Umoja wa Mataifa waionya Ethiopia kuhusu kupeleka majeshi Somalia | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.11.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa waionya Ethiopia kuhusu kupeleka majeshi Somalia

Umoja wa mataifa umeonya kuwa kitendo cha Ethiopia kupeleka vikosi vyake nchini Somalia kunaweza kuzorotesha zaidi hali mbaya ya usalama katika eneo hilo.

default

 Ofisi wa umoja huo inayohusika na masuala ya kibinadamu imesema kupanuliwa kwa mgogoro nchini Somalia kutawafanya watu wengi zaidi kuyahama makaazi yao. Wakati huo huo kuna ripoti kuwa gari lililobeba wanajeshi wa Kenya limeripuliwa karibu na mpaka wa Somalia.

Ripoti hiyo ya ofisi ya umoja wa mataifa inayohusika na masuala ya kibinadamu imesema kuwa taarifa za Ethiopia kujiingiza kijeshi nchini Somalia zimepokelewa kwa wasi wasi mkubwa na mashirika ya kibinadamu, kwa sababu kitendo hicho kitawafanya watu wengi nchini humo kuyahama makazi yao, na kuzidisha ugumu wa kufikiwa na misaada.

Ofisi hiyo ilikariri maelezo ya wananchi wa Somalia ambao walisema walishuhudia mlolongo wa malori ya jeshi la Ethiopia ukiingia nchini mwao tarehe 19 mwezi huu wa Novemba. Ethiopia imezikanusha ripoti hizo.

Umoja wa mataifa unasema kuwa licha ya juhudi za jumuiya ya kimataifa kupeleka msaada wake nchi Somalia, bado raia wapatao laki mbili na nusu wa nchi hiyo wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha nja, hasa hasa katika maeneo ya kati na kusini yaliyo chini ya udhibiti wa wanamgambo wa Al Shabab.

Wakati hayo yakijiri, kumetokea mripuko kwenye lori lililowabeba wanajeshi wa Kenya katika eneo la Mandera karibu na mpaka wa Somalia, na ripoti za vyombo vya habari nchini Kenya zinasema wanajeshi 11 walijeruhiwa katika mripuko huo.

Afisa mwenye cheo cha Kanali katika jeshi la Kenya Cyrus Oguna amelithibitishia shirika la habari la Reuters kuwa mripuko huo ulitokea, na kuongeza kuwa walikuwa wakitathmini athari zake. Kamanda wa polisi katika eneo ulikotokea mripuko huo Leo Nyongesa amesema hakuna mwanajeshi yeyote aliyekufa.

Somalia Mogadischu

Wapiganaji wa kundi la Al-Shabab.

Kumektokea miripuko kadhaa nchini Kenya tangu nchi hiyo ilipopeleka vikosi vyake nchini Somalia mwezi uliopita, kupambana na wanamgambo wa Al Shabab. Wakazi wa eneo la Mandera wanasema jeshi limeweka ulinzi mkubwa kuzunguka sehemu ya mripuko.

Kwenye uwanja wa mapambano ndani ya Somalia kumeripotiwa mashambulizi ya ndege kwenye kambi za wanamgambo wa Al Shababu. Mkazi wa mji wa Badade alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema yalitokea mashambulizi matatu kwenye ngome za Al Shababu, ambayo yaliwafanya wakazi wote kuingiwa na woga na kuukimbia mji.

Mashambulio hayo yalithibitishwa na serikali ya Somalia mjini Mogadishu, lakini haikusema kama yalifanywa na jeshi la Kenya. Al Shababu pia walithibitisha kushambuliwa huko, wakisema yalidondoshwa mabomu saba. Wanamgambo hao hata hivyo walisema shambulio hilo halikusababisha hasara yoyote kwa sababu wapiganaji wake walikuwa tayari wametoka kwenye kambi zilizolengwa.

Umoja wa Afrika una kikosi cha kulinda amani nchini Somalia, ambacho jukumu lake kubwa ni kulinda serikali ya mpito mjini Mogadishu isiangushwe na wanamgambo wa Al Shababu. Kikosi hicho kinaundwa na wanajeshi kutoka Uganda na Burundi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 24.11.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13GKt
 • Tarehe 24.11.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13GKt

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com