1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuiwekea vikwazo zaidi Urusi

Mohammed Khelef8 Septemba 2014

Ukraine na waasi wanalaumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa, huku Umoja wa Ulaya ukikutana kujadili vikwazo vipya dhidi ya Urusi wanayoituhumu kuunga mkono waasi hao.

https://p.dw.com/p/1D8cl
Mpiganaji wa upande wa waasi mjini Donestk,
Mpiganaji wa upande wa waasi mjini Donestk,Picha: Reuters/M.Shemetov

Licha ya kuingia dosari kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwishoni juzi na jana, Shirika la Ushirikiano wa Usalama la Ulaya, (OSCE) lilisema kwa ujumla makubaliano hayo yanaendelea kutekelezwa, japo yako kwenye wakati mgumu.

Balozi Thomas Greminger wa Uswisi, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa shirika hilo, aliuambia mkutano wa dharura wa mataifa 57 wanachama wa OSCE kwamba siku chache zijazo kuanzia sasa zitakuwa muhimu sana.

OSCE imetuma wachunguzi 250 nchini Ukraine, kufuatilia mzozo huu ambao sasa Umoja wa Mataifa unasema umeshapoteza maisha ya watu 2,729. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binaadamu, Ivan Simonovic, aliuambia mkutano huo wa OSCE kwamba ikiwa idadi ya wahanga wa ajali ya ndege ya MH17 ya Malaysia itajumuishwa kwenye orodha hiyo, basi hadi sasa mzozo wa mashariki mwa Ukraine umeshapoteza maisha ya zaidi ya watu 3,000.

Amnesty International yadai Urusi inawasaidia waasi

Hayo yakiendelea, shirika la haki za binaadamu la Amnesty International lilisema lina ushahidi usiopingika kwamba Urusi imekuwa ikiwasaidia wapiganaji wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Kifaru cha Ukraine kwenye eneo la mzozo mashariki mwa nchi hiyo.
Kifaru cha Ukraine kwenye eneo la mzozo mashariki mwa nchi hiyo.Picha: AFP/Getty Images/P. Desmazes

Akizungumza na shirika la habari la Reuters akiwa kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kiev, katibu mkuu wa shirika hilo, Salil Shetty, alisema wamekusanya picha za satalaiti zinazoonesha Urusi ikikusanya silaha zake kwenye eneo hilo.

"Tulichonacho ni picha mpya za satalaiti zinazoonesha ushawishi wa moja kwa moja na Urusi. Urusi haiwezi kukana kuwa sehemu ya mzozo huu tena. Vikosi vyenye kuratibiwa vyema, kimfumo kabisa na silaha viko huko. Hakuna namna yoyote ambapo waasi wangeliweza kujipanga kiasi hicho," alisema.

Serikali ya Urusi inakanusha kutuma wanajeshi ama kuwapa silaha waasi, ingawa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na mashirika mengine yanasema ushahidi wa wazi unaashiria Urusi inafanya hivyo.

Umoja wa Ulaya kuthibitsha vikwazo vipya

Viongozi wa Umoja wa Ulaya walitazamiwa kukutana Jumatatu (8 Septemba) kutangaza vikwazo vyao vipya vya kuiadhibu Urusi baada ya mapigano ya mwishoni mwa wiki kutishia kuyavunja makubaliano ya kusitisha mapigano. Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, alisema wamegundua "Urusi inakubali tu kufanya mazungumzo pale inapokuwa kwenye wakati mgumu."

Mwanajeshi wa Ukraine katika moja ya vituo vya ukaguzi mashariki mwa nchi hiyo.
Mwanajeshi wa Ukraine katika moja ya vituo vya ukaguzi mashariki mwa nchi hiyo.Picha: picture-alliance/dpa/R.Pilipey

Duru hiyo mpya ya vikwazo itaimarisha hatua ambazo tayari zilishachukuliwa dhidi ya Urusi tangu tarehe 1 Julai, zikilenga kuwazuia watu binafsi kusafiri na kuzuia mali zao na pia kubana fursa za masoko kwa kampuni za mafuta na silaha za Urusi.

Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev, ameapa kuchukuwa hatua kali dhidi ya Ulaya kwa kuzizuwia ndege zake kuruka juu ya anga la nchi hiyo kuelekea Asia, lau vikwazo hivyo vipya vitaidhinishwa hivi leo.

Kwenyewe mashariki mwa Ukraine, Jumatatu ilianza kwa wanajeshi wa serikali kuimarisha ngome zao kwenye mji wa Mariupol, baada ya mashambulizi ya Jumamosi (6 Septemba) ya waasi. Mashambulizi hayo yalimuua mwanamke mmoja, akiwa mtu wa kwanza kabisa kufa tangu pande hizo mbili kusaini makubaliano ya kumaliza miezi mitano ya mapigano siku ya Ijumaa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Saumu Yussuf