1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umma bado watanda uwanja wa Tahrir

26 Novemba 2011

Maelfu ya watu wameendelea kukusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo na miji mengine nchini Misri, wakiulaumu utawala wa kijeshi kwa 'kuyaiba' mapinduzi ya umma na kuutaka uachie madaraka haraka.

https://p.dw.com/p/13Haq
Maelfu ya waandamanaji wakisali katika uwanja wa Tahrir.
Maelfu ya waandamanaji wakisali katika uwanja wa Tahrir.Picha: dapd

Maandamano hayo yanaendelea kwa wiki nzima sasa, na ikiwa ni siku mbili tu, kabla ya uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanywa hapo Jumatatu. Waandamanaji pia wanapinga kuteuliwa kwa Kamal al-Ganzouri kuwa waziri mkuu mpya, baada ya kujiuzulu kwa baraza la mawaziri mwanzoni mwa wiki hii. Ganzouri aliyewahi pia kushikilia wadhifa huo huo, wakati wa utawala wa Hosni Mubarak, amesema utawala wa kijeshi umempa nguvu kubwa zaidi kuliko mtangulizi wake.

Maandamano yameendelea kuwa ya amani, huku polisi wakijizuia kutumia nguvu, kama ilivyokuwa hapo mwanzo. Kwa mujibu wa wizara ya afya, hadi kufikia jana, idadi ya watu waliopoteza maisha, kutokana na makabiliano ya polisi na waandamanaji, ilikuwa imefikia 41. Marekani na Umoja wa Ulaya zimeutolea wito utawala wa kijeshi nchini Misri, kurudisha madaraka kwa utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/ZPR

Mhariri: Prema Martin