1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UHARIRI WA MAGAZETI YA UJERUMANI

B.Kuemmerling/P.Martin20 Februari 2008

Mada kuu iliyoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo Jumatano,tena ni kashfa ya kukwepa kulipa kodi ya mapato kwa kuficha pesa nchini Lichtenstein.

https://p.dw.com/p/DAMD

Kashfa ya kukwepa kulipa kodi kwa mamilioni imezusha mvutano mkubwa kati ya Ujerumani na Lichtenstein.Kiongozi wa taifa hilo,Mwana-mfalme Alois von und zu Liechtenstein amewatuhumu maafisa wa Ujerumani kuwa walikwenda kinyume na sheria na ametishia kuchukua hatua ya kuwashtaki waliohusika.Lakini serikali mjini Berlin imekanusha tuhuma hizo na kuonya kuwa itachukua hatua za kimataifa dhidi ya makimbilio ya kukwepa kodi.

Gazeti la SCHWARZWÄLDER BOTE kutoka Oberndorf limemnukulu mkuu wa taifa hilo dogo na kusema:

Mwana-mfalme huyo amefoka kweli.Kwani yeye anahisi kuwa "nchi hiyo ndogo" imeshambuliwa na "taifa kubwa la Ujerumani."Tangu maafisa wanaosaka watu wanaokwepa kulipa kodi kuanzisha msako mkubwa katika miji mbali mbali ya Ujerumani,Liechtenstein inahofia sifa yake kama mahala pa kufichiwa siri za pesa.Kwani utajiri wa taifa hilo dogo unatokana na taasisi zisizojulikana ambazo zimeundwa kwa pesa zilizotoroshwa,ili kuepuka kulipa kodi ya mapato.Sasa,dola hilo linakabiliwa na wakati mgumu,lasema Schwarzwälder Bote.

Na kutoka Munich gazeti la ABENDZEITUNG linasema:

Hapa,mtu anapaswa kukumbuka kuwa mfumo wa biashara wa taifa hilo dogo hasa unatoa nafasi ya kuficha pesa za magendo na rushwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.Na matajiri wasiotoshelelezeka wanasaidiwa kukwepa kodi na badala yake wale wenye mapato madogo ndio hulipia anasa zinazonufaisha umma mzima.Yadhihirika kuwa Mwana-mfalme huyo katika tuhuma zake alikuwa akitetea kundi hilo la matajiri,kwa hivyo wala asitiwe maanani lasema gazeti la ABENDZEITUNG kutoka Munich.

Tukibakia huko huko Munich gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linasema:

Familia ya Mwana-mfalme Alois von und zu Liechtenstein ambayo pia humiliki benki nchini humo inaona kuwa nchi hiyo ndio iliyofanyiwa udhalimu kwani habari za siri za benki zimenunuliwa kutoka nchi hiyo.Kwa maoni ya Mwana-mfalme huyo,maslahi ya kifedha yasigubike maadili ya kisheria ya nchi hiyo.

Hayo ni sawa,lakini nchini Lichtenstein maslahi ya kifedha na maadili ya kisheria ni mambo mawili yanayofungamana kwa sehemu kubwa.Kwani sheria ya nchi hiyo inatoa nafasi ya kuingiza mapato halali ya nchi zinginezo.

Tunamalizia kwa NURNBERGER ZEITUNG linalosema:

Nchi hiyo ndogo ya Liechtenstein ingebakia taifa masikini isipokuwa kwa benki na taasisi zake.Kwa hivyo mtu anaweza kumuelewa kiongozi wa nchi hiyo alipohamaki kuhusu kashfa ya Zumwinkel.Kwani kashfa hiyo,inahatarisha sifa ya Lichtenstein kama pepo ya watu wanaokwepa kulipa kodi ya mapato.Lakini ukweli huo ndio unampa haki Mwana-mfalme Alois von und zu Lichtenstein kuwatuhumu maafisa wa Ujerumani kuwa walikwenda kinyume na sheria waliponunua siri za benki zilizoibiwa? lauliza gazeti la Nürnberger Zeitung.