1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yasita kuhusu vikwazo vipya dhidi ya Iran

Kalyango Siraj19 Septemba 2008

Rais Nejad hajali

https://p.dw.com/p/FLSs
Fundi katika kiwanda cha Uranium karibu na mji wa TehranPicha: AP

Marekani na Ufaransa zinataka vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran viwekwe hara ili kuiwezesha nchi hiyo kukubali miito inayoitaka kusitisha shughuli zake za kinyuklia.

Hata hivyo Ujerumani kwa upande wake imenyamaa kimya kuhusu suala hilo.

Wakati mataifa ya magharibi yakitaka Iran kuwekewa haraka vikwazo zaidi,Ujerumani kwa upande wake inasitasita

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani,Jens Ploetner,amesema kuwa Berlin baado inapendelea kujadiliana na Tehran.

Alipoulizwa kuhusu vikwazo dhidi ya Iran msemaji huyo amesema kuwa Umoja wa Ulaya baado unaendeleza mazungumzo na Iran na kutaraji kuwa kutapatikana matunda mazuri.

Ameongeza kuwa ikiwa mazungumzo hayo hayatazaa matunda yoyote yale,serikali ya Ujerumani inaamini kuwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndipo litakapokuwa njia bora wakati huo na mazunguzo lazima yafanyike kuona kama kunahitajika maazimio mapya.

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani, amesema kuwa Berlin inasikitishwa na ripoti iliotolewa jumatatu na shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomic.

Ripoti hiyo ilisema kuwa Iran haijasimamisha shughuli zake za kurutubisha madini ya Uranium kama ilivyoagizwa na Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani amesema kuwa waziri Frank-Walter Steinmeier amesisitiza umuhimu wa kulimaliza suala hilo mapema wakati wa mazungumzo yake na cheo somo wake wa Iran Manouchehr Mottaki siku ya jumatatu.

Ujerumani ni sehemu ya mataifa sita duniani yanayojaribu kuishawishi Iran kuachana na mpango wake wa Nuklia kwa kuipa vishawishi .

Marekani,ambayo inahofia kuwa Iran inajaribu kutengeneza bomu la Nuklia,dai linalokanushwa na Tehran,imeiambia jumatatu kuwa, itawekewa vikwazo vipya na Umoja wa Mataifa ikiwa haitaachana na mpango wake wa Nuklia. Ufaranza nayo iliunga mkono onyo hilo.

Nae rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad,amekariri kuwa Tehran haiwezi kuachana na mpango wake wa kurutubisha madini ya Uranium.Pia hakujali vikwazo zaidi dhidi ya nchi yake.

Na hayo yakiarifiwa nchini Iran kwenyewe,kiongozi wa kidini wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei amemlaumu msaidizi wa rais wa Iran,Esfandier Rahim Mashaie,kwa matamshi yake kuwa nchi hiyo ni rafiki kwa watu wa Israel.

Akisema kuwa matamshi hayo sio kweli,ameishutumu Israel kwa kile alichosema kuwa imechukua maisha ya wapalestina kama vile nyumba zao,ardhi, mashamba pamoja na biashara zao.