1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi wa Urusi kuhusu Navalny

Saleh Mwanamilongo
8 Septemba 2020

Mkuu wa Tume ya haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa,ameitolea mwito Urusi kuendesha uchunguzi wa kina kuhusu  madai ya kushambuliwa kwa sumu Alexei Navalny.

https://p.dw.com/p/3iAje
Schweiz Genf | UN-Hochkommissarin |  Michelle Bachelet
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Mkuu wa Tume ya haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa,Michelle Bachelet ameitolea mwito Urusi kuendesha uchunguzi wa kina,uliowazi na huru kuhusu  madai ya kushambuliwa kwa sumu  Alexei Navalny,mpinzani mkuu wa rais Putin. Wakati huohuo Urusi inamtaka balozi wa Ujerumani nchini humo kutoa maelezo kuhusu mkasa huo.

Michelle Bachelet alisisitiza kuhusu umuhimu wa kufahamu ukweli kuhusu tukio hilo. Rupert COLVILLE,msemaji wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa amesema kwamba  ni lazima kuweko na uchunguzi ,baada ya wataalamu wa Ujerumani kusema kuna ushahidi tosha kwamba Navalny alipewa sumu ya kiwango cha kivita ya Novichok.

‘'Haitoshi kukanusha kwamba hakupewa sumu na kukataa uchunguzi wa kina,ulio huru na wa wazi katika jaribio hilo la mauwaji. Ni jukumu kwa viongozi wa Urusi kuendesha uchunguzi wa kina kuhusu wahusika wa uhalifu huo. Uhalifu mkubwa sana ulifanyika katika ardhi ya Urusi''

Mwanaharakati huyo wa kupambana na rushwa  mwenye umri wa miaka 44 na mpinzani  mkuu wa rais Vladimir Putin,aliuguwa ghafla wakati alipokuwa ndani ya ndege na kupewa tiba ya awali mwanzo kwenye hospitali mojawapo ya Siberia kabla ya kuletwa mjini Berlin.

Jaribio hilo la mauwaji ni la hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya wakosoaji wa rais Putin.

Shikinizo la kimataifa dhidi ya Urusi

Mkuu wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa,amesema kwamba idadi ya visa vya mashambulizi ya sumu au majaribio ya mauwaji ya kulengwa mnamo miongo miwili dhidi ya raia wa Urusi nje na ndani ya nchi hiyo inatisha.

Alexei Navalny,mpinzani mkuu wa rais wa Urusi Vladimir Putin.
Alexei Navalny,mpinzani mkuu wa rais wa Urusi Vladimir Putin.Picha: Reuters/T. Makeyeva

Wiki iliyopita serikali ya Ujerumani ilisema "habari za kutisha” zilizoonesha "bila shaka yoyote" kuwa tukio la kupewa sumu Alexei Navalny lilikuwa jaribio la mauaji kwa kutumia sumu inayoathiri mishipa ya fahamu ya aina ya Novichok.

Balozi wa Ujerumani mjini Moscow amealikwa na wizara ya mambo ya nje ya Urusi ili kutoa maelezo kuhusu tuhuma za Ujerumani dhidi ya Urusi. Duru zinaelezea kwamba balozi huyo anatakiwa kukutana kesho Jumatano na Sergei Lavrov waziri wa mambo ya nje wa Urusi.

Maria Zakharova msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi amesema kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba Ujerumani haikutoa ushahidi wa kutosha kuhusu madai yake ya kwamba Navalny alipewa sumu ya Novichok.

Taarifa ya hospitali ya Charité, mjini Berlin, anakotibiwa Navalny imesema leo kwamba , hali ya mgonjwa huyo imeimarika kiasi cha kuwaruhusu madaktari kumuondoa katika hali ya nusu kaputi, na kumuondoa hatua kwa hatua katika mashine za kumsaidia kupumua.