1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani haitishwi na Italia

1 Julai 2016

Ujerumani watakutana ana kwa ana na adui ambaye kawaida huwakosesha usingizi katika mashindano ya kimataifa. Italia. Ni mchuano unaotarajiwa kwa hamu wa robo fainali ya dimba la Euro 2016 mjini Bordeaux

https://p.dw.com/p/1JHXP
Deutsche Fußballnationalmannschaft Frankreich Evian UEFA EURO 2016
Picha: picture-alliance/dpa/A.Dedert

Mabingwa hao wa dunia wameshindwa kila mchuano wa hatua ya mchujo na Waitalia kwa karibu kipindi cha nusu karne lakini mara hii wana matumaini kuwa wanaweza kuweka kikomo laana hiyo. Walishindwa na Italia katika fainali moja ya Kombe la Dunia mwaka wa 1982 na nusu fainali mbili za Kombe la Dunia (1970, 2006) na pia hatua ya nusu fainali ya Euro 2012. Hata hivyo beki wa Ujerumani Jerome Boateng anasema hawana kiwewe chochote "Sote tunajua Italia imeonyesha uwezo wake, hasa katika dimba hili. Imekuwa imara na isiyopendeza kucheza dhidi yake. Kwetu sisi, ni muhimu kutafuta njia ya kushinda. Na kucheza kama timu. Tunasubiri mchuano wa leo. Naamini utakuwa mchezo mzuri. Na tunataka kushinda.

UEFA EURO 2016 Achtelfinale Italien vs. Spanien
Ujerumani inalenga kuishinda Italia kwa mara ya kwanza katika dimba la kimataifaPicha: Reuters/C. Hartmann

Na ni kweli kwamba kuna dalili kuwa huenda mara hii ukawa ni wakati wa Wajerumani kutabasamu, kwa sababu hadi kufikia sasa katika dimba hili hawajafungwa bao hata moja. Ujerumani iliikandika Italia 4-1 katika mchuano wa kirafiki mwezi Machi lakini meneja wa timu Oliver Bierhof anasema matokeo hayo hayana umuhimu wowote katika mchuano wa leo "Labda timu ya Italia ni imara zaidi kuliko 2012. Mwaka huo walikuwa na Balotelli ambaye alikuwa hatari kwetu, lakini sasa wamejipanga sana na wagumuna hivyo tuko makini. Lakini tunaanza upya na kilichotokea nyuma sio muhimu kwetu.

Timu ya Italia chini ya kocha Antonio Conte haina majina makubwa ya zamani lakini ni miongoni mwa timu nne ambazo hazikushindwa katika michuano ya kufuzu na imeendelea kupata matokeo mazuri katika dimba hili, kwa kufungwa bao moja tu katika mechi nne.

Safu yao ya ulinzi inayofahamika kama BBC, ikiongozwa na Giorgio Chiellini akicheza pamoja na wenzake wa Juventus Andrea Barzagli na Leonardo Bonucci, imekuwa nguzo muhimu katika mafanikio yao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef