1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yawazuia wanaume wa Urusi kuingia nchini mwake

Bruce Amani
30 Novemba 2018

Maafisa wa Ukraine leo wamewazuia wanaume raia wa Urusi wa umri kati ya  miaka 16 na 60 kuingia nchini humo katika hatua ya karibuni ya kuongezeka kwa mvutano baina ya nchi hizo mbili jirani

https://p.dw.com/p/39Blh
Russland Konflikt Krim Ukraine | Ukrainische Schiffe im Hafen von Kerch
Picha: picture-alliance/dpa/Tass/S. Malgavko

Mgogoro wa muda mrefu ambao uliibuka  tena Jumapili iliyopita wakari walinzi wa mpakani wa Urusi walipozigonga na kuanza kuzifyatulia risasi meli tatu za Ukraine karibu na Rasi ya Crimea, ambayo Urusi iliiinyakua mwaka wa 2014. Meli hizo zilikuwa zikijaribu kupita katika mlango wa Kerch kuelekea katika Bahari ya Azov. Warusi haobaadaye wakazikamata meli hizo pamoja na mabaharia 24. Bunge la Ukraine Jumatatu likaidhinisha muswada wa rais wa kuweka sheria ya kijeshi nchini humo kwa siku 30 kufuatia msuguano huo.

Petro Tsygykal, mkuu wa walinzi wa mpakani nchini Ukraine ametangaza leo kwenye mkutano wa usalama kuwa Warusi wote wa kiume wa kati ya umri wa miaka 16 na 60 watazuiwa kuingia nchini humo wakati sheria ya kijeshi ikiendelea kutekelezwa.

Rais Petro Poroshenko aliumbia mkutano huo kuwa hatua hizo zimechukuliwa ili kuizuia Urusi kuunda vikosi vya kijeshi vya siri kwenye ardhi ya Ukraine.

Uamuzi huo unafuatia tangazo la Alhamisi la Rais wa Marekani Donald Trump la kuufuta mkutano uliosubiriwa kwa hamu na kiongozi wa Urusi Vladmir Putin, Trump alisema sio vyema kwa yeye kukutana na Purin kwa sababu Urusi haijawaachilia huru mabaharia wa Ukraine.

Kiongozi aliyeteuliwa na serikali ya Urusi kuchunguza malalamiko dhidi ya serikali katika jimbo la Crimea ameyaambia mashrika ya habari ya Urusi kwamba mabaharia wote wamehamishwa kutoka kizuizi kimoja cha Crimea. Makamanda watatu wamepelekwa Moscow. Haijafahamika maramoja kama wengine 21 wamehamishwa.

Mahakama ya Crimea mapema wiki hii iliamuru mabaharia hao wa Ukraine wawekwe jela kwa miezi miwili wakisubiri kukamilishwa uchunguzi.

Wakati huo huo, shirika la ujasusi la Ukraine linafanya upekuzi nyumbani kwa Padre mkuu wa nyumba kubwa kabisa ya watawa mjini Kiev ambayo ni sehemu ya Kanisa la Orthodox la Urusi.

Ihor Guskov, mkuu wa shirika la ujasusi la Ukraine – SBU amewaambia wanahabari leo kuwa maafisa wake wanapekua nyumbani kwa Padre Pavlo anayesimamia Monasteri ya Pechersk mjini Kiev.  Amesema mhubiri huyo anashukiwa kwa "kuchochea chuki”.

Kumekuwa na ongezeko la uhasama kati ya Ukraine na Urusi tangu Urusi iliponyakua Rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine mwaka wa 2014. Urusi pia inawaunga mkono wanaharakati wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine kwa kuwapeleka kisiri nchini humo wanajeshi na silaha. Mapigano ya eneo hilo yamewauwa karibu watu 10,000 tangu mwaka wa 2014 lakini yakapungua baada ya makubaliano ya Minsk ya mwaka wa 2015.

Mwandishi: Bruce Amani/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman