1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umaarufu wa Angela Merkel wapanda.

29 Oktoba 2009

Atajwa kuwa mwanamke mwenye nguvu duniani.

https://p.dw.com/p/KIVu
Kansela Angela Merkel.Picha: AP

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye alichaguliwa rasmi na bunge kwa mhula mpya hapo Jumatano amechukua nafasi ya kwanza katika orodha ya jarida la Forbes kama mwanamke mwenye nguvu kabisa duniani kwa mwaka wa nne mfululizo.

Merkel mwenye umri wa miaka 55 na ambaye kitaaluma ni mwanafisikia, alifuata mbinu za kunusa hali ya mambo na ya kinyonga wakati wa utawala wa kikoministi katika Ujerumani mashariki ya zamani na kugeuka kiongozi wa kwanza mwanamke wa Ujerumani ilioungana na mwanasiasa wa kwanza mwenye umri mdogo kuwa Kansela.

Alimaliza kiu chake cha kutaka kuwa kiongozi wa taifa alipoingia madarakani 2005 na kuiongoza serikali kuu ya muungano kati ya wahafidhina na Social Democrats baada ya uchaguzi ambao haukutoa mshindi wa wazi.

Merkel ambaye anakiri kwamba si msemaji mwenye kipaji kikubwa hadharani, amefanikiwa kuonyesha sifa za kuweza kuliongoza taifa lenye idadi kubwa ya wakaazi katika umoja wa ulaya na nguvu za kiuchumi.

Wakosoaji wake walimlaumu hapa na pale hadi alipotokeza kuonyesha muelekeo wa uongozi wake.

Hatua yake ya tahadhari pia ilizusha shutuma kali, wakati msukosuko wa fedha ulipoyakumba masoko duniani mwaka jana, na viongozi wenzake wakampa Merkel jina la " Bibi asiye na lolote" wakitarajia hatua kubwa ya Ujerumani kuyapiga jeki mabenki.

Hivi sasa serikali yake mpya na waliberali wanaopendelea wafanyabiashara, inakosolewa pia kwa kuandaa mpango wa kiasi ya euro bilioni 24 wa kodi nafuu kwa miaka minne ijayo, licha ya kuongezeka nakisi katika bajeti. Lakini Merkel anasema ukuaji uchumi utairuirejesha hazina ya Ujerumani mahala pake.

Bibi Merkel amejipatia mafanikio kadhaa katika sera ya kigeni nikiwa ni pamoja na maridhiano yaliopatikana katika bajeti ya Ulaya 2005 na makubaliano kuhusu hali ya hewa alipokua mwenyekiti wa kundi la nchi nane zilizoendelea kiviwanda, jambo ambalo lilimpatia taji la utani"Bibi wa Dunia."

Merkel pia akarekebisha kile alichokiona ni kujitenga kwa mtangulizi wake Gerhard Schroeder na vita vya Marekani nchini Irak. Wiki ijayo atakua kiongozi wa kwanza wa Ujerumani tangu 1957 kuyahutubia mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani-Congress.

Aliondoka Hamburg alikozaliwa kwa jina la Angela Kasner wiki chache baada ya kuzaliwa wakati baba yake aliyekua mhubiri wa Kiprotestanti kuamua kufanya kazi katika Ujerumani mashariki ya kikoministi.Merkel alipata shahada ya juu ya udaktari katika fizikia na kujitenga na siasa hadi ulipoanguka ukuta wa Berlin miaka 20 iliopita.

Mwaka 1990 akajiunga na chama cha kihafidhina Christian Democratic Union-CDU na kushinda kiti cha bunge katika Ujerumani mashariki ya zamani na huo ukawa mwanzo wa kupanda kwake hadi kuwa Kansela.

Merkel wiedergewählt Flash-Galerie
Bibi Merkel akipongezwa na wabunge baada ya kuchaguliwa na bunge.Picha: AP

Mumewe Joachim Sauer waliofunga ndoa miaka 11 iliopita ni mkemia na mtu mwenye haya mbele ya hadhara. Alikataa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa mkewe 2005 kuwa Kansela na pia hakuwepo Jumatano ya wiki hii wakati Bibi Angela Merkel alipoapishwa tena baada ya kuchaguliwa na bunge kwa mhula wa pili wa miaka minne mengine kama Kansela wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman /AFP

Mhariri:Othman Miraji