1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri:Leo tarehe 20 Machi ni mwaka wa nne tangu uvamizi wa majeshi ya Marekani nchini Irak.

Mohammed AbdulRahman20 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CHHs

Katika mkutano na waandishi habari mwishoni mwa mwaka jana, mwanasayansi mmoja kutoka chuo cha afya cha John Hopkins Bloomberg huko Baltimore-Maryland, aliwasilisha tarakimu kwamba takriban watu 655.000 wameuwawa katika vita vya Irak ,na kila siku idadi inaongezeka, huku mwisho wa vita hivyo ukiwa hauonekani.

Mwaka wa nne tangu vilipoanza vita vya Irak, bado kinachotawala ni vurugu na matumizi ya nguvu, huku Wamarekani wakikabiliwa na masuali kama kweli watamudu kuidhibiti hali hii, na iwapo bado Rais George W.Bush ataweza kulishawishi bunge-baraza la Kongresi- kuwa atashinda- Hayo ndiyo yanayohitajika zaidi.

Pale wademokrats waliposhinda uchaguzi wa Novemba na kuyadhibiti mabaraza yote mawili ya bunge, rais wa Marekani Bush alisema anataka washirikiane pamoja bila ya kusimama katika misingi ya kichama. Pia mdemokrat Nancy Pelosi, spika wa baraza la wawakilishi, alisema katika hotuba yake mwezi Januari kwamba wajumbe wa vyama vyote viwili hawana budi kuzingatia manufaa ya siku zijazo.

Kwa hilo la kushirikiana pamoja , hadi sasa halijapatikana. Wademokrat wamejaribu kuwasilisha azimio lao katika baraza la Seneti. Halafu mpango wa kugharimia vita mpaka sasa haujapata maridhiano ya kisiasa ya pamoja . Changa moto ya warepublican kwa upande mwengine imeshindwa kutoa nafasi ya kusonga mbele kisiasa, badala yake kinachoshuhudiwa ni kuongezeka idadi ya vifo na majeruhi.

Suala kuu ni mkakati wa kisiasa na kijeshi. Upande wa kijeshi kukiwa na waziri mpya wa ulinzi na kamanda mpya anayeongoza harakati za kijseshi Irak, matumaini ni kwamba hali hatimae itadhibitiwa.

Robert Gates anafuata sera nyengine kuliko mtangulizi wake Donald Rumsfeld, na ana sifa ya hali ya juu. Mbunge wa chama cha demokrat John Murtha, amependekeza kurudi nyumbani haraka kwa wanajeshi walioko Irak, tena kwa heshima na anasema Gates anapaswa kuielewa vyema zaidi hali ilivyo kuliko mtangulizi wake.

Binafsi waziri wa ulinzi amesema ushindi katika vita vya Irak hauwezi kupatikana kijeshi tu. Ni wajibu wa wairaki wenyewe, wanasaiasa wa Irak kusaka suluhisho kwa nchi yao. Lakini wamarekani sasa hawawezi tena kubeba jukumu hilo, kwa sababu ni dola ilioanzisha vita na inabeba dhamana ya hapa ilipoifikisha Irak.

Kwa hivyo muhimu kabisa ni kusaka njia muafaka kuleta suluhisho: Miongoni mwayo kuwapa mafunzo wanajeshi na polisi, kukarabati miundo mbinu, kuanzisha utaratibu wa kisiasa utakaoleta uchaguzi na katiba ya kweli.

Kiongozi wa tume ya pamoja ya wademokrat na warepublican, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje James Baker, amependekeza kujumuishwa kwa pande zote zinazohusika kisiasa na kijeshi katika kuleta suluhisho.

Ni miaka minne sasa tangu Marekani ilipovianzisha vita hivi. Bila ya kuzingatia makosa yaliofanyika na kukubali makosa kwa kusaka njia mpya, njia hiyo haiwezi kupatikana.

Bila shaka Marekani inataka kuona Irak ya kidemokrasi. Demokrasi maana yake ni kupatikana maridhiano. Wakati warepublikan na wademokrat nchini Marekani kwenyewe wanashindwa kuwa na maridhiano, vipi wanaweza kulitegemea hilo kwa wairaki ?