1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine na Maonyesho ya Kimataifa ya ITB-Magazetini

6 Machi 2014

Mzozo wa Ukraine,rufaa katika kesi dhidi ya rais wa zamani Christian Wulff,na maonyesho ya kimataifa ya utalii ITB mjini Berlin ni miongoni mwa mada zilizomulikwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1BL4C
Waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk alipokuwa ziarani kwenye makao makuu ya Umoja wa ulaya mjini BrusselsPicha: DW/ B. Riegert

Tunaanzia Ukraine ambako licha ya wanadiplomasia wa madola makuu kuingia mbioni kujaribu kuepusha usizidi makali mzozo baada ya Urusi kutuma wanajeshi katika ghuba ya Crimea,nchi hiyo inajikuta ukingoni mwa kufilisika.Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya jana imeamua kuipatia Ukraine msaada wa Euro bilioni 11 katika kipindi cha miaka miwili inayokuja.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linajiuliza kuhusu undani wa msaada huo na kuandika?"Euro bilioni tatu kutoka bajeti ya Umoja wa Ulaya,na Euro bilioni nane kutoka benki ya uwekezaji ya Ulaya pamoja na benki ya ujenzi mpya na maendeleo zinatolewa kwa lengo la kuisaidia serikali ambayo hadi wakati huu haijafanya mengi kustahiki mkopo.Mbali na kuelemea upande wa magharibi.Lakini madhumuni hasa ya Euro bilioni 11 ni nini?Kuiokoa nchi hiyo isifilisike?Kuwaonyesha wakaazi walio wengi wa mashariki wanaoelemea upande wa Urusi,faida za kuwa mwanachama wa Umoja wa ulaya.Kuivutia Urusi.Kuuonyesha ulimwengu kwamba licha ya mgogoro unaozikaba nchi za kanda ya Euro bado kuna uwezekano wa kuwajibika hata kama mlima wa madeni utaongezeka?Au ndo watu wanataka kuonyesha moyo wa kuleta mageuzi?Yote hayo hayasaidii kitu."

Faida ya Mabilioni ya Euro

GGazeti la "Nordwest" linatathmini hali namna ilivyo mjini Kiev na kujiuliza kama kweli msaada huo wa fedha utasaidia:"Kwa kuahidi msaada wa mabilioni ya Euro Umoja wa ulaya unaendelea kujaribu kuivutia upande wake Ukraine.Nchi hii takriban imefilisika,pesa kutoka Brussels zinaweza pengine kusaidia kuzuwia vurugu kubwa zaidi kutokea katika janga la mgogoro wa kisiasa na kiuchumi.Lakini serikali ya mpito si imara.Na msaada wa fedha kutoka Umoja wa ulaya katika hali kama hii ni sawa na bahati nasibu."

2014 Freispruch für Ex-Bundespräsident Christian Wulff
Rais wa zamani Christian Wulff baada ya kutajwa na mahakama ya mjini Hannover, hana hatia,februari 27 iliyopitaPicha: picture-alliance/dpa

Kesi dhidi ya Rais wa Zamani Haijamalizika

Waliofikiria kuwa kesi dhidi ya rais wa zamani wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Christian Wulff imemalizika,wamekosea.Mwendesha mashtaka mjini Hannover ameamua kukata rufaa.Suala wahariri wanalojiuliza ni jee rufaa hiyo itakubaliwa? Gazeti la "Neue Presse" linaandika:"Yeyote aliyejiuliza wakati wa kesi hiyo kwanini jaji Rosenow amewaita mashahidi wengi kama wale na ambao hawajasaidia kufichua ukweli,hakosi kujipatia jibu:Hakutaka kuuachia upenu upande wa mashtaka wa kukata rufaa.Jaji Rosenow amefanya kazi yake ipasavyo na kwa namna hiyo mtu anaweza kuashiria,miezi michache tu kutoka sasa korti kuu ya Ujerumani itatamka:rufaa imekataliwa.Hapo Wulff atakuwa ameshaifikia shabaha yake.Hakuna njia bora zaidi ya kutakaswa na makosa yote kuliko hiyo.Hata hivyo mwendesha mashtaka hajaondowa uwezekano wa kubadilisha msimamo wake.Na ingekuwa uzuri kwasababu wakati huo,kadhia hiyo ingefikia mwisho wake.

ITB 2014 05.03.2014 Berlin
Maonyesho ya kimataifa ya Utalii ITB mjini BerlinPicha: DW/S. Kinkartz

Maonyeshi ya ITB yavutia

Na hatimaye wahariri hawajayasahau maonyesho makubwa ya kimataifa ya Utalii-ITB, yaliyofunguliwa jana mjini Berlin. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika:Mashirika mengi zaidi kuliko mwaka jana yanawakilishwa ili kuwavutia wananchi wenye kiu cha kupitisha likizo zao nchi za nje katika wakati huu ambao hali ya kiuchumi ni nzuri na riba ni hafiifu.Mashirika ya Ujerumani yameingia mbioni.Si ajabu kwa hivyo kuona hata yale maeneo yanayopendwa na watalii yanapigania wateja.Kwamba zaidi ya thuluthi mbili ya wajerumani wanapenda kupitisha likizo zao nchi za nje,haimaanishi pekee kwamba wanapenda bei za nafuu na kwenda maeneo ya mbali zaidi:Wanavutiwa zaidi na ukarimu na huduma bora wanazopata..

Amina:

Na kwa ripoti hiyo kuhusu maonyesho ya kimataifa ya Utalii mjini Berlin ndio na sisi tunazifunga kurasa za magazeti ya Ujerumani.........................

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo