1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yatoka sare na Mexico

Halima Nyanza28 Juni 2011

Hapo jana, siku ya pili ya michuano ya kombe la dunia la Soka la Wanawake, inayofanyika hapa Ujerumani, timu nne zilijimwaga uwanjani, Uingereza ikimenyana na Mexico wakati Japan ilipoikaba New Zealand.

https://p.dw.com/p/11kUu
Picha: picture-alliance/dpa

Katika mechi iliyochezwa katika mji wa Wolfsburg, shuti kali la mbali lililopigwa na Monica Ocampo, wa timu ya Mexico, katika dakika ya 33, lilikatiza matumaini ya Uingereza kutoka kifua mbele katika mpambano huo, na badala yake kutoka sare kwa kufungana bao moja kwa moja.

Akizungumzia bao hilo alilolifunga  Monica Ocampo ambaye alionekana kung'ara katika mchezo huo wa jana, alisema anamshukuru mungu kuweza kutikisa nyavu za Uingereza, kwani bao hilo ndilo lililowarudisha tena mchezoni.

Uingereza ndio iliyoanza kuliona lango la Mexico kwa goli lililofungwa na Fara Williams, katika dakika ya 21,toka kuanza kwa mechi hiyo.

Akizungumzia mchezo huo kocha wa timu ya Uingereza Hope Powell, amesema wamecheza vizuri lakini wanapaswa kucheza vizuri zaidi ili kuweza kubaki katika mashindano hayo.

Amesema wanajua kile wanachotarajia katika mchezo huo, na kuongeza kuwa wachezaji wake wanauzoefu wa kutosha hawana wasiwasi wowote, maana wanajiamini kwa kile wanachokifanya.

Na katika mpambano uliochezwa jana katika mji wa Bochum hapa Ujerumani, Japan iliianza vyema michuano hii ya kombe la dunia la soka la wanawake mwaka 2011, kwa kuibwaga New Zealand bao mbili kwa moja.

Frauen Fußball WM Japanische Nationalmannschaft
Kikosi cha JapanPicha: AP

Yuki Nagasato na Aya Miyama  ndio waliosababisha timu yao kutoka kifua mbele.

Bao la kufuta machozi la New Zealand lilifungwa na Amber Hearn.

Japan sasa inaongoza kundi B kwa kuwa na point tatu, ikifuatiwa na Mexico na Uingereza zenye points mbili kila moja, huku New Zealand ikishika mkia.

Wakati kundi A, wenyeji Ujerumani ambao pia ndio mabingwa watetezi wanaongoza, wakifuatiwa na Ufaransa na Canada huku Nigeria ikishika mkia bila ya points.

Na leo basi ni zamu ya kundi C, ambapo Sweden itavaana na Colombia, huku Marekani ikikutana na Korea kaskazini.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, afp, FIFA.com-FIFA women)