1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kutoa euro bilioni 1 kusaidia Syria

John Juma
25 Aprili 2018

Wawakilishi zaidi ya 80 wa nchi, mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa, wanakutana mjini Brussels Ubelgiji kwa siku ya pili kujadili mustakabali wa Syria. Ujerumani imeahidi kutoa euro bilioni moja kusaidia Syria

https://p.dw.com/p/2wcKT
Belgium Treffen der Geldgeber für Syrien
Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Umoja wa Ulaya umezihimiza Urusi na Iran kuishinikza Syria ishiriki katika mazungumzo ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, wakati ambapo wafadhili wa kimataifa wakiahidi kutoa mabilioni ya dola kuwasaidia raia ambao wamezingirwa kwenye machafuko hayo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, amesema Urusi na Iran ambazo ni washirika wa karibu wa rais wa Syria Bashar al-Assad zina jukumu la kusaidia kumaliza vita vya Syria ambavyo vimedumu kwa miaka minane sasa.

Wawakilishi zaidi ya nchi 80, mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa, wanakutana mjini Brussels Ubelgiji kwa siku ya pili kujadili mustakabali wa Syria. Hii ni baada ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuonya kuwa kuna kitisho cha kutokea janga baya la kibinadamu katika eneo la Idlib ambalo linadhibitiwa na waasi.

Mogherini: Suluhisho la kisiasa chini ya mchakato wa Umoja wa Mataifa linahitajika

Eneo la Idlib linadhibitiwa na waasi nchini Syria
Eneo la Idlib linadhibitiwa na waasi nchini SyriaPicha: picture alliance/ZUMAPRESS/Edlib

Akizungumza baada ya kuwasili Brussels katika mkutano wa kujadili mustakabali wa Syria, Mogherini amesema wanaamini kuwa njia pekee ya kupata amani ya kudumu nchini Syria ni kupitia suluhisho la kisiasa chini ya mchakato wa Umoja wa Mataifa.

"Syria si ubao wa kuchezea chess kwa mataifa makubwa. Syria ni ya watu wa Syria na leo tutahamasisha kwa upande mmoja, uungwaji mkono wa kisiasa ili kuwe na mchakato wa kisiasa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa , mbao ndio muktadha pekee ambapo suluhisho la kisiasa kwa Syria, linaweza kupatikana”

Ulaya pia inalenga kutumia mkutano huo kuanzisha upya mazungumzo yaliyoongozwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva, lakini ambayo yamepata matokeo finyu katika awamu zote nane. Hii ni kwa sababu kwa kiwango fulani, serikali ya Rais Assad haijaonesha nia kamili kushiriki katika mazungumzo hayo.

Urusi yakosoa kutoshirikishwa kwa Syria katika mkutano

Hata hivyo balozi wa Urusi katika Umoja wa Ulaya Vladimir Chizhov amesema wawakilishi wa serikali ya Syria walipaswa kualikwa katika mkutano huo wa kuchangisha fedha.

Rais wa Syria Bashar al-Assad akiwa amezingirwa na wanajeshi wake mjini Damascus
Rais wa Syria Bashar al-Assad akiwa amezingirwa na wanajeshi wake mjini DamascusPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/Syrian Presidency

”Ninafikiri ni kosa, walipaswa kualikwa. Tunazungumzia namna ya kushughulikia mahitaji ya watu wa Syria, hivyo kunapaswa kuwe na mtu anayewawakilisha watu wa Syria”

Mara kwa mara Urusi imekuwa ikiikingia kifua Syria katika Umoja wa Mataifa, kisa cha hivi karibuni kikiwa ni dhidi ya madai ya nchi za magharibi kwamba utawala wa Rais Assad ulifanya shambulizi la silaha za sumu mjini Douma.

Umoja wa Mataifa umesema jumla ya dola bilioni 9 zinahitajika mwaka huu kutoa misaada ya kiutu nchini Syria na kuwasaidia wakimbizi katika nchi jirani.

Uingereza na Ujerumani zimetoa ahadi zao leo huku Ujerumani ikisema itatoa zaidi ya euro bilioni moja.

Takwimu za Umoja wa mataifa zinaonyesha kuwa, watu milioni 6.1 ambao hawana makao nchini Syria wameikimbia nchi hiyo na wengine milioni 13, miongoni mwao watoto milioni 6 wanahitaji misaada

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga