu makubalianoa ya mkataba wa Minsk, kumedhihirisha haja ya kusonga mbele na jitihada za kutafuta kwa suluhisho la kisiasa la migogoro huu, " amesema Zerihoun.

Katika mkutano huwo pande mbili za Ukraine na Urusi zilitupiana lawana juu ya nani anayehusika na kuanzisha tena mapigano hayo.

Balozi wa Urusi kwa Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin ameueleza mkutano huwo kuwa ni wa mchezo, huku Ukraine ikiwa inadhibiti miji kadhaa katika eneo linalotakiwa lisiwe na mapigano chini ya makubaliano ya mkataba wa Minsk.

Churkin ameongeza kwamba Umoja wa Mataifa umekuwa ukitumiwa kama jukwaa la kufanyia propaganda, katika mgogoro huwo wa Ukraine.

Hat hivyo Marekani Ufaransa pamoja na Uingereza, zimeishutumu Urusi kwa kufanya uchokozi unaochochea mgogoro huwo.

"Kinachoonekana leo ni matokeo ya ukiukaji wa Urusi wa mipaka ya Ukraine.Ulioanza pale ilipoivamia Crimea zaidi ya miaka miwili iliyopita, na kulipanua jeshi lake katika ardhi hiyo, pamoja na kuyapa msaada wa silaha makundi yanayotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine," balozi wa Marekani Samantha Power aliliambia baraza hilo kwamba.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape

Mhariri: Gakuba Daniel