1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani Iwajibike Zaidi Ulimwenguni

3 Februari 2014

Mkutano wa kimataifa kuhusu Usalama na mjadala kuhusu kuwajibika zaidi Ujerumani katika majukwaa ya kimataifa, pamoja na hotuba ya waziri mkuu wa Uturuki Racep Tayyip Erdogan mjini Berlin magazetini

https://p.dw.com/p/1B1om
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani akihutubia mkutano wa Usalama mjini MunichPicha: picture alliance/abaca

Tuanzie lakini kusini mwa Ujerumani,mjini Munich ambako mkutano wa usalama wa kimataifa umemalizika na mjadala kuzidi kupamba moto kuiona Ujerumani ikiwajibika zaidi katika majukwaa ya kimataifa.Gazeti la "Mittelbayerische" la mjini Regensburg linaitathmini hotuba ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck katika mkutano huo na kuandika:"Si haki kumsingizia mkuu wa kasri la Bellevue,Joachim Gauck eti anataka kuchanganya masuala ya kijeshi katika siasa ya nje ya Ujerumani.Masuala ya kina aliyoyazusha rais wa shirikisho mjini Munich yanahusiana zaidi na mchango we siku za mbele wa Ujerumani katika medani ya kimataifa.Haki ya kukaa kando na kutofanya lolote Ujerumani iliyokuwa ikiitumia kwa miongo kadhaa kutokana na sababu za kihistoria,haifai tena hivi sasa anahisi rais Gauck.Na hajakosea hata kama matokeo ya hali hii si ya raha, ni ghali na yana madhara yake.

Ujerumani iangalie wapi kusaidia

Maoni sawa na hayo yametolewa pia na mhariri wa gazeti la "Nordwest" la mjini Oldenburg anaeandika:"Mabishano kuhusu miito ya kuitaka Ujerumani iwajibike zaidi siku za mbele hayana kikomo; yanaanzia "Ujerumani ijiandae hadi kufikia kutumwa jeshi la Ujerumani Bundeswehr katika pembe tofauti za dunia".Hata kama ni sawa kuiona dola kuu la kiuchumi barani Ulaya likiwa na usemi katika siasa ya nje,wakati huo huo lakini ni kosa na pengine hata si vizuri kudai wanajeshi wa Ujerumani ,washirikishwe siku za mbele katika nyanja za mapigano ulimwenguni.Kujitoa Ujerumani katika hali ya kukaa kando isilinganishwe hata kidogo na jukumu la kupigana.Lakini pia kuwaachia washirika pekee jukumu la kulinda amani,ni kinyume na fikra ya mshikamano,na kutokana na kuzidi majukumu ya Marekani,Ufaransa na Uingereza ni shida kuhakikisha ufanisi wa majukumu hayo.Hata hivyo serikali kuu ya Ujerumani itakuwa inafanya la maana kama itapima kwanza wapi panahitajika msaada zaidi.

Waziri mkuu wa Uturuki Berlin

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu hotuba itakayotolewa kesho na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyib Erdogan mjini Berlin.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika:Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kuhutubia mjini Berlin kesho jumanne.Mada inahusu"Uturuki,Ulaya na Ulimwengu katika karne ya 21".Lakini waziri mkuu wa Uturuki anataka kuzungumzia nini hasa?Yeye mwenyewe hajui kina msubiri kitu gani wiki zinazokuja.Hajawahi hata mara moja kuuna wezani wake wa nguvu bungeni ukimomonyoka katika kipindi chote cha miaka 11 madarakani.Wingu jeusi limetanda katika chama chake cha AKP,hali ya kisiasa haikadiriki na uongozi wa serikali yake unawekewa suala la kuuliza.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman