1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wawaonya wapigakura Uingereza

Mohammed Khelef16 Juni 2016

Wiki moja kabla ya kura ya maoni nchini Uingereza, idadi ya wanaotaka kujitoa Umoja wa Ulaya yapanda na khofu miongoni mwa viongozi wa Umoja huo imetanda wakitoa wito wa kuwataka wapigakura wasiiondowe nchi yao.

https://p.dw.com/p/1J8DK
Kampeni ya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Kampeni ya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.Picha: picture-alliance/dpa/A. Rain

Wasiwasi kwamba huenda Waingereza walio wengi watapiga kura ya kuukataa Umoja wa Ulaya unazidi kupanda kote barani humu. Hivi leo (Juni 16), Mkuu wa Kamisheni ya Umoja huo, Jean-Claude Juncker, aliwaambia wajumbe wa kongamano la uchumi mjini Saint Petersburg, Urusi, kwamba hata kama kujitoa kwa Uingereza hakutauwa Umoja wa Ulaya, bado kutaacha athari kubwa.

"Ikiwa Uingereza inaondoka kwenye Umoja wa Ulaya, hiki kitakuwa kipindi cha wazi cha ukosefu mkubwa wa uhakika, ndani ya Uingereza yenyewe na ndani ya Umoja wa Ulaya na zaidi kwenye kiwango cha kilimwengu. Jambo hili linapaswa kuepukwa," alisema Juncker.

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, ambaye yuko ziarani Helsinki, Sweden, amesema litakuwa kosa kubwa endapo kambi inayotaka Uingereza iachane na Umoja wa Ulaya itafanikiwa. Naye pia, alielezea matumaini ya Umoja wa Ulaya kuendelea kuwepo, lakini akisisitiza kuwa gharama yake itakuwa ni kubwa kwa pande zote husika.

Ujerumani yataka Uingereza ibakie

Hapa Ujerumani, Waziri wa Uchumi Sigmar Gabriel, amesema kitendo hicho kitayafanya mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya kuanza kufikiria pia kuhama. Akizungumza kwenye kongamano la kibiashara kati ya Ujerumani na Poland, Gabriel amesema ana matumaini Uingereza itabakia.

"Sote tunajuwa kwamba Ulaya inakabiliana na changamoto ya tarehe 23 Juni. Matokeo yoyote ya kura hiyo - na sisi Wajerumani na nategemea pia watu wa Poland - tunatarajia Uingereza itasalia kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, sio tu kwa sababu za kiuchumi. Sura ya Ulaya itabadilika. Tutaonekana kama bara ambalo haliwezi kutegemewa hasa", alisema Gabriel.

Kampeni ya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Kampeni ya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.Picha: Getty Images/AFP/B. Stansall

Benki Kuu ya England yaonya

Kwenyewe nchini Uingereza, Benki Kuu ya England imeonya kwamba kura hiyo ya maoni ya wiki ijayo ni kitisho kikubwa kwenye soko la dunia. Dondoo za mkutano huo kwa mwezi Juni zinasema kuwa matokeo ya kura ya maoni yanayatisha masoko ya fedha ndani na nje ya Uingereza.

"Endapo Uingereza itapiga kura ya kujitoa Umoja wa Ulaya, thamani ya sarafu ya pound kitachuka zaidi, na pengine kwa haraka zaidi," zinasema dondoo hizo.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kampuni ya Ipsos Mori na kuchapishwa hivi leo unaonesha kuwa asilimia 53 ya wapiga kura wanaunga mkono kile kilichopewa jina la Brexit, yaani kujiondoa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya, huku asilimia 47 ndio wanaotaka kubakia kwenye jumuiya hiyo ya mataifa wanachama 28.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo