1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapania kuupiga vita ukimwi

Oummilkheir8 Machi 2007

Serikali kuu ya Ujerumani imepania kutoa kipa umbele kwa juhudi za kupambana na ukimwi ulimwenguni.Juhudi hizo zinashika nafasi ya mbele pia wakati huu ambapo Ujerumani ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya.

https://p.dw.com/p/CHIf
Waziri wa afya wa serikali kuu ya Ujerumani Ulla Schmidt
Waziri wa afya wa serikali kuu ya Ujerumani Ulla SchmidtPicha: AP

Jana bunge la shirikisho limepitisha mkakati wa kinga dhidi ya ukimwi .Mkakati huo umelengwa kulifikia lengo la millennium,la kuzuwia kuenea ukimwi ulimwenguni hadi ifikapo mwaka 2015.

Maradhi ya ukimwi yameenea kwa kasi katika kipindi cha miaka 25 iliyopita na kuwaletea majonzi mamilioni ya watu kote ulimwenguni.Tangu yalipochomoza hadi wakati huu maradhi hayo hatari yameshagharimu maisha ya watu milioni 30,mamilioni ya watoto wamegeuka yatima,au wamewfiwa na mmoja kati ya wazee wao wawili.Idadi ya wanawake wanaoambukizwa ukimwi inazidi kuongezeka kote ulimwenguni.

Miongoni mwa hatua mpya na muhimu katika kupambana na ukimwi,zilizodhihirisha kuleta tija katika mwaka 2006,ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapatiwa njia za kujikinga na maradhi hayo,wanapata tiba na kuhudumiwa-kutiliwa mkazo huduma za wakinamama na haki zao pamoja na kuimarishwa mfumo wa afya.

Ukimwi na virusi vya HIV si tatizo linaloukumba ulimwengu wa tatu tuu,anasema waziri wa afya wa serikali kuu ya ujerumani Ulla Schmidt.Nchini Ujerumani pia watu wanazidi kuambukizwa na maradhi hayo.

“Mwaka uliopita,watu 2700,wake kwa waume wameambukizwa na la kutisha zaidi hapa ni kwamba licha ya mikakati madhubuti tuliyo nayo,idadi ya wanaoambukizwa inazidi kuongezeka.Sababu mojawapo ni kwamba watu wanazidi kupuuza hatari iliyopo,kwasababu wengi wanaamini kwamba mchanganyiko wa madawa sio tuu unamrefushia mtu maisha,bali unaponyesha hasa.”

Waziri wa afya wa serikali kuu ya Ujerumani ametahadharisha dhidi ya hisia kama hizo akisisitiza bado ukimwi unaendelea kuangamiza maisha ya binaadam.Waziri wa afya Ulla Schmidt amesema maelezo yatazidishwa hasa kuelekea yale makundi yanayokabiliwa na hatari ya kuambukizwa ukimwi.

Mpango wa kimkakati ulioidhinishwa na baraza la mawaziri unazungumzia juu ya kutengwa yuro milioni 12 na laki tatu-yuro milioni tatu zaidi ikilinganishwa na hapo awali.

Katika daraja ya kimataifa Ujerumani inapanga kuongeza kwa tuhuluthi moja fedha msaada wa kupambana na maradhi hayo ya kuambukiza kwa maneno mengine yuro milioni 400.

Waziri wa misaada ya maendeleo Heidemarie Wiezorek-Zeul anasema msaada huo ni wa lazima watu wakitilia maanani pekee mwaka jana watu karibu milioni tatu wamefariki dunia kwasababu ya ukimwi.

Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya ujerumani Heidemarie Wiezoreck Zeul anaendelea kusema:

“Mwishoni mwa mwaka 2006,watu milioni 40 wameambukizwa.Na kusini mwa bara la Afrika kuna watoto yatima ambao idadi yao ni sawa na idadi ya watoto wanaoishi nchini Ujerumani,yaani watoto milioni 15.Mtu anaona kwa jinsi gani maradhi haya ya kuambukiza ni hatari-hasa barani Afrika,ingawa kwengineko pia katika nchi za ulimwengu wa tatu hali pia inatisha.”

Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani anahisi juhudi za kupambana na ukimwi zitagharimu muda,hata hivyo anasema matumaini yameanza kuchomoza baada ya bei za madawa kupungua kwa karibu asili mia 90 tangu mwaka 2000.