1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yakumbuka miaka 5 tangu mabomu ya Madrid kutokea

Thelma Mwadzaya11 Machi 2009

March 11, 2004 sio tu siku iliyotokea shambulio baya kabisa la kigaidi, ambalo Hispania iliweza kuathirika nalo, lakini pia nchi hiyo inaadhimisha mabadailiko makubwa katika sera

https://p.dw.com/p/H9hs
Gari la polisi lililowasafirisha washukiwa wa shambulio la mabomu ya MadridPicha: AP

Polisi na maafisa wa serikali waliokuwa wakifanya uchunguzi, kazi zao zikaongozwa na sheria mpya. Kwa mafanikio , zaidi ya watu 370 hadi sasa wamekamatwa nchini Hispania, kwa kuhusika na mtandao wa kigaidi wa kimataifa. Miaka mitano baada ya shambulio hilo la kigaidi , Hispania bado ni lengo la mashambulio zaidi na eneo muhimu. Hususan eneo la Katalani , linaonekana kuwa eneo la kukutana kwa wale wanaotaka kufanya ugaidi. Hali ya hatari haijakuwa kubwa kuliko hivi sasa, anasema mkuu wa polisi.


Hakuna mtu anayefahamu, kile ambacho kimo ndani ya majengo ya eneo moja kaskazini mashariki ya jiji la Madrid. Na kwa yule anayefahamu , ni aghalabu kuzungumzia lolote. Nyuma ya milango minene ya chuma katika majengo hayo ndiko kunakodunda moyo wa watu wanaopambana na ugaidi nchini Hispania. Hifadhi ya takwimu, taarifa za mada za jini, nyaraka zilizoghushiwa, mabaki ya mada za kutengenezea milipuko, pamoja na dazeni kadha za wanasayansi watafiti, ambao wote wanafanyakazi za tathmini.

Kwa hiyo kituo hiki cha taifa kinajaribu kuratibu hatua za kupambana na ugaidi, kama maafisa hao wanavyosema, kuwa mbele kila wakati kwa uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi. Kwa hiyo baada ya shambulio la March 11 2004 kitisho kwa Hispania kimekuwa kikubwa zaidi, anasema mkuu wa kitengo cha kupambana na ugaidi.''Kinadharia tunajikuta katika hali ya juu kabisa ya kitisho. Na ni dhahiri kuwa hali hiyo iko juu zaidi kuliko 2004.''



Hispania ni lengo kuu la magaidi wa Kiislamu, kwasababu hakuna video yeyote ya kundi la al-Qaeda ambayo haitoi onyo kwa nchi hiyo.


Takriban mashambulio matano yamezuiwa na polisi katika miaka iliyopita, mojawapo likiwa dhidi ya njia ya treni ya Metro katika mji wa jimbo la Katalania wa Barcelona. Kwa hiyo Hispania sio tu lengo la mashambulizi , lakini pia kuwa kituo muhimu cha magaidi, ambacho kinatumiwa kutayarisha mashambulio duniani kote, na uandikishaji wa wapiganaji wa Kiislamu, pamoja na kupatiwa mafunzo ya nadharia.

Mitandao mingi ya kigaidi ina mizizi yake katika jimbo hilo la Hispania, watu waliofanya mashambulio dhidi ya mji wa Bombay Novemba mwaka jana walitayarishwa na raia mmoja wa Pakistan, ambaye kwa miaka kadha alikuwa anadai kuwa ni mfanyabiashara ambaye amekuwa akiishi katika eneo la zamani la mji wa Barcelona. Katika eneo hilo ndipo ilipojengwa miundo mbinu, kama anavyoeleza mchunguzi Baltazar Garzon.

''Mitandao, nyaraka pamoja na kadi za kughushi za kuhifadhi takwimu, usafirishaji wa fedha, ambazo wanachama wa mitandao ya makundi mengine hupokea na kuzificha, hii ndio kazi kubwa, ambayo makundi haya ya kigaidi nchini Hispania yanajishughulisha zaidi.''


Baada ya shambulio la March 11, maafisa wa usalama nchini Hispania walianza kufanyakazi kwa ushirikiano. Wakati huo tayari kulikuwa na wataalamu 100, wakijishughulisha na magaidi ya Kiislamu, hii leo wingi wao ni mara 13. Wakati huo huo ushirikiano na mataifa mengine katika mapambano dhidi ya ugaidi ulianzishwa, kama anavyosema mwanasheria mkuu wa serikali Dolores Delgado.

''Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu sana. Kwasababu tunachunguza ushahidi mwingi, ambao unakuja kutokea nchi nyingine , na ni lazima watufahamishe kuhusu hilo.''


Lakini pamoja na hayo kazi ya kupambana dhidi ya ugaidi ni ngumu sana. Makundi yanakuwa madogo madogo yasiyotegemeana na yaliyojificha. Ndio sababu wale wanaofanyakazi ya kupambana dhidi ya ugaidi nchini Hispania hawataki kujidanganya, licha ya mafanikio yote waliyoyapata, hatari ya kutokea shambulio bado ipo juu kila wakati.