1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Marekani wawasili nchini Pakistani

Tuma Provian Dandi16 Novemba 2007

Katika kile kinachoelezwa ni kupoza makali ya utawala wa Rais Perves Musharraf, ujumbe wa Marekani leo umewasili nchini Pakistani kwa ajili ya kusuluhisha siasa za nchi hiyo

https://p.dw.com/p/CIlf
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Negroponte
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John NegropontePicha: AP

Ujumbe wa Marekani ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Bwana John Negroponte, umewasili mjini Islamabad nchini Pakistani kwa ajili ya kupoza makali ya siasa za Rais Perves Musharraf, baada ya malalamiko ya wananchi kuwa makubwa.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri wa Marekani inalenga kutoa shinikizo dhidi ya Rais Musharraf kuondoa hali ya hatari aliyoitangaza tangu mwanzoni mwa mwezi huu, iliyosababisha vurugu, vifo na majeruhi wengi nchini Pakistani.

Wanasiasa kutoka upande wa upinzani wametoa mwito kwa ujumbe huo wa Marekani kuibana serikali ya Rais Musharraf na ikibidi kuikatia misaada inayopata ikiwa itashindwa kurejesha demokrasia na kuondoa hali ya hatari.

Tangu kuanza kwa vurugu hizo, Marekani imekuwa kimya kutoa tamko lolote kutokana na urafiki wa karibu kati ya Rais George Bush na Musharraf.

Wapakistani wanaituhumu serikali ya Rais Musharraf na maofisa wenzake wa kijeshi kwa kufuja misaada ya pesa zinazolewa na Marekani kwa manufaa yao binafsi huku wakiwakandamiza raia wenzao kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.

Hali hiyo imemshushia umaarufu Rais Perves Musharraf kama anavyoeleza Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Bibi Benazir Bhutto, aliyeachiwa huru leo hii baada ya kuzuiwa nyumbani kwake kwa kipindi cha juma moja.

O-Ton Bhutto

#Hakuna mazungumzo tena na Rais Musharraf. Na sasa umaarufu wake umeshuka yeyote atakayeshirikiana naye ni sawa na kujilisha sumu, zamani alikuwa mtu mzuri lakini hivi sasa anatapatapa#

Bibi Bhuto ambaye amejipatia umaarufu mkubwa tangu aliporejea nyumbani mjini Karachi akitokea uhamishoni katika falme za Kiarabu mwezi uliopita, amesema kwa sasa hayuko tayari kushirikiana na utawala wa Jenerali Musharraf.

Kiongozi huyo anayeongoza chama cha Pakistani Peoples Party, amesikitishwa na jinsi serikali iliyoko madarakani inavyotumia pesa za wananchi na misaada kubana demokrasia na kukuza mauaji, huku haki zote za kiraia zikikaliwa na watu wachache.

Wapakistani wanataka misaada hiyo itumike kwa mipango iliyokusudiwa, ikiwemo kuwapa wananchi usalama wa uhakika, utawala bora pamoja na kuinua uchumi wa nchi hiyo.

Kuhusu ujumbe wa Marekani nchini Pakistani kukutana na kambi ya upinzani akiwemo Bibi Benazir Bhutto mwenyewe, hakuna dondoo zozote zilizotolewa.

Ujumbe huo wa maofisa wa Marekani umewasili nchini Pakistani zikiwa zimepita saa chache tangu kuapishwa kwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo Bwana Mohammedmian Soomro, aliyepewa jukumu la kusawazisha mambo na kuandaa uchaguzi wa Bunge utakofanyika tarehe tisa Januari mwaka ujao.

Bwana Soomro, amechukua nafasi ya Shaukat Aziz aliyekuwa akishikilia wadhifa wa Uwaziri Mkuu wa Pakistani.