1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yahitaji sera mpya kuhusu wakimbizi

20 Aprili 2015

Boti iliyokuwa ikisafirisha wahamiaji 700 imezama mwishoni mwa juma karibu ya pwani ya Libya. Katika maoni ya mwandishi wa DW, Johannes Beck anasema wakati umewadia kwa Ulaya kuwa na sera mpya kuhusu wakimbizi.

https://p.dw.com/p/1FAw4
Wahamiaji hukabiliwa na hatari kubwa katika Bahari ya Mediterania
Wahamiaji hukabiliwa na hatari kubwa katika Bahari ya MediteraniaPicha: Opielok Offshore Carriers/dpa

Ni tukio gani hasa inabidi kwanza litokee, hadi hatimaye Umoja wa Ulaya ubadilishe sera yake kuhusu wakimbizi? Ni watu wangapi wanapaswa kwanza kuzama katika Bahari ya Mediterania ili wanasiasa wa Ulaya washtuke. Ni ibada nyingine ngapi za mazishi inabidi zifanyika hadi pale Umoja wa Ulaya uchukue hatua?

Italia yenye kuzongwa na madeni ilifanya kile kilichozishinda nchi nyingine za Ulaya, baada ya boti kuzama katika kisiwa chake cha Lampedusa mwezi Oktoba mwaka 2013. Meli za kijeshi za Italia zilianza kupiga doria katika njia za baharini kati ya Afrika Kaskazini na Ulaya Kusini, kama sehemu ya operesheni iliyoitwa ''Mare Nostrum''.

Nchi hiyo iliweza kuokoa maisha ya watu waliokuwa wakizama, huku nchi nyingine za Ulaya zikisita kuchangia kwenye bajeti ya Euro milioni 108 kugharimia operesheni hiyo kwa mwaka. Badala yake Ulaya ilikabidhi jukumu la kuokoa maisha ya wakimbizi kwa shirika lake la kukagua mipaka, Frontex.

Mwandishi wa DW, Johannes Beck:
Mwandishi wa DW, Johannes Beck:

Ujumbe wa ''Triton'' ulianza mwezi Novemba mwaka jana, ukichukuliwa kuwa wenye gharama ndogo kuliko Mare Nostrum. Hii ndio sababu ujumbe huo unajikita katika kuokoa maisha ya watu walio karibu na mwambao wa Ulaya, na hausaidii kuepusha maafa kama haya kwenye pwani ya Afrika Kaskazini, hali inayoyaweka hatarini maisha ya maelfu ya watu.

Huu sio muda wa kauli za kuomboleza

Nisingependa kuwasikia tena wanasiasa wa Ulaya wakitamka maneno ya kuombolea baada ya msiba wa hivi karibuni katika Bahari ya Mediterania. Wale ambao hawataki kushiriki katika operesheni kama Mare Nostrum kwa sababu wanadhani ni ghali mno, angalau wawe wakweli na wasema hadharani kwamba maisha ya watu wa Eritrea, Ethiopia au Syria hayana thamani kubwa.

Hebu tazama sera ya kilimo ya Ulaya, na utabaini ubeuzi kuhusu zile kauli juu ya kuigharimia operesheni ya Mare Nostrum. Umoja wa Ulaya huwasaidia wakulima wake kwa Euro bilioni 50 kila mwaka kupitia ruzuku wanazopata. Hii inamaanisha kwamba umoja huo hutumia fedha nyingi kila siku kwa ruzuku ya wakulima wake, kuliko gharama ya operesheni ya Mare Nostrum kwa mwaka mzima.

Matakwa matatu

Wazo la sera mpya kwa wakimbizi limekuwepo kwa miaka mingi. La kwanza, mkakati wa muda mfupi: Operesheni za kutafuta na kuokoa watu wanaokabiliwa na hatari ya kuzama zianze tena katika eneo zima la Bahari ya Mediterania, na bila shaka, ligharimiwe na nchi zote za Umoja wa Ulaya. Italia haiwezi hata kidogo kuachiwa peke yake mzigo wa kuhangaika peke yake kama ilivyotokea kwenye operesheni ya Mare Nostrum.

Meli za doria ya baharini zinaweza kuokoa maisha ya wakimbizi wengi
Meli za doria ya baharini zinaweza kuokoa maisha ya wakimbizi wengiPicha: Reuters/Guardia Costiera

La pili, mkakati wa muda wa kadri: Sera za Umoja wa Ulaya kuhusu uhamiaji hazina budi kufanyiwa mabadiliko. Mbali na kuruhusiwa kwa wakimbizi kuja Ulaya kuepuka unyanyasaji wa kisiasa na vita kama vile vinavyoendelea nchini Syria, wahamiaji wanapaswa pia kuruhusiwa kuingia Ulaya kwa sababu za kiuchumi.

Ukweli usio rasmi ni kwamba tayari Ulaya tayari imekuwa bara la wahamiaji. Nchi nyingi zenye idadi kubwa ya wazee zitaendelea kuwahitaji wahamiaji. Mfumo wa viwango vya wanaohitajika unaweza kuufanya mchakato huo kuwa wenye uwazi na unaoheshimu sheria. Hii inaweza kusitisha safari za wale wanaotafuta kazi ambao wanakimbilia boti ya wasafirishaji haramu wa binadamu kupitia Bahari ya Mediterania.

La tatu, mkakati wa muda mrefu: Umoja wa Ulaya unapaswa kuyamulika matatizo yanayowafanya watu watake kuzihama nchi zao. Wale walioharibu taasisi za utawala nchini Libya kutumia operesheni ya kijeshi, hawawezi kuondoka tu na kuiacha nchi hiyo ikididimia katika ghasia.

Umoja wa Ulaya unapaswa pia kusisitiza kuheshimiwa kwa haki za binadamu, kwa mfano nchini Eritrea ambako wakimbizi wengi wanafanya safari za boti hutoka. Hata Ujerumani imelifumbia macho kwa muda mrefu, na wakati mwingine imeipa serikali ya kiimla ya nchi hiyo msaada wa maendeleo.

Tumekuwa na muda mrefu wa maneno na malalamiko, sasa ni wakati wa vitendo.

Mwandishi: Johannes Beck

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Iddi Ssessanga

http://www.dw.de/opinion-eu-needs-a-new-refugee-policy/a-18392877