1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine mbioni kufikia makubaliano na wakopeshaji

7 Aprili 2015

Ugiriki itajitahidi kufikia makubaliano ya awali na taasisi za kimataifa zilizoikopesha nchi hiyo wakati wa mkutano na mawaziri wa nchi zinazotumia sarafu ya euro barani Ulaya uliopangwa kufanyika Aprili 24.

https://p.dw.com/p/1F3Vz
Christine Lagarde (L) shakes hands with Greek Finance Minister Yanis Varoufakis during an extraordinary euro zone finance
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Christine Lagarde (kushoto) akiwa na Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis.Picha: REUTERS/F. Lenoir

Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis ameliambia gazeti litolewalo kila siku nchini Ugiriki la Naftemporiki kwamba makubaliano hayo ya awali na wakopeshaji hao lazima yafikiwe katika mkutano wa mwaziri wa fedha wa nchi za kanda ya sarafu ya euro barani Ulaya.

Serikali ya Ugiriki ilmewasilisha orodha ya mpango wake wa mageuzi kwa taasisi za mikopo za Ulaya unaojumuisha hatua za kupambana na ukwepaji kodi na kuoanisha shughuli za utawala kwa matarajio ya kuweza kupatiwa mkopo uliobakia wa dola bilioni 7.9 kuisaidia nchi hiyo isifilisike .

Wakati kukiwa hakuna dalili ya ufumbuzi kutoka kwa taasisi ya mikopo ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika kufikia makubaliano serikali ya Ugiriki imeonya kwamba hazina ya taifa itaishiwa na fedha mwezi huu na kupelekea kufilisika kwa Ugiriki pamoja na kujitowa katika kanda inayotumia sarafu ya euro Barani Ulaya.

Wasi wasi wa kufilisika kwa Ugiriki

Akiwa mjini Washington Varuofakis alijaribu kuondowa hofu ya uwezekano wa kufilisika kwa nchi hiyo kwa kusema kwamba Ugiriki haitokuwa na tatizo la kulipa deni lake kwa IMF kunakatorajiwa wiki hii.

Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis
Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis VaroufakisPicha: Reuters/E. Vidal

Ugiriki inadaiwa na Shirika hilo la Fedha la Kimataifa euro milioni 450 na kuna wasi wasi kwamba nchi hiyo inaweza kufilisika wakati wa kulipa mkopo huo kunakotarajiwa hapo Alhamisi.Varoufakis amemwambia mkuu wa IMF Christine Lagarde wakati wa mazungumzo ya ana kwa ana mjini Washington kwamba Ugiriki italipa deni hilo kabla muda iliyotakiwa kufanya hivyo kumalizika.

Lagarde amesema hapo jana kwamba kuwepo kwa hali ya mashaka hakuna maslahi na Ugiriki na amekaribisha uthibitisho uliotolewa na waziri huyo kwamba italipa deni lake kwa taasisi hiyo hapo Aprili 9.

Masharti ya IMF

Duru za Wizara ya Fedha zimesema Shirika la Fedha la Kimataifa IMF linataka Ugiriki lipunguze zaidi malipo ya pensheni na kupandisha kodi yake ya thamani kama sehemu ya mageuzi ya kiuchumi.

Bendera ya Umoja wa Ulaya (kushoto) ikipepea sanjari na bendera ya Ugiriki.
Bendera ya Umoja wa Ulaya (kushoto) ikipepea sanjari na bendera ya Ugiriki.Picha: Reuters/Y. Behrakis

Ugiriki imekuwa ikitegemea mikopo ya mabilioni ya dola kuinusuru isifilisike jambo ambalo limewaathiri vibaya sana wananchi wa kawaida ambao imebidi wavumilie kupunguzwa kwa mafao yao ya kustaafu na mishahara pamoja na kuongezewa kodi.

Licha ya makubaliano ya serikali ya nchi hiyo na wakopeshaji wake serikali imekuwa ikiburuza miguu kutekeleza mageuzi ya kiuchumi ambayo yangeliweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo na uwezo wake wa ushindani.

Wakati wa mahojiano Varoufakis amesema ufumbuzi wa matatizo ya Ugiriki utapatikana ndani ya Umoja wa Ulaya na kufuta uvumi kwamba serikali yake inaweza kutafuta wakopeshaji kutoka nje ya Umoja wa Ulaya kama vile China au Urusi.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa

Mhariri: Hamidou Oummilkheir