1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya raia, Sri-Lanka.

Halima Nyanza/AFP/AP11 Mei 2009

Umoja wa Mataifa leo umelaani mauaji ya raia yaliyofanywa nchini Sri lanka mwishoni mwa wiki na kuyaita mauaji ya kiholela, ambapo zaidi ya watoto 100 wameuawa, wakati serikali na waasi wakitupiana lawama.

https://p.dw.com/p/Hnf2
Watoto zaidi ya 100 wameripotiwa kuuawa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini Sri Lanka.Picha: AP

Msemaji wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Sri Lanka, Colombo Gordon Weiss amesema idadi kubwa ya raia wanaouawa wakiwemo watoto zaidi ya 100 kunaonesha ukweli wa kuwepo kwa mauaji hayo ya kiholela kutokana na kusababisha kwake umwagaji damu mkubwa.


Waasi wanasema raia wameuawa wakati jeshi likiendelea na mashambulio yake, lakini hata hivyo Wizara ya Ulinzi imelaumu waasi hao wa Tamil Tigers kwa mashambulio wanayofanya ili ''kutengeneza'' hali mbaya ya kibinadamu na kufanya Jumuia ya Kimataifa kuingilia kati.


Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo imesema waasi hao wamekuwa wakishambulia raia kwa silaha nzito na badala yake kutupia lawama majeshi ya Sri Lanka.


Jumatatu serikali ya nchi hiyo ilisema watu 250 wameuawa ama kujeruhiwa katika shambulio wanalolaumu kufanywa na waasi, huku mtandao unaoripoti habari za waasi ukifahamisha kuwa idadi ya watu hao waliouawa mwishoni mwa wiki imeongezeka na kufikia 3,200.


Nao Maafisa Afya wa serikali kwenye eneo hilo la kaskazini linalokabiliwa na mapigano wamesema mashambulio yaliyofanywa siku mbili katika eneo hilo, Jumamosi na Jumapili yamesababisha vifo vya raia 430 na wengine maelfu wamejeruhiwa.


Wakati huohuo Muungano wa Mashirika ya Haki za Binadamu yamelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumzia vita hivyo.


Aidha Mashirika ya Haki za Binadamu na Makundi ya Kuzuia Mapigano yameitaka Japan, nchi ambayo inaongozwa kwa kuifadhili Sri Lanka misaada kuchukua hatua na kukabiliana na hali mbaya ya kibinadamu iliyoko nchini humo.


Wito huo umetolewa katika barua ya pamoja ya Viongozi wa mashirika ya kiutu, likiwemo Shirika la Haki za Binadamu la Human Right Watch, Amnesty Internation, kwenda kwa Waziri Mkuu wa Japan Taro Aso.


Serikali ya Sri Lanka hivi karibuni imekosoa mataifa ya magharibi kwa kutaka usimamishaji wa mapigano, ambao utamaliza kampeni yake dhidi ya Waasi wa Tamil Tigers kabla ya kufanikisha operesheni hiyo.


Mwezi uliopita Jeshi lilitangaza kusimamisha matumizi ya silaha nzito kwa ajili ya kuwalinda raia.


Madai ya madhara yanayotokea katika uwanja wa vita yamekuwa vigumu kuthibitishwa ukweli wake kutokana na Waandishi wa Habari na Waangalizi wa Kimataifa kutoruhusiwa kufika katika eneo hilo.


Maelfu ya raia wanaaminika kukwama katika eneo hilo lenye mapigano, huku Umoja wa Mataifa uzkisema raia hadi 6500 wanaweza kuwa wameuawa na wengine elfu 14 kuwa wamejeruhiwa katika mapigano hayo tangu mwezi Januari.


Mapigano hayo kati ya Majeshi ya Sri Lanka na Waasi wa Tamil Tigers yamedumu kwa karibu miaka 40.


Mwandishi: Halima Nyanza(AFP/AP)

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman