1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yailaza Ureno 3:2

20 Juni 2008

Ujerumani imekata tiketi ya nusu-finali ya kombe la Ulaya.

https://p.dw.com/p/ENQx
Michael Ballack na timu yake.Picha: AP

Ulaya imeanza kutetemeka - wajerumani wamefufuka na hawataki kurudi nyumbani Juni 29 kutoka Vienna bila ya taji la 4 la kombe la Ulaya.Ujerumani jana ilikata tiketi yake ya nusu-finali baada ya kuichezesha Ureno na Christiano Ronaldo kindumbwendumbwe na mwishoe, kuipiga kumbo nje ya mashindano ´kwa mabao 3:2.

Leo ni zamu ya Wacroatia na waturuki kukata tiketi ya pili ya nusu-finali na kupanga miadi na Ujerumani jumatano ijayo-Juni 25.

Ilikua tena Lukas Podolski akishirikiana na chipukizi mwenzake Bastian Schweinsteiger,waliovuruga mchezo wa wareno pale Podolski alipotimka mbio na dimba wingi wa kushoto na kumuachia Schweinsteiger kupiga hodi katika lango la wareno na akaitikiwa. Haukupita muda, Schweinsteiger mara hii kupitia mkwaju wa freekick alipomlishia Miroslav Klose, kutia kichwa kwa bao la pili.Na kama katika mpambano wa kuania nafasi ya 3 ya kombe lililopita la dunia Ujerumani ilipocheza na Ureno,2006 ilikua Schweinsteiger aliewachimbia kaburi na kuwazika wareno.

Hivi ndivyo Lukas Podolski alietoa ile pasi maridadi iliongoza katika bao la kwanza alivyoueleza mchezo:

"Nadhani hakuna alietutarajia tungetamba kama tulivyotamba.Na baada ya mchezo ule inafurahisha zaidi kuona tumecheza uzuri na kustahiki kushinda."

Philip Lahm, beki mashuhuri wa Ujerumani anaependa kutia fora usoni kwa kasi alisema:

"Imani ndio kila kitu na timu yetu ilijiaamini na hasa jinsi ilivyotamba kipindi cha kwanza ilipocheza kwa ujasiri mkubwa ."

Nahodha wa Ujerumani pale ilipotwaa kombe la dunia 1974 na kocha 1990 Franz Beckenbauer,alikua na pongezi nyingi kwa timu ya Ujerumani kama sie alidai kabla kuwa Ujerumani haingefua dafu mbele ya wareno.Katika makala yake katika toleo la leo la gazeti mashuhuri la BILD alisema, "Taifa zima linafurahia ushindi wa jana usiku wa mabao 3-2 dhidi ya Ureno.

Beckenbauer akaongeza,

"Kuishinda Ureno ni kuishinda timu iliotamba uzuri katika kombe hili kuliko nyengine yoyote duru ya kwanza.Lakini, mara nyingi hutokea hivyo, timu zinazofyatua mizinga yao na mapema, hazifiki mbali."-alisema Beckenbauer.

Nae kocha wa Ujerumani aliefungiwa chumbani mbali na chaki ya uwanja kama adhabu na rifu pale Ujerumani ilipocheza na Austria Joachim Loew akielezea masahibu yaliompata huko juu alisema:

"Kutoka jukwaani uwanjani ,unapata msisimko zaidi lakini unajihisi upo mbali mno na kinachopita uwanjani.Unaona baadhi yanayopita uzuri kabisa,lakini kuwa mbali mno na timu yako kunaumiza kichwa."

Ikiwa moyo wa ujasiri wa kushinda Kombe huonekana katika duru hii ya pili ya kutoana-knockout stage- basi tumeiona jana Ujerumani ikitoa salamu kwa Uturuki au Croatia zinazocheza leo .

Gazeti la Guardian la Uingereza linasema timu hii ya Ujerumani hailingani na zile kali za zamani,lakini imerithi ukaidi wa kutosalim amri na mapema.

Maalfu ya wajerumani jana walishuhudia changamoto na Ureno iliochezwa mjini Basel,Uswisi na mitaa yote ilikuwa mitupu-watu wakiwa ama majumbani au mikahawani.

Ushindi wa jana dhidi ya Ureno baaada ya kuanza vibaya,kunatoa salamu kwa Holland inayocheza kesho na Urusi kuwa Ujerumani imefufuka.

Tusubiri jioni hii Croatia itakapocheza na Uturuki itatoa salamu gani.