1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaanza kwa kishindo kulitetea taji

5 Septemba 2016

Ujerumani imeanza kwa kishindo kikubwa kampeni ya kulitetea taji lake la ubingwa wa dunia, kwa kuichapa Norway magoli 3-0 Ugenini. Thomas Mueller amekiaga kipindi cha ukame wa magoli kwa kupachika mawili kimiani.

https://p.dw.com/p/1Jw94
Thomas Mueller akisherehekea bao lake
Thomas Mueller akisherehekea bao lakePicha: picture-alliance/AP Photo/J. O. Nesvold/NTB Scanpix

Ilikuwa mechi ya kwanza ya timu ya taifa ya Ujerumani, Die Mannschaft chini ya nahodha mpya, Manual Neuer, lakini kivutio kikubwa kilikuwa Thomas Mueller, aliyemaliza kipindi cha miezi 10 ya ukame wa magoli, kwa kuingiza magoli mawili na kung'ara katika mechi hiyo.

Goli la Mueller katika dakika ya 16 ya mchezo lilikuwa lake la kwanza kwa timu ya taifa tangu Oktoba 2015. Goli hilo liliingia baada ya purukushani mbele ya lango la Norway, ambalo kipa Rune Jarstein hakuweza kulidhibiti vyema. Goli la pili la Mueller, na la tatu kwa Die Mannschaft usiku wa Jumapili, lilitinga wavuni mnamo dakika ya 60 ya mchezo, na kuvunja matumaini ya Norway kuambulia chochote katika mechi hiyo.

Joshua Kimmich, nyota ya siku za usoni

Kijana anayetarajiwa kung'ara siku za usoni, beki wa Bayern Munich Joshua Kimmich pia aliandika jina lake kwenye ubao wa magoli, kwa kuífungia Ujerumani goli la pili mnamo dakika ya mwisho kabisa ya kipindi cha kwanza.

Joshua Kimmich, kijana anayetiliwa matumaini siku zijazo
Joshua Kimmich, kijana anayetiliwa matumaini siku zijazoPicha: picture alliance/augenklick/GES/M. Ibo Güngör

''Tungeweza kushinda magoli mengi zaidi ugenini'', alisema Mueller baada ya mechi, na kuongeza kuwa hata hivyo, wanaridhika na namna walivyoanza michuano hii kuwania nafasi ya kushiriki kombe la dunia la mwaka 2018, litakalochezwa nchini Urusi.

Thomas Mueller ambaye hakufanya vyema katika fainali za Euro Juni iliyopita, alisifiwa na kocha wake Joachim Loew, kama mchezaji anayeibuka wakati wa mashindano yanayohusu kombe la dunia.

''Bila shaka magoli haya yatasaidia kumuongezea kujiamini, na kumwezesha kupata mengine zaidi mnamo wiki chache zijazo'', alisema Loew akimaanisha Thomas Mueller.

England nayo yaanza vyema

England nayo ilianza vizuri katika kundi F kwa kuishinda Slovakia goli moja kwa sufuri. Ingawa England iliudhibiti mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho, ilisubiri hadi dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza kupata bao lililofungwa na Adam Lallana.

Wayne Rooney, nahodha wa timu ya England
Wayne Rooney, nahodha wa timu ya EnglandPicha: picture alliance/Back Page Images

Awali, kocha Sam Allardyce ambaye hii ilikuwa mechi yake ya kwanza kama kocha wa England, alikuwa amesema angeridhika iwapo timu yake ingetoka sare ugenini.

Uganda yaondoa jinamizi la miongo minne

Barani Afrika, timu 16 zitakazoshiriki fainali za Kombe la Afrika la Mataifa (CAN) mwaka 2017 nchini Gabon zimekwishajulikana. Gumzo kubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni kufuzu kwa timu ya taifa ya Uganda, Uganda Cranes, ambayo ilikata tiketi yake kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Comoro.

Mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Namboore mjini Kampala ilishuhudiwa na mashabiki zaidi ya 40,000 ambao walijawa na furaha kupita kiasi baada ya timu yao kufaulu kuingia fainali za CAN kwa maara ya kwanza katika muda wa miaka 39.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef