1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kujadili tatizo la wakimbizi Calais

31 Julai 2015

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anaongoza mkutano wa kamati ya serikali yake COBRA inayolishughulikia tatizo hilo leo (31.07.2015) huku polisi wa Ufaransa wakiwazuia wahamiaji wasiingie njia ya chini kwa chini.

https://p.dw.com/p/1G7ob
Frankreich Flüchtlinge am Eurotunnel Calais
Wakimbizi wakielekea njia ya Eurotunnel huko Frethun karibu na Calais (26.07.2015)Picha: Reuters/P. Rossignol

Kwa mujibu wa magazeti ya Uingereza, The Times na The Daily Telegraph, wizara ya ulinzi ya Uingereza pia inatafakari kuruhusu maeneo kadhaa ya ardhi yake yatumike kama eneo la muda la kuegesha malori kusaidia kupunguza foleni ndefu katika barabara ya Kent, kusini mwa England, kutokana na ucheleweshaji.

Waziri Mkuu Cameron alikosolewa vikali kwa matamshi yake kuhusu mzozo wa wahamiaji Calais aliyoyatoa akiwa ziarani nchini Vietnam kwa kuwafananisha wakimbizi na kundi kubwa la wadudu au ndege wanaotaka kuingia Uingereza kutafuta maisha mazuri na ajira.

Kaimu kiongozi wa chama cha Labour Harriet Harman alimshutumu Cameron kwa kutumia lugha ya uchochezi huku mgombea nafasi ya uenyekiti wa chama cha Labour Andy Burnham akisema kauli hiyo ni ya kufedhehesha. "Tunazungumzia binaadamu hapa, si wadudu," alisema kiongozi wa chama cha Liberal Democratic, Tim Farron.

David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza David CameronPicha: Reuters/T. Melville

Anna Musgrave, Meneja Utetezi wa shirika linalotetea masilahi ya wakimbizi, Refugee Council, alisema maneno aliyotumia Cameron ni ya kutowajibika. "Nafikiri inavunja moyo sana kusikia waziri mkuu akitumia lugha ya aina hiyo ya kutojali na ya kudhalilisha. Nadhani hajapewa taarifa sahihi. Anatakiwa aonyeshe uongozi mzuri katika kulishughulikia tatizo hili. Atumie lugha ya heshima na kuwajibika badala ya kuchochea hofu.

Naye Lisa Doyle, Mkuu wa Utetezi wa shirika hilo alisema, "Kauli ya namna hii ni ya uchochezi wa hali ya juu na inakuja wakati ambapo serikali inatakiwa kuelekeza nguvu zaidi katika kushirikiana na nchi nyingine za Ulaya kutafuta njia muafaka ya kuushughulikia mzozo huu wa kibinaadamu."

Doyle pia alisema Uingereza inajivunia utamaduni wa kuwakaribisha wakimbizi na ni muhimu sana utamaduni huu ulindwe wakati wa mzozo.

Onyo juu ya maamuzi ya kibaguzi

Mjumbe maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya uhamiaji, Peter Sutherland, alionya kwamba Uingereza inakabiliwa na kitisho cha kuchukua hatua za kibaguzi katika kuutatua mzozo wa wahamiaji katika bandari ya Calais, baada ya waziri mkuu Cameron kuahidi kuwarejesha makwao wahamiaji wanaoingia nchini humo bila vibali.

"Madai ya Uingereza kuwafukuza wakimbizi wanaotaka kuboresha hali yao kiuchumi ni hatua ya kibaguzi kwa uhuru wa kutembea," alisema Sutherland.

Mjumbe huyo maalumu aidha amesema madai ya Cameron yametiwa chumvi na yalilenga kuchochea wasiwasi kuhusiana na idadi ya wahamiaji wanaoingia Uingereza.

LKW-Fahrer überprüfen ob sich Flüchtlinge in ihrem Laderaum versteckt haben
Madereva wa malori wakichunguza kama wakimbizi wamedandiaPicha: DW/B. Riegert

Watu zaidi ya 1,000 waliteremka katika njia za reli kwa miguu karibu na njia ya Eurotunnel mwendo wa saa tatu jana usiku, lakini wakazuiwa na polisi huku wengine 30 wakikamatwa. Takriban watu 3,000 kutoka mataifa yakiwamo Syria na Eritrea, wamepiga kambi katika bandari ya Calais kaskazini mwa Ufaransa na wanajaribu kuvuka kwenda Uingereza kwa njia isiyo halali kwa kudandia malori na treni.

Sharif Udin, mkimbizi kutoka Afghanistan aliyeko Calais, alisema, "Tunapenda kwenda Uingereza. Ni kuzuri. Na hapa maisha ni magumu kwa sababu tunalala nje barabarani, msituni. Kwa mtindo huu mambo ni magumu."

Ufaransa imeongeza idadi ya maafisa wa polisi huko Calais na ni wakimbizi wachache tu waliojaribu kuingia njia ya chini kwa chini usiku wa kumakia leo ikilinganishwa na siku zilizopita. Uingereza imeahidi paundi milioni 7 kuboresha waya wa seng'eng'e kukizunguka kituo cha treni cha Coquelles, kaskazini mwa Ufaransa.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/dpae

Mhariri:Daniel Gakuba