1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatoa muongozo mpya kuhusu Afrika

16 Juni 2011

Serikali ya Ujerumani imepitisha mkakati mpya kuhusu sera zake kuelekea bara la Afrika, unaoshadidia aina ya mashirikiano yanayojikita katika uimarishaji wa amani na kuinua uchumi wa bara hilo masikini kabisa duniani

https://p.dw.com/p/11arS
Kansela Angela Merkel anasoma muongozo mpya kuhusu Afrika kabla haujafikishwa mbele ya baraza la mawaziriPicha: dapd

Alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Guido Westerwelle, aliyewasilisha muongozo kuhusu sera ya serikali kuu ya Ujerumani kuelekea bara la Afrika. Muongozo huu mpya kuelekea Afrika ulishakuwa tayari umetajwa katika waraka wa kuunda serikali ya muungano kati ya CDU/CSU na Waliberali wa FDP mnamo mwaka 2009.

Kwa kutangaza muongozo kuelekea bara la Afrika, serikali kuu ya Ujerumani imedhamiria kufungua ukurasa mpya katika ushirikiano pamoja na bara la Afrika na kuanzisha ushirika sawia kati ya pande hizo mbili, amesema hayo waziri wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle, na kuongeza:

"Kwa kupitisha muongozo kuhusu Afrika, inamaanisha tunalilenga bara lote la Afrika, jambo hilo linahitaji moyo wa kijasiri, lakini pia tunabidi na tunataka kuwa na moyo wa kijasiri katika uhusiano wetu pamoja na bara la Afrika."

Westerwelle Afrika-Konzept
Waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle akifafanua muongozo mpya kuelekea AfrikaPicha: dapd

Lengo la kwanza lililotajwa katika muongozo huo ni "amani na usalama", hatua ambazo zinatakiwa ziimarishwe kwa kuzidisha uwezo wa mataifa ya Afrika kujiepusha na kumaliza migogoro katika daraja ya kimkoa. Zaidi ya hayo, serikali kuu ya Ujerumani inataka kusaidia kuimarisha demokrasia na mfumo wa mataifa yanayoheshimu sheria kwa kuwapatia mafunzo mahakimu na mawakili. Serikali kuu ya Ujerumani inapigania kuona adhabu ya kifo inabatilishwa, mitindo ya kuandamwa na kuadhibiwa mashoga inakoma na kuwepo usawa wa jinsia.

Lengo jengine la sera ya Ujerumani kuelekea Afrika linahusiana na namna ya kupalilia ukuaji wa kiuchumi na kulipatia bara la Afrika maarifa yanayotokana na nguvu za kiuchumi za Ujerumani.

Südafrika thermische Solaranlage
Bibi huyo wa Afrika kusini aweka mtambo wa kunasa nishati ya juwa juu ya paa la nyumba yakePicha: picture-alliance/dpa

Serikali kuu ya Ujerumani inapanga kuhimiza wajasiria mali wa Ujerumani wawekeze barani Afrika, pamoja na kusaidia kuinua miundo mbinu barani humo. Muongozo huyo mpya unazungumzia pia haja ya wajasiria mali wa Ujerumani kuwekeza katika sekta ya nishati na mali ghafi, pamoja na kuendelezwa mbinu za kubuni nishati mbadala.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,/reuters

Mhariri: Miraji Othman