1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania, Ugiriki zakumbwa na maandamano

Admin.WagnerD26 Septemba 2012

Uhispania inajiweka sawa kutangaza bajeti ya mwaka 2013 inayoendana na mpango wa kubana matumizi ya serikali. Wakati bajeti hiyo ikisubiriwa, maandamano makubwa yamefanyika katika mji mkuu Madrid kulalamikia mpango.

https://p.dw.com/p/16Eh3
Waandamanaji wakikabiliana na polisi mjini Madrid
Waandamanaji wakikabiliana na polisi mjini MadridPicha: dapd

Bajeti hiyo yenye kuzingatia sera za kukaza mkwiji itatangazwa huku serikali ya Uhispania ikiwa imekabiliwa na shinikizo la masoko ya fedha kwa upande mmoja, huku maandamano ya wananchi mitaani yakiweka mbinyo kutoka upande mwingine.

Washirika wa Uhispania katika eneo linalotumia sarafu ya euro wamekubali kuipa nchi hiyo mkopo wa uokozi anaofikia euro bilioni 100, kusaidia sekta ya mabenki ambayo inakabiliwa na hasara, kutokana na matatizo ya kiuchumi yaliyoanza mwaka 2008. Serikali mjini Madrid inasema haihitaji kiasi chote hicho, ikisisitiza kwamba euro bilioni 60 zinatosha.

Vipengele muhimu vya bajeti hiyo ambayo itawekwa wazi kesho Alhamis vinajulikana tangu mwezi Julai. Serikali inataka kuokoa euro bilioni 150 kati ya mwaka 2012 na 2014, ikianzia na euro bilioni 39 mwaka kesho.

Kukusanya fedha hizo, itabidi kuongeza kodi na kupunguza matumizi katika sekta za afya na elimu. Lakini, mpango huo haupokelewi vyema na wananchi.

Polisi wakiwatawanya waandamanaji
Polisi wakiwatawanya waandamanajiPicha: dapd

Maandamano makubwa Maelfu ya waandamanaji wametelemka katika mitaa ya mji mkuu Madrid usiku wa kuamkia leo, kuelezea kinaganaga kero wanalolipata, huku wakipaza sauti na kusema, 'aibu, jiuzulu' ''mikono juu, huu ni wizi''. Polisi walitumia risasi za mpira na virungu kuwatawanya waandamaji hao, ambao hawakubali kutimliwa kirahisi. Vitengo vya huduma ya dharura vimesema kwamba watu 60 walijeruhiwa katika maandamano hayo, 27 kati yao wakiwa maafisa wa polisi.

Baada ya mifukuzano na polisi, baadhi ya waandamanaji waliamua kukaa kwa utulivu katika uwanja ujulikanao kama Plaza Neptuno, huku wakitazamana uso kwa uso na polisi wa kutuliza ghasia waliopiga msitari mbele yao. Kabla ya hapo, baadhi ya waandamanaji walipata mkong'oto wa polisi, walipotaka kuvamia jengo la bunge.

Waandamanaji hao wanasema sera za serikali ya mhafidhina Mariano Rahoy za kupunguza mishahara na kuongeza kodi, zinawaumiza wananchi katika hali ambayo wanasema haifai.

''Tunao wanasiasa wengi kupindukia, na wanatumia pesa nyingi, na wanataka kutunyang'anya kila kitu'' Amesema mwandamanaji mmoja. ''Nimefukuzwa kazi, mme wangu bado yuko kazini, lakini sijui atabakia na ajira kwa muda gani, sijui.'' Amelalamika mwingine.

Wakati wa kampeni ya uchaguzi, waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy aliahidi kutoyagusa malipo ya uzeeni, ambayo yanafikia asilimia 25 ya matumizi ya serikali. Kutimiza ahadi hiyo kumesababisha mfumko wa bei wa kati ya asilimia tatu na tatu na nusu, hali ambayo haiyafurahishi masoko ya fedha.

Ugiriki nako hali si shwari

Wafanyakazi wanaofanya mgomo Ugiriki
Wafanyakazi wanaofanya mgomo UgirikiPicha: picture-alliance/dpa

Kwingine ambako mambo hayajatulia ni nchini Ugiriki, ambako kazi imesimama, kutokana na mgomo ulioitishwa na vyama vya wafanyakazi, kupinga hatua zaidi za kujibana mkanda.

Maandamano hayo yamefuatia onyo la Mkuu wa Shirika la Fedha ulimwenguni IMF, Christine Lagarde, kwamba kadri mageuzi ya kiuchumi yanavyozidi kucheleweshwa, ndivyo matatizo ya kifedha yatakavyokithiri.

Migomo miwili mikubwa ya wafanyakazi ilifanyika nchini Ugiriki mwezi Februari, lakini mgomo huu ni wa kwanza kuijaribu serikali ya mseto inayoongozwa na waziri mkuu Antonis Samaras, ambayo ilichukua madaraka mwezi Juni.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman