Ujerumani yawakamata washukiwa watatu wa ugaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yawakamata washukiwa watatu wa ugaidi

Ujerumani imewakamata wanaume watatu wanaoshukukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi ambao walipania kuushambulia uwanja wa ndege wa Frankfurt na kambi kubwa ya jeshi la Marekani.

Uwanja wa ndege wa Frankfurt

Uwanja wa ndege wa Frankfurt

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, amesema wanaume hao wamekuwa wakipanga kufanya mashambulio katika uwanja wa ndege wa Frankfurt na kambi ya jeshi la Marekani ya Ramstein. Aidha waziri Jung amesema kitisho cha kufanyika mashambulio hayo kilikuwa dhahiri. Waziri huyo ameongeza kusema kwamba vyombo vya usalama nchini Ujerumani vimefanya kazi nzuri na hawezi kusema mengi zaidi kwa wakati huu.

´Ninataka kwanza kuwahakikishia kwamba vyombo vyetu vya usalama vimefanya kazi nzuri kufanikisha kukamatwa kwa washukiwa. Inadhihirisha pia kwamba watu hao ni hatari na nawaomba munielewe kwamba katika hali hii sipendi kusema lolote.´

Uwanja wa ndege wa mjini Frankfurt, ni mojawapo ya viwanja vilivyo na shughuli nyingi barani Ulaya, na kambi ya Ramstein ya jeshi la Marekani, hutumiwa kuratibu harakati za jeshi la Marekani nchini Irak na Afghanistan.

Katika taarifa iliyotolewa kabla mkutano na waandishi habari hii leo, ofisi ya muendeshaji mkuu wa mashtaka mjini Karlsruhe amesema operesheni imefanywa katika miji mbalimbali ya Ujerumani. Taarifa hiyo imesema waongozaji mashtaka wa Ujerumani waliamuru jana wanaume hao watatu wa kundi la kigaidi la kiislamu wakamatwe na watafikishwa mahakamani baadaye leo.

Washukiwa wote watatu wana mafungamano na Pakistan na wamekuwa wakijaribu kufanya majaribio na vifaa vya kulipuka na kutengeneza mabomu ya kutega ndani ya magari.

Imeripotiwa kwamba vifaa vinavyoweza kulipuka vimepatikana ndani ya nyumba moja katika mji wa jimbo la kaskazini la Hesse. Duru zinasema mpango wa kufanya mashambulio hayo mjini Frankfurt ulikaribia kukamilika. Chanzo kingine cha habari kimeripoti kwamba risasi zilifyatuliwa wakati polisi walipoivamia nyumba moja katika jimbo la North Rhine Westfalia.

Televisheni inayomilikiwa na serikali ya Ujerumani, Sudwestrundfunk, imewanukulu maafisa wa polisi mjini Berlin wakisema washukiwa wawili ni raia wa Ujerumani waliosilimu na mmoja alikuwa na pasi ya kusafiria ya Pakistan. Hata hivyo ripoti nyengine zinasema mshukiwa wa tatu anamiliki pasi ya Uturuki na Ujerumani.

Mbunge mashuhuri Wolfgang Bosbach amesema njama ya kuushambulia uwanja wa ndege wa Frankfurt na kambi ya jeshi la Marekani ilipangwa ifanyike sambamba na kumbukumbu za mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Msemaji wa jeshi la Marekani barani Ulaya mjini Stuttgart, Kapteni Jeff Gradeck, amesema bado hawajapokea habari zozote kuhusu kambi zao kulengwa katika mashambulio ya kigaidi. Hakuna taarifa yoyote iliyotolea na maafisa wa uwanja wa ndege wa Frankfurt.

Kukamatwa kwa washukiwa watatu nchini Ujerumani kumefanyika siku moja baada polisi nchini Denmark kuwakamata waislamu wanane wanaoshukiwa kuwa na njama ya kupanga shambulio la bomu na kuwa mafungamano na kundi la kigaidi la al Qaeda. Ujerumani, ambayo ina wanajeshi wake nchini Afghanistan, imekuwa katika hali ya tahadhari kufuatia vitisho vya mashambulio.

 • Tarehe 05.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH8T
 • Tarehe 05.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH8T

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com