1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa umoja wa nchi za Kiarabu hausaidii raia Syria

Sekione Kitojo12 Januari 2012

Mjumbe wa zamani wa kundi la uchunguzi la umoja wa nchi za Kiarabu amesema kuwa wachunguzi kadhaa wa umoja huo wameondoka Syria ama huenda wakafanya hivyo hivi karibuni kwa sababu ujumbe huo umeshindwa

https://p.dw.com/p/13iKz
Waandamanaji wakiandamana nchini Syria kuupinga utawala wa rais Bashar al-Assad
Waandamanaji wakiandamana nchini Syria kuupinga utawala wa rais Bashar al-AssadPicha: Reuters

Makundi ya upinzani nchini Syria yamesema kuwa wachunguzi ,ambao wamepelekwa nchini humo Desemba 26 mwaka jana kuangalia iwapo Syria inaheshimu mpango wa amani wa umoja wa mataifa ya Kiarabu , wamempa Assad muda zaidi tu kukandamiza maandamano ambayo yamezuka hapo March mwaka jana , yakitiwa nguvu na vuguvugu la maandamano ya umma katika mataifa mengine ya Kiarabu.

Wajumbe wa uchunguzi wajitoa

Anwar Malek , raia wa Algeria ambaye amejitoa katika ujumbe huo wa uchunguzi wiki hii, amesema kuwa wengi wa wajumbe wenzake wanakubaliana na msimamo wake.

Siwezi kueleza idadi , lakini ni wengi. Iwapo utazungumza nao , hasira yao ni dhahiri, ameliambia shirika la habari la reuters kwa simu, na kuongeza kuwa wengi hawawezi kuondoka kwasababu ya amri kutoka katika serikali zao.

Amesema kuwa mtaalamu wa masuala ya sheria kutoka Morocco , mfanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada kutoka Djibouti na Mmisri pia wamejitoa kutoka ujumbe huo.

Kuondoka kwao hakukuweza mara moja kuthibitishwa, lakini mjumbe mwingine , ambaye ameomba kutotajwa jina , ameliambia shirika hilo la habari kuwa anapanga kuondoka Syria leo Ijumaa. Ujumbe huo hauna faida kwa raia, amesema na kuongeza, hausaidii chochote.

Umoja wa mataifa ya Kiarabu , ambao unasikiliza ripoti kamili kutoka kwa ujumbe huo hapo Januari 19, umegawanyika kuhusiana na suala hilo la Syria, wakati Qatar inakosoa zaidi na Algeria inatetea hatua zilizochukuliwa na serikali ya Syria.

Ujumbe huo, wa kwanza wa aina yake kufanywa na umoja wa mataifa ya Kiarabu , unaongozwa na jenerali kutoka Sudan Mohammed al-Dabi, ambaye ameshutumiwa na makundi ya haki za binadamu kutokana na jukumu lake katika mzozo wa Darfur.

Hillay Clinton ashutumu hotuba ya Assad

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amesema jana kuwa ujumbe huo wa uchunguzi hauwezi kuendelea milele na kupuuzia hotuba ya Assad siku ya Jumanne kuwa ni ya kipuuzi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Rodham Clinton
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Rodham ClintonPicha: AP

Assad alivunja ukimya wa miezi sita na kujitokeza hadharani siku ya Jumanne akiushambulia umoja wa mataifa ya Kiarabu , Arab league ambao umesitisha uanachama wa Syria Novemba mwaka jana kuhusiana na jinsi ilivyoshughulikia ghasia nchini humo zilizosababisha umwagikaji wa damu.

Assad avunja ukimya

Assad amelaumu ghasia hizo kwamba zimesababishwa na magaidi ambao atawaadhibu kwa mkono wa chuma. Mzozo nchini Syria , ambapo wapiganaji wamejiunga na kile kilichoanza kama harakati za amani kumaliza utawala wa miaka 41 wa familia ya Assad, umesababisha vifo vya zaidi ya watu 5,000, kwa mujibu wa makadirio ya umoja wa mataifa. Serikali imesema wanajeshi wake 2,000 pamoja na polisi wameuwawa tangu wakati huo.

Rais Bashar al Assad akiwahutubia wafuasi wake mjini Damasvus
Rais Bashar al Assad akiwahutubia wafuasi wake mjini DamascusPicha: picture-alliance/dpa

Shutuma za Malek zinatoa pigo zaidi kwa ujumbe huo ambao maafisa wa Syria wamekuwa kwa muda mrefu wakiupinga.Malek ambaye kwa sasa yuko nchini Qatar , amesema kuwa matumizi ya nguvu yanayofanywa na jeshi la Syria yameendelea bila kukoma wakati akiwa mjini Homs. Waziri mkuu wa Qatar Sheikh Hamad bin Jassim al-Thani , ambaye anaongoza kamati ya umoja wa nchi za Kiarabu kuhusu Syria , amesema kuwa hali ya shaka inaendelea kukua juu ya uwezo wa ujumbe huo wa uangalizi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Saumu Yusuf