1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yazungumzia maandamano nchini Syria

Admin.WagnerD27 Aprili 2011

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, amesema Rais Bashar Assad hawezi kuwa na uwezo wa kuongoza mabadiliko nchini mwake yanayoshinikizwa na waandamanaji.

https://p.dw.com/p/114gZ
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza,William HaguePicha: AP

William Hague anasema kiongozi huyo anaegemea upande mmoja wa utawala wake, na vilevile vile hana uhakika kama ataweza kufanikisha kwa uhuru agenda ya mabadiliko.

Waziri huyo alimtembelea Assad nchini Syria mapema mwezi Januari kwa mazungumzo.

Uingereza imeilaani serikali ya Syria kwa kitendo chake cha kukandamiza waandamanaji, lakini ikadokeza kwamba itachukua hatua tofauti na ile ya Libya.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje amesema hali ya mambo ni tofauti kwa kuwa Umoja wa Nchi za Kiarabu walitoa wito mataifa kuingia kwa vitendo dhidi ya Libya, zikisadiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

William Hague alisisitiza kwamba rais Assad bado ana nafasi ya kufanikisha mabadiliko ya kidemokrasia na kusema nchi yake itadumisha uhusiano wa kidiplomasia.

Aidha, kwa upande mwingine, wapinzani nchini Syria wamsema harakati zao za kimapinduzi zitauvunja utawala wa nchi hiyo ikiwa raisi Bashar hatotoa mwanya wa kuweko demokrasia.

Kauli hiyo ilitolewa na umoja wa wanaharakati wa upinzani nchini humo pamoja na wenzao walio nje ya nchi.

Wamesema mabadiliko ya kidemokrasia yatasadia kuilinda nchi kutoka katika kipindi cha machafuko,vurugu na vita vya wenywe kwa wenyewe.

Vurugu zilizoanza tangu katikati ya mwezi mwach zimesababisha mauwaji ya watu 400 nchini humo, huku kiasi ya watu 120 wakiuwawa katika kipindi cha mwisho wa wiki pekee.

Waandamanaji walikuwa wakishinikiza kuweko mabadiliko, lakini hivi sasa wameongeza madai kwa kutaka Rais Bashar Assad aondoke madarakani.

Bado hali si shwari. Serikali ya nchi hiyo imeendelea kutawanya vikosi vya askari katika mitaa ya mjii mkuu wa Damascus usiku wa kuamkia leo baada ya vifaru kushambulia raia katika mji mwingine uliopo kusini mwa nchi hiyo wa Deraa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza, Reutes, zaidi ya askari 2,000 walisambazwa katika mji wa Douma jana, na kuendeshwa ukaguzi wa vitambulisha katika vituo kadhaa.

Nayo Ufaransa imemwita balozi wa Syria nchini Ufaransa katika ofisi ya wizara ya mambo ya kigeni wake kwa mashauriano juu ya hali inavoendelea huko Syria.

Wachambuzi wa siasa za Syria wanasema nchi hiyo imekuwa ikitawaliwa kiukoo tangu enzi za baba wa Bashar, marehemu Hafez al-Assad, aliengia madarakani kwa mapinduzi 1970. Assad huyu wa sasa amerithi wadhifa kutoka kwa Baba yake.

Mwandishi: Sudi Mnette

Mhariri: Miraji Othman