1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaongoza kundi C

Sekione Kitojo
10 Oktoba 2016

Mabingwa wa dunia Ujerumani inaongoza katika kundi C baada ya michezo mwili ya kufuzu katika fainali za kombe la dunia

https://p.dw.com/p/2R5gv
Fußball WM-Qualifikationsspiel Deutschland Tschechien in Hamburg
Picha: picture alliance/dpa/M. I. Güngör

Mabingwa  wa  dunia  Ujerumani  yaongoza kundi  lake  la  C baada  ya  kupata  ushindi  katika  michezo  yake  miwili  ya  mwanzo ya  kufuzu  kucheza   fainali  za  kombe  la  dunia mwaka  2018  nchini  Urusi. Kesho Jumanne(11.10.2016)  itapambana  na Ireland ya  kaskazini.

Ujerumani  iko  katika  njia  salama  kuelekea  kuutetea  ubingwa  wake  wa  kombe  la  dunia  mwaka  2018  nchini  Urusi  baada  ya  kuiangusha  jamhuri  ya  Czech  kwa  mabao  3-0  siku  ya  Jumamosi  mjini  Hamburg. Kikosi  hicho  cha  kocha  Joachim Loew  kilionesha  tangu  mwanzo  kuwa  nani  ni  mwenye  nyumba  mjini  Hamburg  na  mashabiki  walijionea  kandanda  safi  kutoka  kwa  kikosi  hicho. Kocha  wa  Ujerumani  Joachim Loew  anathibitisha hayo  kwa  kusema.

"Nilikuwa  na  furaha  tele,  kwa  sababu  kikosi  changu  tangu  mwanzo kilikuwa  na  udhibiti  kamili  wa  mchezo  huo. Ulikuwa  ni  mchezo  mzuri   sana  wachezaji  wakionesha  mchezo  wa  hali  ya  juu  na  kupata  mabao  matatu, ambayo waliyapata  kwa  ushirikiano  mzuri sana, ndio , nilifurahi  sana."

Fußball WM-Qualifikationsspiel Deutschland Tschechien in Hamburg
Mshambuliaji Thomas Mueller akipachika bao la pili kwa Ujerumani mjini Hamburg dhidi ya Jamhuri ya CzechPicha: picture alliance/dpa/D. Bockwoldt

Mkurugenzi  wa  Die Mannschaft  Oliver Bierhoff   alionesha  furaha  kwa  kusema  kikosi  cha  timu  yake  kimeweza  kuudhibiti mchezo  na  kupata  mabao ya  uhakika.

"Ilikuwa  hali  ya  kuonesha  nguvu  tuliyonayo, na  ilikuwa  hali  nzuri. Na  nafikiri, kwamba   timu ilifanya  vizuri  tangu  mwanzo  hadi  mwisho. Waliweza  kucheza  kwa  ushirikiano  na  kujisikia raha  uwanjani , na  kuudhibiti  mchezo  mzima. Na  hii  inajionesha  katika  viwango. Ilikuwa  muhimu , kwamba  baada  ya  michuano  iliyopita  ya  kufuzu, ambayo  haikuwa  mizuri  kwetu, sasa  tunawapa  burudani  mashabiki  wetu."

Fußball WM-Qualifikation - Deutschland Joachim Löw während der Pressekonferenz
Kocha wa Die Mannschaft , timu ya taifa ya Ujerumani Joachim LoewPicha: picture-alliance/dpa/Daniel Bockwoldt

Mapambano  zaidi ya Ulaya

Kesho Jumanne (11.10.2016)Ujerumani  itajitupa  tena  uwanjani  mjini  Hannover  kupambana  na  Ireland  ya  kaskazini timu  ambayo  mara  kadhaa  huipa  kibarua  Die Mannschaft, lakini  mara  hii  kocha  Joachim Loew  amesema  kikosi  chake  kiko  imara  kuwaweka  mahali  wanapostahili  Ireland  ya  kaskazini. Katika  kundi  C pia  Norway  iliyobugia  mabao  3-0 dhidi  ya  Ujerumani  katika  mchezo  wa  kwanza  mwezi  uliopita, itajitupa  uwanjani  kuwania  pointi  tatu  dhidi  ya  San Marino, wakati  Jamhuri  ya  Czch  inapambana  na  Azebarjain.

Leo  Jumatatu(10.11.2016)  kuna  mapambano  mengine  barani Ulaya  kuwania  kufuzu  kucheza  katika  fainali  hizo, ambapo Ureno  iko  nyumbani  kwa  visiwa  vya  Faror, Uswisi  inapambana  na  Andora, Ubelgiji  iko Gibraltar , Bulgaria  inapambana  na  Sweden  na  Ufaransa   ina  kibarua  kigumu  dhidi  ya  Uholanzi. Mlinda  mlango  wa  Ufaransa  Hugo Iloris amesema  huo  utakuwa  mchezo  mgumu  sana  kwa  Ufaransa  leo.

Fussball WM-Qualifikation Niederlange gegen Weißrussland
Mchezaji wa Uholanzi (Njano) akijaribu kumpita mlinzi wa BelarusPicha: Reuters/United Photos/T. Kluiters

"Waholanzi  wana  wachezaji wengi  ambao  wanaweza  kubadilisha  mabo, hususan  katika  eneo  la  kati, mchezaji  mmojawapo  ninayemfikiria  na  ambaye  ni  muhimu  sana  katika  timu  hiyo ni Kevin Strootman , ambaye  alikuwa  majeruhi  na  sasa  amerejea  uwanjani , lakini  pia  washambuliaji wako  na  kasi  sana na  wanaweza  kusababisha  madhara katika  mapambano  ya  mtu  na  mtu, lakini  kwa  jumla, timu  ya  Uholanzi  ina penda  kumiliki  mpira na  watafanya  hivyo, ni  timu ambayo  ina  wachezaji  wengi  wenye  vipaji na  kwa  hiyo  tunapaswa  kuwa  waangalifu sana kesho."

Ufaransa  na  Uholanzi  zinaingia  katika  mchezo  huo  mjini  Amsterdam wakiwa  na  rekodi  zinazofanana  katika  kundi  A.Kila  timu  ina  pointi 4  baada  ya  michezo miwili , kila  timu  ilishinda  mabao 4-1 na  wako  sawa  kwa  pointi na  tofauti  ya  magoli. 
Kocha  Didier Deschamps , ambaye  ikosi  chake  kilifikia  fainali  ya  kombe  la  Ulaya  mwaka  2016, alizungumza  na  vyombo  vya  habari  na  kusema. 

"Huu ni utamaduni  wa  kandanda  la  Uholanzi , kikosi chao ni cha  wachezaji  chipukizi  , lakini  wenye  vipaji, wanapenda  kuumiliki  mpira na  kushambulia, wana wachezaji  wenye  uwezo wa  kubadilisha mfumo  wa  mchezo na  hususan  washambuliaji. Kwa  hiyo  utakuwa  mchezo tofauti  kabisa kuliko siku  ya  Ijumaa kwa  Ufaransa  na  Uholanzi."

Frankreich Euro 2016 Finale Portugal ist Europameister Didier Deschamps
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier DeschampsPicha: Reuters/C. Platiau

Uturuki  ilizamishwa  jana  na  Iceland  kwa  kuchapwa  mabao  2-0  mjini Reykjavic  , wakati  Iceland  ikiimarisha  sifa  yake  ya  kuwa  moja  kati  ya  timu  ngumu  katika  bara  la  Ulaya  kuvunja  ujasiri  wao.
Katika  mchezo  wake  wa  kwanza  Iceland  ambayo  ilifikia  robo  fainali  ya  kombe  la  Ulaya  nchini  Ufaransa mwaka  huu , iliiangusha  Finland  kwa  mabao  3-2.

Waingereza waongoza

Uingereza  inaongoza  kundi  lake F  baada  ya  kushinda  michezo  yake  yote  miwili   ikiwa  na  pointi 6, licha  ya  kumbadilisha  kocha  wake  na  kuongozwa  na  Gareth Southgate baada  ya  kocha  wao  Sami Alerdice  kuachia  ngazi. Mlinda  mlango  Joe Hart  hata  hivyo  amesema  anatarajia  kwamba  Slovenia  watawaiweka  Uingereza  katika  mbinyo  mkali  wakati  timu  hizo  zitakapopambana  mjini Ljubljana  kesho  Jumanne.
Ushindi  dhidi  ya  Slovakia  na  Malta  umeiweka  Uingereza  juu  ya  msimamo  wa   kundi  hilo  F.

Gareth Southgate
Kocha wa mpito wa Uingereza Gareth SouthgatePicha: Imago/Eibner Europa

Mlinzi  wa  Uhispania  Gerard Pique  amepata  uungwaji  mkono  kutoka  kwa  kocha  wa  kikosi  hicho Julen Lopetegui pamoja  na  shirikisho  la  kandanda  la  Uhispania  baada  ya  kutangaza  nia  yake  ya  kuachana  na  timu  ya  taifa  baada  ya  kombe  la  dunia  mwaka  2018.

Pique atangaza kuiacha timu ya taifa

Mlinzi  huyo  wa  timu  ya  Barcelona , ambaye  ameichezea  timu  ya  taifa  ya  Uhispania  mara  86 na  kushinda  kombe  la  dunia  na   ubingwa  wa  mataifa  ya  Ulaya  na timu  hiyo, alisema  ukosoaji  kila  mara  kutoka  kwa  mashabiki  na  vyombo  vya  habari , umeua furaha  ya  kuichezea  Uhispania,  baada  ya  ushindi  wa  mabao 2-0 jana  Jumapili  dhidi  ya  Albania.

FIFA World Cup 2018 - Qualifikationsspiel zwischen Spanien und Albanien mit Gerard Pique
Mlinzi wa timu ya taifa ya Uhispania Gerard Pique (Kushoto)Picha: AFP/Getty Images

Pique  ambaye  alizomewa  na  mashabiki  wa  Uhispania  mwaka  jana, alisababisha  mijadala  katika  mitandao  ya  kijamii kwa  kuvaa  jezi  yake  dhidi  ya  Albania  ambapo mikono  ya  jezi  yake  ilikatwa, na  kuonekana  kwamba  aliondoa  beji inayoonesha  nembo ya  mistari  miekundu  na  njano rangi  za  Uhispania.
Kocha  wa  Uhispania  Lopetegui  amesema  anahisi kumuunga  mkono  mlizi  huyo.

China bado kidogo

Kutokuwepo  kwa  China  kwa  muda  mrefu  katika  eneo  la  juu  katika  soka  la  kimataifa kunaonekana  kutaendelea  kwa  takriban  miaka  mingine  sita  ijayo isipokuwa  pale  tu  Gao Hongbo  atakapoleta  mabadiliko  makubwa  katika  majaaliwa  ya  nchi  hiyo  baada  ya  mwanzo  mbaya  kabisa  katika  duru  ya  mwisho  ya  kufuzu  kucheza  katika  kombe  la  dunia.
Wakati  hatua  zinazopewa  hamasa  na  rais Xi Jinping  kuibadili  nchi  hiyo  kuwa  moja  ya   nchi  zilizoko  katika  nafasi  za  juu  katika  sekta  ya  soko  la  michezo  zikishika  kasi  zaidi, na  timu zenye  utajiri  mkubwa  wa  fedha  zinaendelea  kunawiri, hakujakuwa  na  mabadiliko  kwa  timu  ya  taifa.
Matumaini  matatu  ya  Xi kwa  soka  la  Uchina  ni  kwamba  nchi  hiyo  ifuzu  kucheza  katika  fainali  nyingine  za  kombe  la  dunia  baada  ya  kujitokeza  kwa  mara  ya  kwanza  mwaka  2002, iwe  mwenyeji  wa   fainali  za  kombe  la  dunia  na  hatimaye  ishinde  kombe  hilo.
Baada  ya  michezo mitatu  kati  ya  10  katika  duru  ya  mwisho ya  mchujo  kwa  mataifa  ya  bara  la  Asia  kwa  ajili  ya  fainali za  mwaka  2018, hata  hivyo, China  ina  pointi  moja  tu  kutokana  na  sare  ya  bila  kufungana  na  Iran.

Hong Kong vs China Fußballspiel
Wachezaji wa China wakipambana na Hong KongPicha: picture-alliance/dpa/V. Fraile

Kipigo cha  bao 3-2  dhidi  ya  Korea kusini  kilitarajiwa  lakini  haikutarajiwa  kupata  kipigo  cha  bao 1-0  dhidi  ya  Syria  siku  ya  Alhamis, na  ina  maana  mpambano  wa  kesho  Jumanne  dhidi  ya  Uzbekistan  ni  lazima  China  ishinde iwapo itataka  kulazimisha  kuwa  moja  kati  ya  timu zinazoweza  kushika  nafasi  za  juu  katika  kundi  hilo  hali  ambayo  itawapeleka  Urusi  kwa  fainali  hizo.

Barani Afrika , Nigeria kidedea

Kwa  upande  wa   bara  la  Afrika Nigeria  iliiangusha  Zambia  jana  Jumapili  kwa  mabao  2-1 ,  katika  kundi  B. Nigeria  imeanza  juhudi  hizo  na  mapema  katika  kundi  lao  gumu  ambapo  Algeria  na  Cameroon zilitosheka  na  sare  ya  bao 1-1  mjini  Blida. Congo  ilikubali  kipigo  cha  bao 1-0 dhidi  ya Misri , wakati  Tunisia  iliishinda Guinea  kwa  mabao 2-0 nyumbani  jana  Jumapili.
Duru  nyingine  ya  mchujo  katika  bara  la  Afrika  itafanyika  mwezi  ujao lakini  duru nne  za  mwisho  zitafanyika  kati  ya  Agosti  na  Novemba  mwakani. Mshindi  wa  kila  kundi  kati  ya  makundi  matano atashiriki  katika  fainali  za  kombe  la  dunia  nchini  Urusi.

Großbritannien Manchester - Fussball Premier League - Manchester City vs Manchester United
Kelechi Eheanacho mshambuliaji wa Nigeria akipambana na Eric Bailly wa manchester United katika mchezo wa ligi ya UingerezaPicha: Getty Images/A. Livesey

Wakati  huo  huo  Libya  imemfuta  kazi  kocha  wake  mkuu  Javier Clemente  baada  ya  kipigo  kikubwa  mwishoni  mwa  juma. Shirikisho  la  soka  la  nchi  hiyo  limetoa  taarifa  hiyo , bila  ya  kutoa  maelezo, siku  moja  baada  ya  Libya  kukandamizwa  mabao 4-0  na  jamhuri  ya  kidemokrasi  ya  Congo  katika  kundi  A mjini  Kinshasa siku  ya  Jumamosi.

Na  katika  riadha:

Abel Kirui  wa  Kenya  alichanja  mbuga  na  kumpita  bingwa Dickson Chumba  katika  kilometa  za  mwisho  na  kushinda  mbio  za  Chicago Marathon   jana  Jumapili. Florence Kiplagat  wa  Kenya  pia  alishinda  nae  mbio  zake  za  pili  za  Chicago  Marathon   mfululizo  kwa  wanawake. Kirui  mwenye  umri  wa  miaka  34 alimaliza  mbio  hizo  za  maili 26.2  katika  muda  ambao  si  rasmi  wa  saa  2  dakika 11  na  sekunde 23.

Sport Leichtathletik WM Berlin Deutschland Marathon
Abel Kirui wa KenyaPicha: AP

Mpiganaji  ngumi  maarufu Aaron Pryor , akikumbukwa  kwa  mapambano  yake  makali  na  Alexis Arguello  wa  Nicaragua, alifariki  jana  akiwa  na  umri  wa  miaka  60  baada  ya  kuugua  muda  mrefu  ugonjwa  wa  moyo.
"Tunasikitika  sana na  tuna majonzi  kutangaza  kwamba  mpendwa  wetu  Aaron amefariki nyumbani  ikiwa  na  familia  yake, " Frankie Pryor , mjane  wake, alisema  katika  taarifa   nyumbani  kwa  familia  yake  karibu na Cincinati , Ohio.

Kwa  taarifa  hiyo  ndio  tunakamilisha  habari  hizi  za  michezo  jioni  ya  leo. Hadi  mara  nyingine  mimi  ni  Sekione  Kitojo , Kwaherini.


Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / rtre / dpae

Mhariri:  Mohammed  Khelef