1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukuaji wa uchumi utapunguka nchi zilizostawi kiuchumi

P.Martin7 Novemba 2008

Kwa mujibu wa IMF- kwa mara ya kwanza tangu Vita Vikuu vya Pili,mwakani katika nchi zilizoendelea kiuchumi,ukuaji katika sekta hiyo utapunguka kwa asilimia 0.3 kwa sababu ya mgogoro wa fedha unaoenea kila pembe ya dunia.

https://p.dw.com/p/FpJ7

Hiyo ni kinyume na ripoti yake ya awali iliyotabiri ukuaji wa asilimia 0.5 katika nchi zinazoendelea na asilimia 3.0 kote ulimwenguni.

Taasisi ya fedha yenye nchi wanachama 185,ikirekebisha ripoti yake ya mwezi Oktoba imesema,matumaini ya kuona ukuaji wa kiuchumi duniani,yamepunguka wakati sekta ya fedha ikiendelea kuwa dhaifu na wazalishaji bidhaa na wanunuzi wakizidi kupungukiwa na imani,hali inayohatarisha nafasi za ajira na faida za makampuni ya biashara.Katika ripoti mpya iliyotolewa siku ya Alkhamisi,IMF inatabiri kuwa katika nchi zinazoendelea,kwa mara ya kwanza tangu Vita Vikuu vya Pili,ukuaji wa kiuchumi utapunguka kwa kipindi kizima cha mwaka 2009.Lakini inatazamiwa kuwa hali hiyo itaanza kubadilika mwishoni mwa 2009. Inakadiriwa kuwa kwa jumla,uchumi wa dunia nzima utastawi kwa asilimia 3.7 kulinganishwa na asilimia 1.4 katika nchi zilizoendelea kiuchumi.Na Marekani uchumi utadorora,ikitabiriwa kuwa ukuaji wa uchumi mkubwa kabisa duniani utapunguka kwa asilimia 0.7.IMF imepaswa kurekebisha ripoti yake,baada ya kudhdihirika zaidi hali ngumu zilizosababishwa na mgogoro wa masoko ya fedha kote duniani.

Uchumi wa Uingereza utaumia zaidi ikitabiriwa kuwa mwakani ukuaji wake utapunguka kwa asilimia 1.3 wakati Marekani kitovu cha mgogoro wa fedha ulioibuka Agosti mwaka 2007,baada ya benki za kutoa mikopo ya nyumba kuingia matatani,itashuhudia ukuaji mdogo wa asilimia 1.4 tu.Na katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro,ukuaji wa uchumi wake unatabiriwa kupunguka kwa asilimia 0.5 katika mwaka 2009.Na katika nchi mbili zenye uchumi mkubwa kabisa katika kanda hiyo,ukuaji wa kiuchumi unatazamiwa kupunguka kwa asilimia 0.8 nchini Ujerumani na asilimia 0.5 huko Ufaransa.

Kwa upande mwingine katika nchi zinazoinukia kiuchumi na zinazoendelea, uchumi wake utaendelea kuimarika na kukua lakini kwa kasi ndogo ya asilimia 6.6 katika mwaka huu 2008 na asilimia 5.1 mwakani.Kwa mujibu wa IMF ukuaji wa uchumi katika nchi za Asia ya Mashariki ikiwemo pia China,umepunguka kwa sehemu ndogo,kulinganishwa na nchi zingine zenye uchumi uliostawi,kwani nchi hizo zimenufaika kutokana na masharti bora ya biashara na nchi hizo pia zimeanza kubadilisha sera zake kwa azma ya kuhimiza biashara ndogo ndogo.