1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani bado ipo kwenye mkwamo wa kisiasa

Saumu Mwasimba
1 Desemba 2017

Kansela Merkel na kundi lake washindwa kupata jibu la SPD juu ya kuanza rasmi mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya muungano

https://p.dw.com/p/2oapw
Berlin Angela Merkel, Horst Seehofer und Martin Schulz
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Rais Frank Walter Steinmeier  nchini Ujerumani alikutana na viongozi wa kundi la wahafidhina la vyama vya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU, linaloongozwa na Kansela Merkel na chama cha Social Democratic SPD. Mkutano huo ulilenga  kujaribu kutafuta njia za kuumaliza mkwamo wa kisiasa na hatimae kuunda serikali ya pamoja.Hata hivyo mazungumzo hayo yanaelekea hayakuzaa matunda.

Waziri wa mambo ya nje akitokea chama cha SPD Sigmar Gabriel alisema wazi kwamba chama chake hakitoridhia kirahisi kuingia katika serikali nyingine ya muungano na kundi la Kansela Angela Merkel.Akizuungumza na shirika la habari la Ujerumani ZDF Gabriel alisema  watu hawapaswi kukitarajia chama chake ambacho kwahakika bado kimo ndani ya serikali inayoondoka ,kukubali haraka kujiunga kwa mara nyingine na serikali ya muungano na vyama vya CDU na CSU kutokana na kushindwa kufikiwa makubaliano ya kuunda kile kilichoitwa serikali ya Jamaica.

Berlin - Steinmeier lädt zu GroKo-Gesprächen ein
Kasri la rais wa UjerumaniPicha: Getty Images/S. Gallup

Waziri huyo wa mambo ya nje pia anasema kwamba kwa hivi sasa ni juu ya wahafidhina kuonesha kile haswa wanachokitaka huku akiongeza kusema kwamba kundi hilo la Kanselsa Merkel limekaa chini kwa kipindi cha miezi kadhaa pamoja na wanamazingira au chama cha kijani na waliberali chama kinachopendelea biashara cha FDP bila ya kufanikiwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya pande tatu,na kwahivyo sasa ni wajibu wa kila mmoja kutowatia kishindo  SPD kukubali kuingia katika makubaliano ya kuunda serikali.

Kansela Merkel anajaribu kutafuta mshirika wa kuunda nae serikali tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu Septemba 24 ambako kundi lake la siasa za wastani za mrengo wa kulia kuonekana kuunga mkono mrengo wa siasa kali katika uchaguzi huo.Chama cha SPD ambacho kwa upande wake kimekuwemo ndani ya serikali ya Kansela Merkel kuanzia mwaka 2013 hadi sasa kilipata pigo kubwa katika matokeo ya uchaguzi huo,pigo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya chama hicho tangu baada ya vita vya pili vya dunia,kimepinga tangu mwanzo kujiunga tena na serikali ya muungano na Merkel.

Berlin - Steinmeier lädt zu GroKo-Gesprächen ein - Merkel u Seehofer
Picha: picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Lakini baada ya kiongozi wa chama hicho Martin Schulz kushinikizwa na rais Frank Walter Steinmeier ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje akiwa chama hicho cha SPD kubadili msimamo,alionekana kuwa tayari kujadiliana juu ya mwelekeo wa kuumaliza mkwamo huo wa kiasiasa.Hata hivyo baada ya hapo jana kukaa kwa masaa mawili kwenye mkutano na kundi la Merkel hakuna hatua yoyote kubwa iliyopigwa.Ingawa leo Ijumaa vyama vyote hivyo SPD ,CDU na CSU  vitakutana katika mkutano wa viongozi wa ngazi ya juu kujadiliana vipi kuendelea mbele ama wakubaliane kuunda serikali au kuitisha uchaguzi mwingine.Inatajwa lakini kwamba chama cha SPD hakitarajiwi kuridhia kuanza mazungumzo rasmi ya kuunda serikali hadi pale kitakapofanya mkutano wake mkuu wiki ijayo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo