1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umainifu wa nchi unatiwa mashakani

B.Burkhard / P.Martin13 Novemba 2007

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimekosolewa kuhusu utaratibu unaotumiwa kupata orodha ya ya watu wanaoshukiwa kuhusika na ugaidi.Kwa mujibu wa ripoti iliyotayarishwa na Dick Marty kwa niaba ya Baraza la Ulaya,haki za binadamu zimekiukwa vibaya wakati wa kukusanya habari za washukiwa hao.

https://p.dw.com/p/CH70

Katika ripoti iliyotolewa mjini Paris,mbunge wa Kiswissi Dick Marty amelalamika kuwa watu waliotajwa katika orodha za washukiwa ugaidi,wala hawana haki ya kujitetea.Wengi wao pia hawajui kile wanachotuhumiwa.Inavyoelekea,hata wasio na hatia wamo katika orodha hizo na hakuna utaratibu maalum wa kuwasaidia washukiwa wa aina hiyo kuyaondosha majina yao kutoka orodha hiyo.

Kinachoshangaza ni ile idadi ya nchi zilizokiuka haki za binadamu katika mkumbo wa kupiga vita ugaidi na hali zina serikali zenye misingi ya kisheria.Ukiukaji huo unaanzia mateso,misafara ya siri ya CIA,jela ya Guantanamo Bay ambako hakuna sheria na sasa,kuna utaratibu wa kuweka orodha ya washukiwa ugaidi na kuwanyima watu hao haki ya kujitetea na hivyo ndio kuwatokomeza kiholela.

Vitendo vya aina hiyo,haviwezi kutetewa hata katika vita vya kupambana na ugaidi.Ikiwa leo hii,muuaji wa mara kwa mara ana haki zaidi kuliko mtu aliewekwa kwenye orodha ya washukiwa ugaidi, basi moja ni wazi-yaani nchi iliyo na misingi ya kisheria,ndio ipo njiani kupuuza kile kinachodaiwa kugombewa katika vita vyake dhidi ya ugaidi.

Dick Marty katika ripoti yake ametonesha kidonda.Kwa haki mbunge huyo wa Kiswissi, anabainisha jinsi vita dhidi ya ugaidi vinavyomomonyoa haki za kimsingi.Si hilo tu,kwani tangu muda mrefu,vita hivyo dhidi ya ugaidi vimekuwa kama vita vya siri vya kitamaduni.

Haiwezekani kuwa imesadifika tu,kwamba takriban wote miongoni mwa kama watu 370 walio katika orodha ya washukiwa ugaidi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,ni Waislamu.Je,hatima ya watu hao haina maana hivyo?

Kwa mfano,Youssef Nada mwenye asili ya Kimisri na uraia wa Kitaliana.Yeye amewekwa kwenye orodha ya washukiwa ugaidi na anaendelea kubakia katika orodha hiyo,licha ya kuwa mahakama za nchi ya uraia wake na kule anakoishi,hazikuweza kupata ushahidi wo wote dhidi ya mfanya biashara huyo.Dick Marty hajakosea anaposema leo,ni Youssef Nada,kesho huenda akawa mmoja wetu.

Lakini hata unapokuwepo ushahidi wa kuhusika na harakati za kigaidi,mshukiwa huyo pia,ana haki ya kujitetea na kushtakiwa mahakamani kisheria. Ujumbe wa Dick Marty ni kuwa sheria hizo zinahitaji kuhifadhiwa.Ni dhahiri kuwa nchi inapaswa kujitetea lakini ndio ifuate sheria au sivyo,itapoteza uaminifu wake.