1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kusitisha shughuli za kimisaada Gaza

Kalyango Siraj24 Aprili 2008

Israel yailaumu Hamas kwa kusababisha kwa mgogoro wa mafuta Hamas

https://p.dw.com/p/Dnvb
Waziri Mkuu wa serikali ya Hamas katika eneo la Gaza, Ismail Haniyeh, katikati.Isreal inaulaumu uongozi wa Hamas kwa kusababisha mgogoro wa mafuta katika eneo hilo.Jenereta inayotoa umeme inazimika wakati wowote kutokana na kuishiwa mafuta.Picha: AP

Isreal inalilaumu kundi la Hamas kwa kusababisha ilichokiita mgogoro bandia kuhusu uhaba wa mafuta.

Hali hiyo imemlazimisha mkurugenzi wa shirika linalowahudumia wakimbizi wa Palestina kuonya kuwa shirika lake litasimamisha ugawaji wa chakula katika ukanda wa Gaza katika kipindi cha saa 24 endapo hakitapata mafuta zaidi.

Mafuta hayo yanahitajika kwa ajili ya kusambaza chakula kwa wakimbizi laki sita Unusu walioko Gaza.

Eneo la Gaza linakabiliwa na uhaba wa mafuta.Na inasemekana kuwa eneo hilo huenda likakumbwa na giza kutokana na jenereta inayozalisha umeme kukaukiwa na mafuta.

Isitoshe hali hiyo imelazimisha shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia ugawaji misaada kuonya kuwa linakaribia kusimamisha shughuli zake za kuwapa usaidizi wakimbizi wa kipalestina kwani magari yao hutumia mafuta kusafirisha msaada wa chakula.

Hali hiyo inayaweka maisha ya watu laki kadhaa wa Kipalestina katika hali ngumu.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana jana kujadilia mgogoro huo,lakini badala yake wajumbe wa mataifa ya magharibi wakiongozwa na Ufaransa walitoka nje ya mkutano huo baada ya balozi wa Libya kufananisha hali ilivyo kwa sasa katika ukanda wa Gaza kama ile iliokuwa katika kambi za wakati wa enzi za Unazi.

Israel inatoa hoja kuwa uzuiaji wake wa mafuta kwa Gaza ni muhimu ili kuishinikiza serikali ya Gaza inaoongozwa na Hamas kusimamisha uvurumishwaji wa maroketi,wa kila siku, kwa Israel.

Licha ya mkuu wa shirika la kutoa msaada la Umoja wa mataifa,John Ging,kuhakikisha kuwa hali hiyo inasikitisha,Israel kwa upande wake leo imeulaumu utawala wa Hamas katika ukanda wa Gaza kwa kusababisha ,ilichoita,mgogoro bandia,kwa kukataa makusudi kuchukua na kusambaza lita milioni moja za mafuta zilizotolewa kwa ukanda huo.

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Israel,Arye Mekel amesema kuwa lita milioni moja za mafuta,alizosema ni tosha kwa shughuli za kimisaada,ambazo Israel ilizitoa wiki tatu ziliziopita baado hazijachukuliwa kutoka sehemu ya Palestina ya kituo cha mafuta cha Nahal Oz.

Wakazi wa ukanda wa Gaza wanasema kuwa maafisa wa Hamas huchukua mafuta hayo na kujigawia wenyewe kwa wenyewe,maafisa wa serikali pamoja na wanafunzi wao bila kuyasambaza kwa watu wa kawaida.

Kwa mda huohuo rais wa Palestina, Mahmud Abbas, yuko Washington, Marekani, ili kufanya mazungumzo na utawala wa huko kuhusu mazungumzo ya amani na Israel.Ametazamiwa kukutana leo alhamisi na rais George W. Bush kutafuta msukumo wa mazunguzo yaliyokwama miezi mitano tangu yafifuliwe upya.

Na hayo yakiarifiwa kuna taarifa zinazosema kuwa Uturuki imekuwa inaendesha majadiliano ya upatanishi kati ya Israel na Syria tangu Aprili mwaka wa 2007.

Kutokana na juhudi hizo rais wa Syria,Bashar al- Assad amenukuliwa kusema kuwa Uturuki imemwambia kuwa Israel iko radhi kukabidhi tena milima ya Golan kwa minajili ya kupata amani.Milima hiyo ilitekwa na Israel katika vita vya mwaka wa 1967na kuifanya kama sehemu yake mwaka wa 1981.

Na kwa upande mwingine maafisa wa kijasuasi wa Marekani watalielezea baraza la Congress kuhusu ushahidi mpya wanaosema walioupata kuambatanana juhudi za Syria za kujenga vinu vya Nuklia ikisaidiwa na Korea Kaskazini.

Maelezo hayo yatakuwa ya faragha na yanafanyika baada ya shambulio ambalo halikufafanuliwa lililofanywa na Israel ndani ya Syria mwezi wa Septemba mwaka jana.

Syria kwa upande wake inakanusha madia ya kuwa na mpango wowote wa kutengeneza silaha za nuklia.